Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mudhihir akatwa mkono
Mudhihir akatwa mkono
By Habari Tanzania | Published  09/15/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Tamali Vullu na Joseph Zablon


MBUNGE wa Jimbo la Mchinga (CCM), Mudhihir Mudhihir, amehamishiwa katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), JIJINI Dar es Salaam, akiwa amekatwa mkono wa kulia kutokana na ajali aliyoipata mkoani Lindi, juzi.

Mudhihir, mmoja wa wabunge wacheshi, alihamishiwa katika taasisi hiyo iliyo ndani ya eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili, majira ya saa 8:00 mchana, jana, baada ya kusafirishwa kwa ndege maalum ya kukodi kutoka Lindi alikokuwa amelazwa tangu juzi jioni.

Taarifa zinaeleza kuwa, ndege hiyo inayomilikiwa na kampuni binafsi ya Coastal Travel, ilikodishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano kutokana na ushauri wa madaktari.

Alipofikishwa hospitalini hapo, Mudhihir ambaye mbali ya kukatwa mkono wake wa kulia eneo la chini kidogo ya bega, ana jeraha aliloshonwa katika paji lake la uso, alipelekwa moja kwa moja katika chumba maalum kilichopo kwenye wodi nambari J.

Wauguzi waliozungumza na waandishi wa habari wa gazeti hili, walisema hali ya kiafya ya mwanasiasa huyo, aliyepata kuwa Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu, imekuwa ikiimarika tangu awasili hapo jana.

Muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo, viongozi mbalimbali walianza kuwasili kumjulia hali, wakiwamo, Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Afya, Prof. David Mwakyusa, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, wabunge na watu wengine mbalimbali.

Mbunge wa Kyela, Harrison Mwakyembe, alishindwa kujizua hospitalini hapo na kujikuta akibubujikwa na machozi muda mfupi tu baada ya kutoka kumuona mwanasiasa mwenzake.

“Ama kweli hujafa hujaumbika..., inasikitisha sana,” alisema Mwakyembe kwa sauti ya uchungu huku akifuta machozi kwa kitambaa.

Akizungumza kwa kujitahidi na Tanzania Daima, huku akiwa amezungukwa na ndugu na jamaa mbalimbali waliokwenda kumjulia hali, Mudhihir alisema alikuwa akisikia maumivu katika mkono wake wa kulia ambao ndiyo uliokatwa.

“Sijambo, namshukuru Mungu, ila ninahisi maumivu katika mkono huu uliokatwa,” alisema Mudhihir kwa hisia na kisha akafumba macho kisha akageuza kichwa mwelekeo mwingine wa kitanda.

Ofisa Uhusiano wa MOI, Almas Jumaa, alilieleza Tanzania Daima kwamba, hali ya Mudhihir imekuwa ikionekana kuimarika zaidi kadiri muda ulivyokuwa ukisonga mbele.

Jumaa, aliwataka wananchi kutokuwa na hofu yoyote, kwani mbunge huyo wa CCM alikuwa chini ya uangalizi wa ziada wa madaktari wa kitengo hicho.

Watu waliokuwapo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere, wakati ndege iliyomleta mbunge huyo ilipofika, walisema aliletwa akiwa katika kitanda maalum na akaingizwa kwa machela kwenye gari la wagonjwa lilikuwapo tayari eneo la uwanja wa ndege.

Kutoka Lindi, Mudhihir alikuwa amesindikizwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Said Sadiki na Mbunge wa Mtwara, Mohamed Said na wakapokewa uwanjani hapo na baadhi ya viongozi wakiwamo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Mbatia na Mbunge wa Nachingwea ambaye pia ni Naibu Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Mathias Chikawe.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, juzi alilieleza gazeti hili kuwa, Mudhihir, alipata ajali hiyo ya gari lake kupinduka, juzi saa 12.30 jioni, eneo la Lindi Mjini wakati akiwa peke yake ndani ya gari alilokuwa akiliendesha.

Taarifa nyingine zilizopatikana jana zinaeleza kuwa, gari hilo lilipinduka wakati Mudhihir alipofunga breki ghafla, alipokuwa akimkwepa mwendesha baiskeli aliyekatiza ghafla mbele ya gari lake.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.