Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mudhihir anena
Mudhihir anena
By Marshy Abdu | Published  09/18/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
Mudhihir anena
na Moses Kisa na Abdilahi Daudi


MBUNGE wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir, amewataka Watanzania kutoihusisha ajali iliyosababisha akatwe mkono wake wa kuume na masuala ya kisiasa.

Aidha, mbunge huyo amesema ajali hiyo iliyotokea Lindi mjini mwishoni mwa wiki iliyopita ilikuwa ni mapenzi ya Mungu na haina uhusiano wa namna yoyote na hoja aliyoitoa bungeni dhidi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zuberi Zitto.

Mudhihir, mmoja wa wabunge wacheshi na wenye uhusiano wa karibu na wanahabari, aliyasema hayo jana kitandani kwake katika wodi ya Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), alikolazwa akiendelea kuuguza majeraha aliyoyapata katika ajali hiyo ambayo ilitokea baada ya gari alilokuwa akiliendesha kupinduka katika eneo la SIDO, Lindi mjini.

“Mungu ndiye mpangaji wa kila kitu, sipendi ajali hii ichanganywe na siasa au masuala ya Kabwe, kwani hayaingiliani kabisa na ajali niliyoipata,” alisema Mudhihir aliyeonekana akiwa amechangamka kuliko ilivyokuwa siku chache zilizopita.

Alisema anaamini hivyo kwa sababu binadamu yeyote mwenye akili timamu hawezi hata mara moja akamwombea mwenzake akapatwa na matatizo.

Mudhihir ndiye mbunge aliyetoa hoja ya kulitaka Bunge limuadhibu Zitto kutokana na hoja yake ya kumtuhumu Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kusaini mkataba wa mradi wa uchimbaji wa dhahabu huko Buzwagi akiwa nje ya nchi na kwa njia ya siri.

Hoja hiyo na Mudhihir iliungwa mkono na wabunge takriban wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ndipo Bunge likapitisha azimio la kusimamisha uwakilishi wa Zitto bungeni kwa muda wa miezi mitano hadi Januari mwakani.

Akizungumzia maendeleo yake kiafya, Mudhihir alisema kwa kiwango kikubwa maumivu makali aliyokuwa akiyapata hasa katika mkono wa kulia uliokatwa yamepungua na tayari alikuwa ameshaanza kufanya mazoezi ya viungo chini ya uangalizi wa daktari aliyemtaja kwa jina moja la Marealle.

Mbunge huyo aliyaelezea matibabu anayoyapata hapo tangu afikishwe hospitalini kuwa ni mazuri na ya kiwango cha juu, na akatoa shukrani kwa wote waliochangia kupata kwake nafuu wakiwamo madaktari, wauguzi na viongozi wa Bunge na serikali.

Mudhihir alisema alikuwa pia tayari wakati ukifika kuutekeleza ushauri aliopewa na watu mbalimbali akiwamo Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kwa kutaka aende nchini Ujerumani kupata matibabu zaidi, ikiwa ni pamoja na kuwekewa mkono wa bandia.

Mbali ya hilo, mbunge huyo alisema iwapo hali yake itaendelea kuimarika anatarajia kuwa ataweza kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na kikao kijacho cha Bunge kinachotarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Dodoma.

Mbunge huyo alisema wakati ukifika anatarajia pia kukamilisha ziara yake ya kutembelea kata zote zilizo katika jimbo lake baada ya kuzitembelea 10 na kubakiza tatu tu.

Alizitaja kata ambazo alikuwa hajazitembelea kuwa ni Mbanja, Mchinga na Kilolombwa.

Aidha, Mudhihir alisema mbali ya ajali hiyo kukwamisha ziara yake hiyo, tukio hilo limesababisha alazimike kuahirisha mitihani yake ya mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu Huria cha Dar es Salaam iliyokuwa ianze kufanyika Jumatatu wiki ijayo, Septemba 24 hadi Januari mwakani.

Hata hivyo alisema bado alikuwa anaamini kuwa pamoja na kuahirisha huko, atafanya vizuri kama ilivyokuwa wakati alipofanya mitihani yake ya mwisho.

Mbunge huyo aliyepata kuwa Naibu Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo katika Serikali ya Awamu ya Tatu, alitoa shukurani kwa waandishi wa habari kwa kuandika habari zinazohusu ajali yake, hivyo kuwezesha ndugu, jamaa na viongozi mbalimbali wa serikali kujua ukweli wa mambo kuhusu ajali hiyo.

Mudhihir, ambaye alipata ajali hiyo Septemba 13 mjini Lindi, akiwa katika ziara ya kutembelea jimbo lake, aliahidi kueleza kwa kina kuhusu ajali yake pindi atakapopona.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.