ZIARA ya viongozi wa vyama vinne vya upinzani mikoani kuelezea sakata la kusimamishwa kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe ZuberiZitto (CHADEMA), inaibua kashfa nyingine ambazo zilishaanza kusahaulika.
Katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Kalebezo katika Jimbo la Buchosa, Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, aliahidi kuyataja majina ya viongozi ambao walihusika na dhahabu aliyoikamata katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, ikisafirishwa nje kinyemela.
Mrema alikamata dhahabu hiyo wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, wakati wa utawala wa Awamu ya Pili, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi.
Aidha, katika mkutano huo uliohudhuriwa na umati wa watu, Mrema aliahidi pia kutoa siri kwa kusema aliambiwa nini na Rais Mwinyi baada ya kukamata dhahabu hiyo mwaka 1992.
Mrema aliuambia umati huo kuwa siri hizo zote atazimwaga siku ya hitimisho la ziara hiyo, Septemba 15, katika mkutano mkubwa wa hadhara utakaofanyika katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam.
Sakata hilo la kukamata dhahabu, ni moja ya masuala ambayo yalimjengea sifa Mrema, na kumfanya aonekane kuwa kiongozi mchapakazi miongoni mwa wengine ambao, aidha walitishwa na rushwa au nafsi za viongozi walio juu yao.
Aidha, wazo la ushirikiano baina ya vyama vya upinzani, lilionekana kuungwa mkono sana na wananchi waliohudhuria mkutano huo kwani walikuwa wakishangilia kwa nguvu kila lilipotajwa.
Kwa upande wake, Zitto aliwataka vijana kuamka na kuanza kuitetea nchi yao kwani wasipofanya hivyo, lipo kundi la watu ambao wameelekeza jitihada zao katika kuiba rasilimali za nchi.
Aidha, katika mlolongo wake wa uchambuzi wa majibu ya Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kwa hoja yake binafsi kuhusiana na kusiniwa kwa mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi, alishangazwa na maelezo kuwa mchakato wa kupitia mikataba ya madini nchini ulishakamilishwa.
Akihutubia katika mkutano huo, Zitto alihoji hilo limewezekana vipi wakati zipo kampuni za madini ambazo hazijafikia maafikiano na serikali kuhusiana na mikataba hiyo.
Aliitaja kampuni moja kubwa inayojishughulisha na uchimbaji wa dhahabu Kanda ya Ziwa na kusema kuwa bado haijaanza kulipa kodi serikalini licha ya waziri kuliambia Bunge kuwa kazi hiyo imekamilika.
Aidha, alisema kuwa inashangaza kuwa wakati kampuni hiyo hailipi kodi hapa nchini kutokana na shughuli za uchimbaji wa dhahabu, ina migodi katika nchini nyingine ambako serikali ya nchi hiyo inamiliki hisa katika kampuni hiyo.
“Inashangaza sana kwamba wakati huko wanagawana mapato na serikali kulingana na hisa zao, hapa kwetu tunaambulia patupu na viongozi wetu wakizunguka kuueleza umma kuwa tunanufaika na madini. Hivi tunanufaika wananchi au wao?” alihoji Zitto.
Hoja hiyo ya Zitto ni miongoni mwa kile anachokiita kuwashitaki wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wakati wapinzani wakijitahidi kutetea masuala yenye masilahi kwa wananchi, wao wanawabeza na kuwazomea.
Alianza kazi hiyo mwishoni mwa wiki na wakati akihutubua mkutano jijini Mwanza juzi alisema hali hiyo haiwezi kuondoka iwapo vijana wataendelea kubakia kimya, akawataka kuungana bila kujali itikadi zao za kisiasa na kuunda vugu vugu la kudai, kutetea na kulinda rasilimali za taifa na kukataa kuwa mawakala wa kuuza mali za nchi hii kwa kuwa wao ndio kizazi kinachotegemewa kuleta ukombozi wa kweli wa kiuchumi wa nchi.
Alisema wakati sasa umefika kwa vijana na wananchi wote kutanguliza mbele masilahi ya taifa kwa kuhakikisha kuwa hakuna rasilimali ya nchi hii inayouzwa au kupokwa mbele ya macho yao.
“Vijana tuanzishe vugu vugu la kudai rasilimali za taifa, bila kujali itikadi wala mtu atokako. Ni aibu kwa mbunge wa Kigoma kuanza kudai dhahabu za Kanda ya Ziwa wakati wananchi na vijana wa Kanda ya Ziwa wametulia tu na hawasemi kitu, wakati umefika sasa tuungane kudai rasilimali zetu,” alisema Kabwe huku akishangiliwa na maelfu ya wakazi wa Mwanza.
Alisema kati ya migodi sita inayofanya kazi iliyoko nchini na ukiondoa wa Buhemba uliofilisika, migodi mitano yote iko Kanda ya Ziwa kasoro mmoja tu, wa Resolute Nzenga, ulioko Kanda ya Mgaharibi, lakini mtu wa Mwanza akitaka kwenda Dar es Salaam bila tabu analazimika kupita Kenya na kuwataka wananchi wa kanda hii kujenga utamaduni wa kuhoji kwa nini uchumi haufanani na rasilimali walizo nazo.
Katika hatua nyingine, Zitto aliwataka wananchi kuamua kuanzia sasa iwe mwiko kuwa na wabunge zaidi ya nusu bungeni wa kutoka chama kimoja chochote cha siasa kwani vinginevyo nchi itakwisha, kwa kuwa matumizi ya wingi wa wabunge yameonyesha kuwa ni janga kwa taifa.
“Mmeona wenyewe jinsi wabunge wa CCM wanavyokuwa wakituzomea hata tukitoa hoja za msingi, wamekuwa na matumizi mabaya ya wingi wao, kuanzia sasa iwe ni mwiko kwa chama kuwa na wabunge zaidi ya nusu bungeni, muanze kujenga uzalendo, muache kulalamika na vijana muanze sasa kuwa walinzi wa rasilimali zenu,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo wa juzi, Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe (CHADEMA) aliwataka vijana kuiga mfano wa vijana wenzao wa enzi za Mwalimu Nyerere, ambao waliuchukia ukoloni na kuanzisha mapambano ya kuukataa na wao wanzishe mapambano ya kuletea ukombozi wa uchumi.
“Mwalimu na wenzake wakiwa vijana walisema tukatae ukoloni, na kweli wakakataa na kutuletea uhuru, sisi vijana wa leo tupiganie ukombozi wa uchumi, mkikataa mtakuwa mmeisaliti nchi hii, na mkizubaa rasilimali za nchi zitachukuliwa huku mnaona,” alisema.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Wilfred Rwakatare, alisema linapokuja sula la kudai haki, hakuna mipaka wala itikadi kwani haki inadaiwa na yeyote anayedhani anadhulumiwa.
“Kudai haki hakuhitaji elimu kubwa ya kutisha, kama wewe huridhiki na aina ya maisha unayoishi, jiunge na vugu vugu la kudai haki, kama wewe ni polisi ili uishi unahitaji kumtoa mtu kitu kidogo, jiunge na jeshi la kudai haki, kama wewe ni mwalimu unahisi mshahara wako haukutoshi hata kwa wiki moja, jiunge la vugu vugu la kudai haki. Ndugu zangu haki haijui itikadi wala kabila ni mapambano ya watu wote,” alisisitiza Rwakatare.
Alitoa mfano wa msemo mmoja wa Kihaya wenye tafsiri ya Kiswahili kwamba mbwa akitaka kufa huziba pua, na kusema kwamba CCM wameziba pua hawasikii wa kuona alama za nyakati, na kuongeza kwamba uamuzi waliofanya wa kumsimamsisha Zitto ni dalili za mbwa anayetaka kufa.
Katika mkutano huo Mrema, huku akishangiliwa kwa nguvu na wananchi waliokusanyika hapo, aliwataka Watanzania kutowaruhusu CCM kuzima changamoto iliyoanzishwa na Zito na Dk. Willibrod Slaa, kwa kuwa ni kawaida ya CCM kuhujumu ajenda za maana na kuzifanya kama za mzaha huku taifa linaangamia.
Alisema sasa wameachana na ujinga wa zamani na kwamba vyama hivyo vinne vya CHADEMA, CUF, NCCR – Mageuzi na TLP wameamua kwa dhati kabisa kuungana katika uchaguzi wa mkuu wa mwaka 2010.
“Nyinyi Mwanza ndio mnatuangusha, yuko wapi mbunge wenu wa upinzani, hamna hata diwani mmoja, sasa mwaka 2010, tumeamua kuacha ule ujinga wa zamani, tutaweka mgombea urais mmoja, mbunge mmoja kila jimbo na diwani mmoja kila kata,” alisema na kushangiliwa kwa nguvu.
Akihitimisha mkutano huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, huku akimnukuu mwanafalsafa wa Kimarekani David (1718 - 1760), alisema katika mapambano ya kudai haki, ni lazima watu wakubali kuumia, ni lazima watu wachache waumie kwa ajili ya wengi, na kusema yeye amejitoa kwa ajili hiyo.
Viongozi hao wamepanga kuzunguka katika mikoa 12 kabla ya kuhitimisha ziara hiyo lakini kumekuwa na maombi kutoka mikoa mingi ambayo haitazungukiwa na viongozi hao, wakitaka wafike huko pia.
Aidha, katika mkutano uliofanyika mjini Geita, Mrema aliahidi kumkabidhi Zitto nyaraka kuhusiana na kashfa za ubadhirifu uliofanywa na viongozi wa serikali na CCM wakati yeye (Mrema) alipokuwa serikalini.
Mrema alisema atakabidhi nyaraka hizo katika mkutano wa hadhara utakaofanyika Dar es salaam kuhitimisha ziara hiyo.
“Yapo mambo mengi sana ambayo hamyajui wananchi, ambayo yalikuwa yanafanywa na viongonzi wa CCM, mpaka sasa naamini yanaendelea kufanyika na ndiyo maana Zitto ameyakuta na sasa anayaweka hadharani, sasa ni wakati wangu na mie kumkabidhi Zitto nyaraka zote na yeye aweze kuzifanyia kazi,” alisema Mrema.
Alisema alishindwa kufanya hivyo mapema kwa sababu hakuona mtu jasiri kama alivyokuwa yeye ambaye angeweza kuzishughulikia nyaraka hizo ipasavyo.
Alisema nyaraka hizo zina ushahidi wa kuwatia hatiani viongozi ambao ni wezi wa mali ya umma.