Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Waliofukuzwa Mtibwa wamwandikia Kikwete
http://www.habaritanzania.com/articles/4155/1/Waliofukuzwa-Mtibwa-wamwandikia-Kikwete
By Habari Tanzania
Published on 09/2/2007
 
WALIOKUWA wafanyakazi wa kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, wamemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete, wakimlalamikia mwajiri wao kwa kutowalipa mafao kwa muda wa miaka minane sasa.

na Tamali Vullu


WALIOKUWA wafanyakazi wa kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, wamemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete, wakimlalamikia mwajiri wao kwa kutowalipa mafao kwa muda wa miaka minane sasa.

Katika barua hiyo, wafanyakazi hao wanadai kuwa, tangu waachishwe kazi katika kiwanda hicho, mwajiri wao ameshindwa kuwalipa mafao, hali ambayo imewasababisha kuishi maisha magumu.

Wakizungumza katika ofisi za Tanzania Daima jana, walisema walipokwenda kufuatilia mafao yao katika ofisi za Mfuko wa Pensheni wa PPF, walielezwa kuwa, mwajiri wao alikuwa hajawasilisha michango tangu mwaka 1999, alipochukua kiwanda hicho.

Walielezwa kuwa hawataweza kulipwa mafao yao na PPF, mpaka mwajiri wao apeleke fedha hizo ambazo ni zaidi ya sh milioni 800.

Wafanyakazi hao wakiongozwa na mwenzao, Jovith Bitamale, alisema tayari wameshawalisha malalamiko yao Ikulu na kupokewa na Katibu wa Katibu Kiongozi na Mwanasheria wake.

“Barua ya malalamiko yetu tumeiwasilisha leo (jana) kwa Rais… kwani ni muda mrefu mwajiri ameshindwa kutulipa haki zetu,” alisema Bitamale.

Wafanyakazi hao wanadai sababu ya kufukuzwa kazi ni kueleza kero zao kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro dhidi ya mmiliki wa kiwanda.

Aidha, wafanyakazi hao wameulalamikia uongozi wa tawi la wafanyakazi kiwandani hapo (TPAWU) kwa kushindwa kuwasaidia ili waweze kupatiwa haki yao.

Sambamba na hayo, wafanyakazi hao wameelezea mapungufu ya taarifa ya uchunguzi wa mgogoro kati TPAWU na uongozi wa kiwanda hicho.

Wafanyakazi hao walidai kuwa katika taarifa hiyo, wamebaini mapungufu makubwa ya kiufundi na pia imeonyesha upendeleo wa majibu kwa uongozi wa TPAWU, Meneja Mkuu na viongozi wa kanda kwa nia ya kuwalinda, huku wakiuacha ukweli ambao ndio kiini cha mgogoro.