VITA ya makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hali ambayo imekuwa ikikitawala chama hicho kila nyakati za uchaguzi, sasa imeanza kuchukua sura mpya.
Ushahidi wa kushika kasi kwa vita hiyo ya makundi ni matukio ya wana CCM, viongozi na makada wa kawaida wa ngazi mbalimbali kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na yale ya kuvurugika kwa uchaguzi katika maeneo kadhaa nchini.
Habari ambazo Tanzania Daima imezikusanya kutoka maeneo mbalimbali nchini zinaeleza kuwa, kukithiri kwa taarifa za wagombea na wapambe wao kunaswa na maofisa wa Takukuru, kumekuwa kukisababishwa na makada wa chama hicho kuwatonya kwa siri watumishi hao wa Takukuru.
Aidha, kukamatwa kwa watu wasio wagombea, wakiwamo wabunge na viongozi wengine wa chama hicho kumeelezwa kuwa kunatokana na jitihada za makundi mbalimbali yenye malengo ya juu kiuchaguzi, kimkoa na kitaifa kutaka kuhakikisha kuwa watu wa makundi yao ndio wanaoshinda katika chaguzi zote za wilaya.
Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana washindi wanaopatikana au makada wanaokamatwa na Takukuru wamekuwa wakihusishwa na ama makundi yenye ajenda moja au yale yanayopingana, si tu kwa ngazi ya mkoa, bali hata kitaifa.
Kutoka Kyela kwa mfano, wana CCM wilayani humo wamekuwa wakieleza kuwa, kundi lililoshinda uchaguzi huo ni lile linaloungwa mkono na watu waliokuwa kinyume cha harakati za kundi la mtandao lililokuwa likimuunga mkono Rais Jakaya Kikwete wakati wa mchakato wa ndani ya chama hicho mwaka 2005.
Kama hiyo haitoshi, hata tukio la wabunge wawili wa CCM waliokamatwa huko Arusha wakiwamo na makada wengine wa chama hicho, mbali ya kuonekana kuwa la kihalifu, limehusishwa pia na siasa hizo hizo za makundi ya mwaka 2005 na yenye malengo ya kimkoa na kitaifa kwa siku zijazo.
Kauli ya Mbunge wa Arumeru Magharibi, Elisa Mollel (CCM) ambaye juzi alikamatwa na Takukuru akihusishwa na vitendo vya rushwa inaonyesha namna makundi ndani ya chama hicho yanavyofanya kazi.
Mollel katika kauli yake, alikaririwa na gazeti moja la kila siku (si Tanzania Daima) akihusisha kukamatwa kwake na kile alichokitaja kuwa ni ‘mkono wa mtu’, wenye malengo ya kisiasa.
Mbali ya hilo, mbunge huyo alieleza kushangazwa kwake na tukio la yeye na Mbunge mwenzake wa Longido, Michael Lekule Laizer, kukamatwa wakiwa hawatoi au kupokea rushwa.
Wabunge hao wawili ambao wote na wenzao wengine tisa, waliachiwa kwa dhamana jana, huku wakisubiri hatima yao ndani ya chama chao ambacho leo kimeitisha kikao cha Kamati ya Maadili kuwajadili, kwa nyakati tofauti walikana tuhuma za rushwa.
Wakati vita ya makundi ikisubiri hatima ya maamuzi ya Takukuru na vikao vya ndani ya CCM, huko Tanga vita ya makundi iliendelea kukitafuna chama hicho.
Vita hiyo ya makundi ndiyo ambayo inadaiwa kuwa msingi wa shutuma za Mwenyekiti wa Wilaya ya Tanga aliyeshinda wadhifa huo mwishoni mwa wiki iliyopita, Mohamed Dhikri, kumtupia makombora ya lawama Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, akimtuhumu kutumia lugha isiyostahili kwa viongozi wenzake.
Aidha, kiongozi huyo wa CCM Tanga aliihusisha ziara ya Makamba mkoani Tanga kuwa iliyokuwa na mwelekeo wa kulipigia kampeni kundi moja.
Mbali ya hilo, vita nyingine ya makundi ndani ya chama hicho, iliibuliwa na mmoja wa wagombea wa nafasi ya Katibu Mwenezi, Shekue Pashua, ambaye aliibua tuhuma nzito dhidi ya kiongozi mwenzake ambaye alimtuhumu kwa kuwakusanya makatibu kata katika Hoteli ya Splendid katika jiji hilo kwa lengo la kumwangusha yeye.
Pashua ambaye anatetea nafasi yake, aliandika malalamiko yake hayo kwa Katibu wa CCM wa Mkoa wa Tanga, hatua ambayo ilisababisha uchaguzi huo uliokuwa ufanyike juzi ukaahirishwa.
Kutoka Mbeya nako, vita hiyo ya makundi imeendelea kukitafuna chama hicho baada ya baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa CCM kubaini njama kabambe za kulibeba kundi la mgombea mmoja wa uenyekiti wa wilaya.
Taarifa kutoka ndani ya chama hicho mkoani humo zinaonyesha kuwa kubainika kwa njama hizo zilizohusisha vijikaratasi haramu vya kura, sanduku moja la ziada la kupigia kura na kupandikizwa kwa wajumbe mamluki 300, ndicho chanzo kikuu cha kuahirishwa kwa uchaguzi uliokuwa ufanyike juzi.
Aidha, kuahirishwa kwa uchaguzi huo kwa sababu ya makundi kulisababishwa na hatua ya makada kadhaa wa chama hicho kutoka katika Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kuendelea kupiga kampeni za kumtaka mgombea mmoja kati ya watatu wa uenyekiti wa wilaya.
Kung’amuliwa kwa njama hizo kulisababisha wagombea wawili wa nafasi hiyo ya uenyekiti, Dor Mohamed Issa na Francis Masole Shonyela, kupinga kuendelea kwa uchaguzi huo na kumwacha mgombea mwenzao, Edson Ross Mwaikambo, kuwa mtu aliyetaka zoezi hilo liendelee.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Mbeya, Elia Nyambo, alikanusha kufahamu lolote kuhusu kuwapo kwa hujuma hizo mbali ya kukiri kuwepo kwa mamluki wengi ndani ya ukumbi.
Hata hivyo Nyambo alikuwa akilalamikiwa na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wa wilaya kwa hatua yake ya kumruhusu Mkuu wa Wilaya ya Mbeya kusimamia zoezi hilo wakati akijua kuwa ni kiongozi wa kiserikali.