Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lowassa acharuka
Lowassa acharuka
By Habari Tanzania | Published  07/1/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Manyerere Jackton na Martha Mtangoo, Dodoma

WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amesema miezi sita baada ya Serikali ya Awamu ya Nne kuingia madarakani, imeona mengi, na amewataka wananchi wafumbe macho kwa hatua zitakazochukuliwa na serikali dhidi ya viongozi wafujaji.

 Katika hotuba yake ya kufunga mjadala wa bajeti ya ofisi yake mwaka 2006/2007, Lowassa, alisema kuna fedha nyingi zinazoliwa kwenye halmashauri mbalimbali nchini, na kwamba hatua zitachukuliwa.

Alisema Serikali za Mitaa ni eneo linalowagusa wananchi moja kwa moja, na kwamba madiwani wasidhani wanaandamwa kwa kuonewa, bali wanaandamwa kwa kuwa serikali inataka watekeleze wanayopaswa kutekeleza.

“Tunakiri kuna matatizo kadhaa katika halmashauri zetu, Serikali Kuu ni jukumu letu kusaidia kuyaondoa. Mwaka huu halmashauri zinapelekewa sh bilioni 700.

 “Uwajibikaji lazima uwepo, kuna baadhi ya wakurugenzi kila siku ni safari za Dar es Salaam, Dodoma, Arusha… safari tu, kuna matumizi makubwa na mabaya ya fedha.

 “Kuna watu kule (kwenye halmashauri), wamejipanga kupora, wanasadiana na viongozi, wakiwamo madiwani kadhaa. Hakuna taratibu nzuri za kudhibiti matumizi, hati chafu wanapewa walioshindwa kufunga hesabu... Mwaka jana walipata Mtwara, Handeni na Misungwi, kuna fedha ambazo hazikwenda... hata halmashauri zilizopata hati safi, kuna matatizo,” alisema.

 Waziri Mkuu alisema katika kukabiliana na matatizo hayo, Serikali Kuu imeamua kuchukua hatua kadhaa.

 Miongoni mwa hatua hizo ni kuwapo mkataba wa kazi kati ya halmashauri na Serikali Kuu, fedha zinazopelekwa, zifanye kazi zilizokusudiwa.

 Ameagiza kila halmashauri iwe na kamati ya kuhakiki miradi mbalimbali kwenye maeneo hayo.

 Kuhusu mifugo, Waziri Mkuu alizungumzia mifugo iliyoingizwa nchini kutoka nchi jirani, na ile iliyopo nchini.

Alisema mifugo yote imekuwa ikiharibu mazingira, na akatoa kauli kali kuhusu mifugo kutoka nchi jirani.

“Haiwezekani nchi yote ikawa malisho, Kagera na Kigoma kuna mifugo mingi kutoka nchi jirani imevamia. Kagera kuna mifugo 70,000 toka nje.

 “Tumechukua hatua za kuiondoa. Tumeondoa ng’ombe 50,000 kutoka Kagera, wamelalamika, vyombo vyao vya habari vimesema hatujali haki za binadamu, eti hatuna uungwana!

“Uungawana? Bunduki zilizokuja nchini hatuzioni? Sisi tumefunga macho, tumeamua mifugo iondoke, inaharibu mazingira yetu, ipo kwenye mapori yetu na misitu yetu.

“Hatuna ‘msalie Mtume’, hatujadiliani kutoondoa mifugo, bali kuipokea huko kwao, wanasema ardhi ni mali ya umma, ndiyo ni mali ya umma wa Watanzania, kama wanataka kuja, wafuate taratibu,” alisema.

Lowassa pia alisema msimamo wa serikali ni kuhakikisha mifugo inafugwa kwa kufuata taratibu zilizopo ili isiharibu mazingira.

Alisema hakuna njia nyingine mbadala, bali ni kukubaliana na uamuzi huo.

Alisema serikali haitaki kuwaona wafugaji wakiwa yatima katika nchi yao, na kwamba utafanywa utaratibu kwa mikoa yote, kuhakikisha wafugaji wanatengewa maeneo kwa kazi hiyo.

Kuhusu kilimo, alisema hiyo ndiyo ajenda ya pili, baada ya elimu inayopaswa kusimamiwa na viongozi katika ngazi zote. Alisisitiza kuwa, kiongozi yeyote atapimwa kutokana na utekelezaji wa ajenda hizo.

Waziri Mkuu alisema ni aibu na fedheha kwa Tanzania kuhemea chakula, ilhali ikiwa na nguvu kazi ya kutosha, mito na ardhi yenye rutuba.

Alisema imeanzishwa programu ya miaka saba, yenye thamani ya sh trilioni 2.5 kwa ajili ya kubadili kilimo nchini.

Waziri Mkuu alizungumzia uondoshaji kero ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam, na kumshangaa Waziri wa miundombinu, Basil Mramba, kwa kushindwa kwake kuanza upanuzi wa Barabara ya Sam Nujoma.

“Mramba hapa achangamke, mradi umechelewa, sioni kwa nini,” alisema.

Waziri Mkuu alikiri kwa kusema kwamba, msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ni mkubwa, hasa wakati wa ugeni wa kitaifa, na akasema hata yeye hujiona ni kero.

Yeye ni mmoja wa viongozi wachache wa kitaifa ambao misafara yao inapopita, magari na watumiaji wengine wa barabara hutakiwa kusimama kando.

Kuhusu Muungano, Waziri Mkuu alisema Watanzania wameridhika na mfumo wa sasa wa serikali mbili, na kwamba wanaotaka tofauti hizo, ni baadhi ya watu kwa tamaa za uongozi.

Alisema kuujadili Muungano ni “ruksa”, lakini hakuna kuuvunja, kwani Watanzania wengi wanachojua ni Muungano kwa vile wamezaliwa na kukulia ndani ya Muungano.

Alikiri kuwa yapo matatizo ambayo yatamalizwa kwa mazungumzo. Alitoa mfamo wa nchi za Canada na Uingereza, ambazo alisema ingawa ziliungana zamani, bado zinaendelea kujadiliana katika nyanja kadhaa.

 “Muungano wetu ni imara na wa kupigiwa mfano duniani na Afrika, ni imara, tunaheshimiwa kwa sababu ya Muungano huu,” alisema.

Waziri Mkuu alisema baadhi ya malalamiko yanayopaswa kutatuliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa upande wa Zanzibar, yataanza kushughulikiwa baada ya kufanya mabadiliko katika sheria ya sasa iliyounda chombo hicho.

Alisema mabadiliko ya sheria hiyo yatawasilishwa bungeni mwaka huu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.