WAKATI Ligi Kuu ya Bara ikianza Jumamosi, washambuliaji wa kutumainiwa katika kikosi cha Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ na Joseph Kaniki, wako mbioni kutimkia nchini Afrika Kusini siku yoyote kuanzia leo.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya watu katika klabu hiyo, zinasema nyota hao wanakwenda ‘Bondeni’ kwa majaribio katika timu ya Free State.
Hata hivyo, habari zinasema mpango huo hata baadhi ya viongozi wanaufahamu, lakini wamegoma kutoa ruksa kutokana na umuhimu wa nyota husika katika kikosi cha timu hiyo.
Mbali ya kukabiliwa na Ligi ya Vodacom, iliyopangwa kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki hii, Simba pia inatakiwa kujiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika mapema mwakani.
“Unajua suala hili ni kweli, lakini kumekuwa na msigano kwa sababu kipindi hiki ni kigumu kutokana na mashindano yanayoikabili Simba,” kilidokeza chanzo chetu.
Kama viongozi wa Simba wangeridhia suala hilo, wachezaji hao wangeondoka siku yoyote kuanzia sasa kwani tayari timu hiyo iliyo ligi kuu nchini humo, inawahitaji kwa majaribio.
Timu hiyo ndiyo anayokipiga kinara wa mabao wa ligi hiyo kwa sasa, Diyo Sibisi akiwa na mabao manne.
Juhudi za kumpata Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali, hazikuzaa matunda, lakini Mweka Hazina Msaidizi, Chano Almasi, alisema hakuna mchezaji atakayeruhusiwa kuondoka.
Alisema suala la mchezaji kupata timu ya kucheza nje ya nchi, ni fahari kwa mchezaji husika, klabu na nchi, lakini kwa sasa Simba inakabiliwa na mashindano.
“Silifahamu hilo, lakini hata kama lipo, kipindi hiki si kipindi cha kuondokewa na wachezaji kwani Ligi Kuu iko jirani, hivyo si wakati muafaka” alisema Chano.
Mbali ya Simba kukabiliwa na mashindano, pia wachezaji husika wana mkataba wa kukipiga Simba kwa msimu huu, hivyo wanapaswa kuitumikia klabu hiyo.
“Hawa ni wachezaji wetu, hivyo hawawezi kuondoka kwa sasa kwa sababu si wakati muafaka na tuna mkataba nao,” alisema Chano.
Haruna ni miongoni mwa wachezaji walio katika kiwango cha juu kiuchezaji, hivyo kuwa muhimu katika timu ya Simba na Stars.