Shirika la kidini nchini linalohudumia wakimbizi TCRS limeanzisha ofisi zake nchini Burundi ili kuwasaidia warundi na wakimbizi watakaorejea nchini mwao kutoka nchini Tanzania.
Mratibu mradi wa shirika la TCRS Bw. Jesse Kamstra ametoa taarifa hiyo wakati akihojiwa na wandishi wa habari juu ya nini watakachofanya kuwasaidia wakimbizi kukuza uchumi binafsi baada ya kurejea nchini mwao.
Bw. Kamstra amebainisha kuwa tayari watumishi kadhaa wameajiliwa nchini Burundi ili kufanikisha azima ya kuhamishia baadhi ya miradi ya misaada nchini humo kutoka katika makambi ya wakimbizi.
Amesema miradi inayotegemewa kuanza hivi karibuni ni pamoja na mradi wa kupambana na virusi vya ukimwi STOP SIDA, miradi ya kilimo na ufugaji pamoja na utoaji wa misaada ya kielimu kwa warundi.
Akitaja sababu za kufungua ofisi hizo nchini Burundi Bw. Kamstra amebainisha kuwa TCRS chini ya ufadhili wa Lutheran World Federation LWF wanafanya kazi maeneo mbalimbali duniani kusaidia wakimbizi na wanaohitaji misaada ya kiutu.
Ametaja baadhi ya wakimbizi waliopata ajira katika ofisi za Burundi kwamba ni waliokuwa wakimbizi nchini Tanzania ambapo amemtaja Bw. Barnabas Bugera na Noa Sebisaba mwasisi wa shirika la STOP SIDA katika kambi ya wakimbizi ya Kanembwa wilayani Kibondo.
Hatua hiyo imefikiwa siku chache kabla shirika la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR kutangaza rasimi mpango wa kuhamasisha wakimbizi walioko magharibi mwa Tanzania kurejea nchini mwao kwa hiari.
Shirika la UNHCR june 20 kama sehemu ya kuadhimisha siku ya wakimbizi duniani lilizindua rasimi hamasa kwa wakimbizi kurejea makwao kwa hiari na limeahidi kufuatilia kwa undani hali ya Amani nchini Burundi.
Wakati huohuo shirika la TCRS limewataka wakimbizi kutumia mila na desturi za nchi zao za asili kujilinda na kukomesha uhalifu katika makambi ya wakimbizi badala ya kutegemea polisi.
Bw. Jesse Kamstra ambaye ni mratibu wa TCRS kitengo cha wakimbizi amesema, kumekuwa na Matukio ya uhalifu ambayo hupelekea wakimbizi kulaumu jeshi la polisi na kusahau kuwa nao wanawajibu wa kujilinda pia.
Amesisitiza kuwa kuwepo kwa jeshi la ulinzi wa jadi yaani sungusungu wanapaswa kuwa chini ya viongozi wa kijamii badala ya kuwa chini ya UNHCR ambapo jamii hudhani kuwa si jukumu lao.
Amewahimiza wakimbizi kufanya uchaguzi wa vijana wanaostahili kuwa walinzi wa jadi ambao watakuwa wakifanya kazi za ulinzi kwa kuamliwa na jamii yao kuliko kutegemea kila kitu kufanywa na UNHCR.
Takribani wakimbizi elfu hamsini wa Burundi wako wilayani Kibondo ambapo wanahifadhiwa katika makambi ya Kanembwa, Nduta na Mtendeli pamoja na wakimbizi kutoka jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo DRC na Rwanda walioko katika kambi ya Mkugwa.