Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »   Polisi yazuia Waislamu
Polisi yazuia Waislamu
By Habari Tanzania | Published  09/6/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Ratifa Baranyikwa na Prisca Nsemwa


POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam, imeyapiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanywa na waumini wa dini ya Kiislamu kesho, kushinikiza kurejeshwa kwa kiwanja wanachodai kimeuzwa kinyume cha taratibu kwa kampuni moja jijini Dar es Salaam.

Maandamano hayo yamepigwa marufuku wakati Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) likitoa taarifa kusisitiza kuwa, kiwanja hicho kimeuzwa kihalali kwa kampuni moja ya jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Alfred Tibaigana, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, maandamano hayo yamepigwa marufuku baada ya polisi kubaini kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kutokea uvunjifu wa amani na kumwagika kwa damu iwapo yangeruhusiwa.

“Hali hiyo inatokana na mvutano uliokuwepo baina ya pande mbili zinazopingana kuhusu suala hilo,” Tibaigana alisema na kubainisha kuwa aliishuhudia hali hiyo alipojadiliana na wawakilishi wa pande hizo ofisini kwake.

Tibaigana alisema kuwa wakati bado anatafakari baada ya kupokea barua toka kwa Sheikh Khalifa Khamis ya kuomba kuandamana siku ya Ijumaa, alipokea barua nyingine toka kwa Kamati ya Maimamu ya kuokoa mali ya waislamu, iliyosainiwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ustadh Said Mwaipopo na Mkurugenzi wa Habari, Chief Hussen Msopa, wakimuomba asitishe maandamano hayo, huku wakitoa sababu saba.

Alisema kuwa barua hiyo inatokana na kikao cha maimamu wapatao 15 wa misikiti ya Tegeta, Buguruni, Tandika, Magomeni, Mwananyamala, Vingunguti, Keko, Kurasini, Tabata, Ubungo, Kimara, Mbezi Beach, Mabibo na Mwenge.

Tibaigana alisema kuwa kati ya sababu walizozitoa, ilikuwepo iliyoeleza kuwa zimepangwa njama na kundi moja, kuingia katika maandamano hayo kwa nia ya kuwadhuru baadhi ya watu, na kudai kuwa kuna vijana wengine walikuwa wamepangwa na Sheikh Khalifa ili kwenda kuvamia na kuiba mabati katika kiwanja hicho kilichopo Chang’ombe.

Aidha, Tibaigana alisema kuwa alitahadharishwa kuwa kuna kundi kubwa la vijana ambao walipanga kuswali katika misikiti ya Manyema, Idrisa, Lindi na Chipata na baada ya swala watajipanga kuzuia maandamano hayo.

Tibaigana alisema kuwa, uamuzi wa kusitisha maandamo hayo unakuja baada ya kufanya majadiliano ofisini kwake na makundi yote mawili.

“Nilijadiliana nao kwa saa tatu, nilitumia busara nyingi ku-control (kudhibiti) kikao hicho, wote walikuwa na chuki kubwa,” alisema Tibaigana.

Hata hivyo, alisema kuwa vitisho vilivyo katika barua ya kundi la Mwaipopo na Msopa, viliendelea kujionyesha waziwazi katika kikao hicho, hadi akafikia hatua ya kuagiza kufunguliwa kwa jalada la uchunguzi.

Alisema kuwa, uchunguzi huo ulioanza jana, utamuwezesha kujua kama kweli vitisho vya kudhuriana na kumwaga damu ni vya kweli, ili kama ni vya kweli, wanaohusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wakati huo huo, Sheikh Khalifa Khamis alisema kuwa Waislamu wameridhia kauli iliyotolewa na Jeshi la Polisi la kusitisha maandamano hayo, hadi uchunguzi utakapokamilika.

Sheikh Khalifa alieleza kuwa, Kamanda Tibaigana aliwaahidi kuwa uchunguzi utakamilika katika kipindi cha siku 14 na mara utakapokamilika, maandamano yataendelea kama kawaida.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Msikiti wa Mtoro uliopo Kariakoo, alieleza kuwa Waislamu watambue kuwa maandamano hayo yataendelea mara baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika.

Aidha aliwataka Waislamu kuacha njaa ya fedha katika vitu vya Mungu, hususani kiwanja hicho, ambacho alidai ni wakfu wa Waislamu kwa sababu njia zilizotumika kumilikishwa kiwanja hicho ni za kitapeli.

Alionyesha kudharau vitisho vilivyotolewa na maimamu, kwamba watavuruga maandamano hayo na kusema kuwa harakati za Waislamu hazitakatishwa na vitisho vya mtu yeyote.

Sakata hilo linatokana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kudaiwa kuuza kiwanja hicho, kinachoelezwa kuwa ni wakfu wa Waislamu, kwa Kampuni ya Quality Group Ltd, inayomilikiwa na Yusuf Manji.

Kwa maana hiyo, Sheikh Khalifa anaongoza harakati za kutaka kiwanja hicho kirejeshwa na pia kumtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli, ajiuzulu kwa kushindwa kukirejesha kiwanja hicho kwa Waislamu.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa uamuzi wa kumilikisha kiwanja kwa Quality Group Limited uliofanywa na vyombo vya juu kabisa vya BAKWATA, ni wa mwisho na hauwezi kubatilishwa.

Habari kutoka ndani ya BAKWATA zilisema kwamba, kikao cha Halmashauri Kuu, Maulamaa na Baraza la Wadhamini kilichofanyika Julai mwaka huu, kiliafiki na kuridhia kiwanja hicho chenye namba 311/1 kilichopo Chang’ombe, wilayani Temeke, Dar es Salaam kuwa ni mali halali ya Quality Group kwa mujibu wa sheria.

Mkutano wa Halmashauri Kuu ulifanyika chini ya mwenyekiti wake, Sheikh Hamisi Mataka na Baraza la Maulamaa lilikutana chini ya uenyekiti wa Sheikh Mkuu, Mufti Issa bin Shaaban Simba.

Taarifa ya BAKWATA ilisema kwamba, si sahihi kwa Waislamu kuchochewa kuacha kushughulikia mambo ya msingi badala ya kuingia katika mitego ya ‘wachache wenye njaa’ wanaotaka kuwatumia.

Viongozi hao wa BAKWATA wamesema kwamba, haistahili hata kidogo Waislamu kuburuzwa na kikundi kinachodai kwamba kinatetea maslahi na haki za Waislamu.

BAKWATA imesema kwamba, Quality Group Limited iliuziwa kiwanja hicho na ikafanya malipo yote kwa mujibu wa mikataba na haiwezekani kuanza tena kurudi nyuma na kuanza kutaka kubatilisha mkataba huo.

“Mtu akishapewa hati ya kumiliki ardhi, hakuna mamlaka yoyote inayoweza kufuta au kubatilisha hati hiyo, isipokuwa rais tu, ambaye naye hufanya hivyo kwa manufaa ya umma au sababu nyinginezo baada ya kuridhika kwamba kuna umuhimu huo,” ilisema taarifa hiyo.

Hata hivyo, BAKWATA ilisema kwamba katika suala hili la kiwanja kilichouzwa kwa Quality Group Limited, hakuna kurudi nyuma, kwani kufanya hivyo itakuwa ni dhuluma tupu.

“BAKWATA haina madai wala lawama zozote kwa Quality Group Limited wala mmiliki wake kijana Yusuf Manji, kwani kila kitu kilifanyika kwa mujibu wa makubaliano na sheria ilifuatwa kikamilifu,” alisema kiongozi mmoja wa BAKWATA ambaye alikuwa miongoni mwa waliofikia uamuzi wa Julai 21, mwaka huu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Abdulmalik)
    Rating
    Maandamano yanini?wakati Kiwanja kimeuzwa na walio jiita Mashekh wetu .
     
  • Comment #2 (Posted by JUMANNE KISHOKAH)
    Rating
    LAKINI BAKWATA HAWASEMI KWA NINI WALIKIUZA KIWANJA MALI YA WAISLAAMU BADALA YA KUKITUMIA KWA MIRADI AU SHUGHULI ZA KIISLAMU. NAO POLISI KAMA WAMEPEWA DOKEZO HIZO SI "WAYASINDIKIZE MAANDAMANO" WAKIWATUPIA MACHO HAO WATAKAOLETA FUJO BADALA YA KUYAPIGA MARUFUKU? KITENDO HICHO NDIO KITAJAZA CHUKI NA HASIRA ZAIDI KATIKA KIKUNDI CHA SHK. KHALIFA HAMIS KULIKONI WAKISHANDAMANA SHAUKU YAO ITAKWISHA.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.