ALIYEWAHI kuwa mume wa Mbunge wa Viti Maalumu, marehemu Amina Chifupa (UVCCM), Mohammed ‘Meddy’ Mpakanjia, aliyelazwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, hali yake ni mbaya na sasa analishwa kwa kutumia mirija.
Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka Hospitali ya Lugalo vimeieleza Tanzania Daima juzi na jana kuwa Mpakanjia aliyefikishwa hospitalini hapo Jumanne jioni, hali yake inazidi kuwa mbaya, kwa kuwa hivi sasa amewekewa mirija, ili iweze kumsaidia kula.
Pia vyanzo hivyo vya habari, vilieleza kuwa Mpakanjia ambaye ni mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, amewekewa mirija kwa ajili ya kutolea haja ndogo.
Vyanzo hivyo vilieleza kuwa licha ya hali yake kuwa mbaya, Mpakanjia aliyefikishwa hospitalini alilazwa katika wodi ndogo namba 11 ya wagonjwa Maalumu (VIP), juzi alihamishiwa kwenye wodi ya watu maarufu namba 2 (VIP) iliyopo hospitalini hapo.
Vyanzo hivyo vinaeleza kuwa Mpakanjia, amekuwa akizungumza maneno yasiyoeleweka kwa binadamu wa kawaida na kuongeza kuwa ana mental confusion.
“Mpakanjia juzi amehamishiwa hapa wodi ya VIP na hali yake ni mbaya, anakula kwa kutumia mirija....hajielewi na anachozungumza hakieleweki. Hali yake inasikitisha sana, kwani hata nguvu za kusimama kitandani hana, mwili wake umedhoofu,” kilieza chanzo chetu cha habari.
Mpakanjia alikuwa mume wa Amina aliyefariki dunia Juni 26 mwaka huu, katika Hospital hiyo hiyo ya Jeshi ya Lugalo, alikuwa amelazwa kwa takriban wiki moja akiugua homa kali na kisukari.
Aidha, gazeti hili juzi na jana limewashuhudia baadhi ya ndugu wa Mpakanjia wakiingia hospitalini hapo kumjulia hali.