Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Zitto aijibu Barrick
Zitto aijibu Barrick
By Marshy Abdu | Published  08/29/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
Zitto aijibu Barrick
na Mwandishi Wetu


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini aliyesimamishwa, Zitto Zuberi Kabwe (Chadema), ameeleza kushangazwa na majibu ya Kampuni ya Barrick Tanzania, iliyoyatoa juzi kuhusu mazingira yaliyosababisha mkataba wa madini wa Buzwagi usainiwe London, Uingereza.

Taarifa ya maandishi ya mbunge huyo, aliyoisambaza katika vyombo vya habari jana, inaeleza kuwapo kwa mkanganyiko mkubwa katika majibu yaliyotolewa na Barrick, juzi, kuhusu suala hilo la Buzwagi, yanapolinganishwa na yale yaliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, bungeni kwa nyakati tofauti.

Akitoa mfano, Zitto ambaye taarifa yake imechapishwa kwa kirefu ndani ya gazeti hili, alisema madai ya Barrick kwamba wao ndio waliomfuata waziri London, Uingereza yanatofautiana na majibu aliyoyatoa Waziri Nazir Karamagi bungeni, Julai 16, mwaka huu.

“Majibu haya ya Barrick kwanza yanapishana sana na majibu mawili tofauti ya Waziri wa Nishati na Madini ndani ya Bunge… Julai 16, mwaka huu, Waziri aliliambia Bunge kuwa uzoefu wake katika medani ya biashara na sekta binafsi, ndio uliosababisha akasaini mkataba huo jijini London na kwamba Bodi ya Barrick ilikuwa inakutana huko.

“Waziri huyo huyo, Agosti 14, mwaka huu, aliliambia Bunge kuwa, mkataba ulitakiwa kusainiwa kabla ya Machi na kujenga msingi wa hoja yake ya uharakishwaji katika faida za mgodi wa Buzwagi.

“…Mashaka yangu na labda ukweli unaanza kudhihiri, unajengwa na tarehe zinazotajwa. Sababu ya uzoefu wa waziri katika biashara na sekta binafsi inayojali muda haitajwi tena katika majibu ya serikali. Sababu ambayo ilinukuliwa na kumbukumbu za Bunge. Barrick nao wamekuja na sababu zao,” anabainisha Zitto katika waraka wake huo.

Zitto ambaye alisimamishwa ubunge kwa sababu ya kuisakama Barrick, katika waraka wake huo, ameeleza pia kushangazwa na hoja hizo za kampuni hiyo na akazielezea kuwa zilizo na ukakasi kutokana na kutoa mambo mengine yanayozidi kuonyesha kuwapo kwa kile anachokielezea kuwa ni mazingira ya rushwa katika mkataba mzima.

Huku akinukuu barua za mawasiliano za kiserikali na kuainisha kumbukumbu zake, Zitto ambaye sasa amejivunia umaarufu mkubwa kitaifa, anasema iwapo Bunge lingekubali kuunda Kamati Teule kuchunguza mazingira ya utiaji wa saini wa mkataba huo wa madini, huenda mambo mengi yangefichuka.

Miongoni mwa barua ambazo Zitto anazinukuu ni ile ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Madini, iliyokutana siku moja tu kabla ya Februari 16, ambayo ndiyo iliyotajwa na Barrick kuwa siku ambayo mkataba ungesainiwa.

“Barua kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Madini kwenda kwa Waziri wa Nishati na Madini ya Februari 16, yenye kumbukumbu namba CDB/143/01 iliyotiwa saini na Meja Jenerali mstaafu Godfrey Mang’enya, inanukuliwa ikisema, ‘…Ufafanuzi ulitolewa na Waziri wa Nishati na Madini kuhusu umuhimu wa kufunguliwa kwa mgodi huo na lengo la serikali kuingia mkataba huu kwa sasa…” anaandika Zitto akirejea barua hiyo.

Kwa tafsiri yake, Zitto anasema maneno hayo ya Mang’enya yanaonyesha kuwapo kwa uwezekano wa waziri kuishinikiza kamati ya ushauri kusaini mkataba, na kwamba Barrick walikuwa wameahidiwa mradi huo hata kabla ya kamati hiyo kukutana.

Kutokana na hilo, mbunge huyo anahoji iweje Kamati ya Ushauri ya Madini iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini, namba tano ya mwaka 1998 isipewe uzito hata mkataba kukubaliwa kabla yenyewe haijaidhinisha kufanya hivyo.

“Barrick wamenukuliwa wakisema eti, mkataba ulikuwa usainiwe Februari 16. Ina maana walipanga siku ya kusaini mkataba kabla ya wanasheria wetu kupitia mkataba na kuukubali,” anasema Zitto kwa mshangao.

Mbali ya hayo, mbunge huyo katika waraka wake huo, anaonekana kuja na mambo mengine mapya nje ya ule mkataba wa Buzwagi, akiandika kuwa kumbukumbu nyingine zinaonyesha kuwa, huko London makubaliano mengine zaidi yanayohusu miradi ya madini yalisainiwa.

“Hivyo, kule Uingereza kilichosainiwa sio Mkataba wa Buzwagi peke yake, bali mabadiliko kadhaa ya mikataba mingine. Kimsingi ukiachana na viongozi wachache, taifa halijui nini kilibadilishwa katika mikataba yote ya Barrick. Licha ya haya yote, serikali inasema taratibu zote zilifuatwa,” anaeleza Zitto kwa mshangao.

Mbali ya Zitto kuzungumzia utata katika tarehe za vikao hadi kufikikiwa kwa makubaliano ya kusainiwa kwa mkataba huo, mbunge huyo anahoji ni kwa namna gani, mihuri na maofisa wote wa serikali na wale wa Barrick waliweza kusafiri katika kipindi cha siku moja tu hadi London na kutia saini mkataba iwapo suala hilo lilikuwa halijafikiwa mapema zaidi.

Aidha, Zitto anasema kabla ya Barrick kuitisha mkutano huo na waandishi wa habari juzi, alikuwa amepokea ujumbe wa maandishi wa simu ya mkononi uliokuwa ukitoka kwa ofisa mmoja wa juu wa Barrick, kwenda kwa Waziri wa Nishati na Madini.

Zitto anasema katika waraka huo kuwa, ofisa huyo wa Barrick alikuwa akimueleza kuhusu uamuzi wa kampuni hiyo kuitisha mkutano na waandishi wa habari na akaahidi kumtumia rasimu ya kile atakachowaeleza waandishi wa habari ili wao (Barrick) na waziri wawe na msimamo mmoja.

Zitto anasema maelekezo ya namna hii, iwapo kweli yalitoka kwa ofisa wa juu wa Barrick kwenda kwa waziri, basi ni ushahidi wa namna kampuni hiyo ilivyo na uhusiano usiofaa na kiongozi huyo, hata kufikia hatua ya kutoa maelekezo serikalini.

“Hata hivyo, sikutaka kuamini kuwa Waziri wa Tanzania anaweza kuandikiwa ujumbe wa namna hiyo na mwekezaji ili kuweka msimamo mmoja kati ya serikali na mwekezaji mbele ya Watanzania juu ya jambo lenye maslahi kwa taifa,” anaeleza mshangao wake Zitto akinukuu ujumbe huo wa maandishi.

Zitto anaonekana kuendeleza ajenda yake dhidi ya Barrick wakati kukiwa na taarifa kuwa, kundi moja ndani ya serikali na kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) limeshaanza kujiandaa kutafuta namna ya kuporomosha umaarufu wake wa kisiasa kwa kujenga hoja mbadala.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.