Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  TRC yakodishwa
TRC yakodishwa
By Marshy Abdu | Published  09/4/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
TRC yakodishwa

na Ratifa Baranyikwa


MKATABA wa ukodishwaji wa Shirika la Reli nchini (TRC) hatimaye umesainiwa huku ukiendelea kuacha utata mkubwa katika masuala kadhaa likiwamo la hatima ya wafanyakazi watakaopunguzwa.

Kikubwa kinachozusha utata huo ni kukinzana kwa kauli zinazohusu wafanyakazi hao zilizotolewa jana hiyo hiyo na Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge na ile ya Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC), Ali Karavina.

Wakati Chenge akisema kuwa wafanyakazi wote wanaopunguzwa wameshalipwa mafao yao stahili, PSRC, katika taarifa yake iliyoitoa baada ya kusainiwa kwa mkataba huo inaeleza kuwa, wafanyakazi zaidi wa 3,000, watakaoachishwa kazi watalipwa mafao yao.

Mbali ya hilo, jambo jingine linaloibua maswali ni lile linalohusu siku ambayo waendeshaji wapya, Kampuni ya Rites kutoka India watakabidhiwa uendeshaji wa shirika hilo hasa baada ya jana kusaini na kutokabidhiwa.

Taarifa za awali kutoka serikalini zilikuwa zikieleza kuwa, Rites walikuwa wakitakiwa wawe wamekabidhiwa uendeshaji wa shirika hilo tangu Septemba mosi mwaka huu.

Katika hotuba yake ya jana, Waziri Chenge aliliongezea utata suala hilo baada ya sehemu ya hotuba yake kuonyesha maneno yakibainisha kuwa jana ilikuwa ndiyo siku ya shirika hilo kukabidhiwa kwa waendeshaji wapya, Rites.

Hata hivyo, maneno hayo katika hotuba ya Chenge yalifutwa kwa kupigiwa mstari katikati na kalamu na kuongezwa maneno ya ziada, yaliyoandikwa kwa mkono kuwa, RITES itakabidhiwa uendeshaji wa TRC Oktoba mosi.

Mkataba huo ulisainiwa jana jijini Dar es Salaam katika ofisi za PSRC, kati ya Mkurugenzi wa Kampuni mpya ya TRL, Sundhir Kumar Seth na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya RAHCO, Agnes Bukuku.

RAHCO imeanzishwa katika mabadiliko ya TRC, kama kampuni itakayosimamia uendeshaji wa kampuni mpya ya TRL na kuhakikisha kuwa miundombinu ya reli nchini inaendelezwa.

Chini ya mkataba huo, wafanyakazi 3,316 wa TRC wamehamishiwa pamoja na mafao yao kwenye Kampuni mpya ya TRL na kuwa mafao yao sasa yataboreshwa.

Aidha, mkataba unaonyesha kuwa wafanyakazi 3,204 aidha wamepunguzwa au watapunguzwa, baada ya Serikali kupitia RAHCO, kutiliana saini mkataba wa ukodishaji.

Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti Mtendaji wa PSRC, Ally Karavina, ilisema kuwa, wafanyakazi waliopunguzwa tayari wameshalipwa haki na stahili zao pamoja na mkono wa heri kutoka serikalini.

Kwa mujibu wa taarifa ya PSRC, chini ya mkataba huo wa ukodishwaji wa TRC kwa miaka 25, RAHCO pia itakuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa mkataba huo na kuhakikisha mkataba unafuatwa kwa mujibu wa makubaliano.

RAHCO pia itafanya kazi ya kufuatilia na kutathmini utendaji wa TRL, na kusimamia utekelezaji wa mipango ya baadaye ya upanuzi wa miundombinu ya reli.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TRL kwa upande wake itakuwa ndiyo mwendeshaji wa biashara za reli ikisimamiwa na RAHCO, wakati Mamlaka ya kusimamia vyombo vya usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA), itakuwa mdhibiti wa shughuli za usafiri wa reli hiyo.

“TRL ni Kampuni iliyosajiliwa nchini na inamilikiwa kwa pamoja na Kampuni iliyoshinda kuendesha shughuli za TRC, Kampuni ya RITES ya India inayomiliki asilimia 51 ya hisa zote za kampuni hiyo na Serikali ya Tanzania inayomiliki asilimia 49,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, wakati wote wa mchakato wa kumpata mwendeshaji huyo, TRL imeweza kukamilisha mipango ya kupata fedha za kugharamia hatua ya awali ya uwekezaji katika kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na kupata mkopo wa dola za Marekani milioni 44 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa muhimu, zikiwemo injini za treni, mabehewa ya abiria na mizigo.

Katika hotuba yake iliyotolewa jana, Waziri Chenge alisema kuwa kampuni mpya ya TRL inatarajia kuimarisha huduma ya usafiri wa reli na kwamba kipaumbele cha kampuni hiyo mpya katika wiki chache zijazo kitakuwa ni kuangalia uwezekano wa kuanzisha safari za treni za abiria kuanzia Dar es Salaam badala ya Dodoma kama ilivyo hivi sasa.

“Serikali inaamini kuwa kampuni mpya itaboresha huduma ya usafiri wa reli nchini na kwa nchi jirani, hasa baada ya kukamilika kwa mpango wa awali wa uwekezaji,” alisema Chenge.

Chenge alisema kuwa mchakato wa kuibinafsisha TRC umepitia mlolongo mrefu pamoja na vikwazo mbalimbali.

Kampuni ya RITES ilishinda zabuni ya kuendesha shughuli za reli mwezi Machi mwaka 2006.

Wakati huo huo Rais Jakaya Kikwete amemteua George Hadji Ally, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya RAHCO kwa kipindi cha miaka mitatu. Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Miundombinu, ilieleza kuwa uteuzi huo ulianza Agosti 31 mwaka huu.

Aidha, Waziri Chenge amewateua wajumbe sita watakaounda bodi ya RAHCO, kuanzia Agosti 31 mwaka huu.

Aliwataja wajumbe hao kuwa ni Agness Bukuku, Balozi Ernest Mulokozi, Mohamed Missanga, Said Bakhresa, Bernard Liamba na Linford Mboma.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.