Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Chaguzi CCM vurugu tupu
Chaguzi CCM vurugu tupu
By Habari Tanzania | Published  08/26/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu


WAKATI chaguzi za ngazi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapindizi (CCM), zikiwa zinakaribia, kampeni ya uchaguzi huo zimetawaliwa na wanachama wa chama hicho kugawanyika katika makundi na kufanyiana kampeni chafu na za kikabila miongoni mwa wagombea hao.

Baadhi ya viongozi wa chama hicho Zanzibar, wameanza kuvurugana katika ngazi mbalimbali za uchaguzi huo.

Uchunguzi wa Tanzania Daima sehemu mbalimbali nchini zikiwamo Unguja na Pemba, umegundua baadhi ya wagombea hivi sasa wameingia katika mvutano mkubwa na kuibua upya makundi ya wagombea urais katika mwaka 2010.

Mvutano mkubwa umetoa katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, Kaskazini Unguja na Wilaya ya Mjini katika Jimbo la Chumbuni.

Huko Kaskazini Pemba, Mkuu wa Mkoa huo, Dadi Faki Dadi, amelazimika kuwaita viongozi wa Serikali za Mitaa (masheha) na kuwatisha kuwa watabeba lawama kwa lolote litakalotokea, iwapo yeye ataanguka katika kuwania nafasi ya NEC.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi ya Wilaya ya Wete, zinasema hali hiyo imetokana na ushindani mkali anaoupata kutoka kwa mpinzani wake mkubwa, Mwakilishi wa zamani wa Jimbo la Micheweni, Rashid Hamad, ambapo pia wamo Naibu Waziri wa Miundombinu, Maua Daftari na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii, Issa Ahmed Othman.

Hali hiyo imesababisha kuwepo migongano ya kisiasa kati ya Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Mbelwa Hamad Mbelwa, na baadhi ya wagombea katika kinyang’anyiro hicho.

Kutokana na wasiwasi wa vigogo wengi kuanguka, barua za vitisho kutoka utumishi zimesambazwa kwa wagombea ambao pia ni watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zikiwataka wachague moja, kuwepo kazini serikalini au utumishi katika chama.

“Barua hizi zimepotoshwa kama kuacha utumishi serikalini, mbona sheria hii ipo tokea kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, na haijatumika hadi safari hii, hizi ni njama za kuwatisha vijana wanaowapa changamoto wazee ving’ang’anizi,” alisema mgombea mmoja kutoka maskani ya Kizota.

Alitoa mfano wa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Idd Pandu Hassan, amekuwa mjumbe wa NEC kwa zaidi ya miaka 15 wakati ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Wana CCM hao walisema kwamba sheria ya utumishi Zanzibar inasema kwamba mtu anapaswa kuacha nafasi ya utendaji serikalini baada ya kuchaguliwa, lakini katika hatua hiyo anapaswa kuchukua likizo bila malipo na kama ataanguka anapaswa kurudi kazini.

Kishindo kikubwa zaidi kimejitokeza katika Jimbo la Chumbuni, ambapo Mbunge wake, Omar Sheha Mussa, anachuana vikali na Mwakilishi wa jimbo hilo, Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi, Machano Othman Said, ambao wamekuwa mahasimu.

Mvutano mkali wa viongozi hao umekuja kwa kila mmoja kutaka mwenzake ang’oke na kila upande kujaribu kuwa na wajumbe wengi wa kamati ya siasa ya jimbo ambao watakuja kupiga kura katika hatua za kura za maoni kwa wagombea ubunge na uwakilishi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Jimbo hilo la Chumbuni lilifanya uchaguzi, ambapo uchunguzi wetu umebaini kambi ya mbunge imepata ushindi mkubwa kwa kuibuka na wajumbe wengi wa kamati ya siasa ya jimbo kuanzia ngazi ya mwenyekiti hadi ujumbe wa halmashauri ya jimbo.

Hata hivyo, katika uchaguzi huo nafasi tatu za Katibu wa jimbo, Katibu wa Siasa na Uenezi na Katibu wa Fedha na Uchumi, zilishindwa kutoa washindi kutokana na mvutano uliojitokeza.

Mgogoro huo hivi sasa umewasilishwa katika ofisi ya chama Wilaya ya Mjini, ambapo Katibu wa Chama wa Wilaya, Aziza Ramadhan Mapuri, alitangaza kuahirisha uchaguzi katika nafasi tatu hizo.

Kutokana na ushindi wa kambi ya mbunge, baadhi ya wafuasi wa mbunge huyo wamekuwa wakitoa maneno ya kejeli kwa mwakilishi ambaye ni waziri katika Baraza la Mawaziri Zanzibar, kwa kuitangaza nafasi yake ya uwakilishi kuwa iko wazi kwa mtu yeyote anayetaka kugombea katika uchaguzi ujao.

Kinachoonekana katika uchaguzi huo ni makundi mawili kati ya mwakilishi na mbunge, ambapo inaaminika mbunge ni kambi ya Dk. Salmin Amour, ambayo inapanga kumsimamisha Dk. Mohammed Gharib Bilal na mwakilishi yuko kambi ya Rais Karume ambayo hadi sasa mgombea wake anadaiwa kuwa Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein.

Kambi ya Dk. Salmin imeonekana hadi sasa wagombea wake wengi kuwa tishio hasa katika Mkoa wa Kaskazni Unguja na Mjini Magharibi.

Mwakilishi wa Chumbuni, Machano Othman Said, pamoja na Mwakilishi wa Donge, ambaye ni Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna, wanaonekana kama wasaliti wa kundi la Dk. Salmin tangu kuingizwa katika utawala wa Rais Karume na hivyo baadhi ya wana CCM wa kambi hiyo kuahidi kuwafundisha siasa kupitia chaguzi zinazoendelea.

Mchuano mwingine hivi sasa unaoonekana ni kati ya Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohammed Aboud na kundi la Dk. Bilal ambao wote wanadaiwa wapambe wao wapo katika pirika kubwa kutafuta wajumbe wa kutosha watakaoingia katika ujumbe wa NEC na mkutano mkuu, wamekasilishwa na hatua ya Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa habari, Ali Juma Shamuhuna, kuamua kuwania nafasi ya urais 2010.

Mafanikio katika kampeni hiyo yameelezwa ndiyo turufu pekee ya kuwavusha katika malengo yao ya kuwania urais wa Zanzibar hapo mwaka 2010 baada ya Rais Karume kumaliza muda wake wa mihula miwili.

Hata hivyo, wazee wanaomshawishi Rais Karume kutafuta njia za kubadilisha katiba ili aweze kuendelea, wanaonekana bado hawajavunjika moyo pamoja na Rais Karume kutangaza hadharani kwamba hana mpango wa kubadilisha katiba kwa nia ya kutaka kuendelea na urais wa Zanzibar.

Wazee hao wa CCM katika hoja yao wanadai kwamba Rais Karume amefanya kazi nzuri katika utawala wake hivyo wana wasiwasi wa kutopatikana mtu mwenye uwezo kama wake.

Huko Magu, wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa CCM wilayani Magu, Mwanza wameanza kutoleana matusi na kashfa nzito.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na baadhi ya wagombea, vigogo wawili wa chama hicho waliokuwa wakipewa nafasi ya kushinda kwenye uchaguzi huo wameanza kutoleana matusi, kashfa nzito na kusababisha baadhi ya wanachama kupoteza matumaini kwao na kuanza kumuunga mkono mgombea ambaye hakuwa na nguvu hapo awali.

Kutokana na hatua hiyo, wagonmbea hao waliitwa kwenye kikao cha chama juzi na kuonywa, lakini bado wanaendelea kufanya kampeni za kuchafuana.

Kadhalika, habari kutoka mkoani Morogoro, zinaeleza kwamba chama hicho kimesema kitawanyang’anya ushindi wagombea watakaobainika kushindwa kutokana na kutoa rushwa.

Katibu wa chama hicho Wilaya ya Morogoro, Kapteni mstaafu, Nicolaus Mvanga, amekaririwa akisema kuna taarifa ambazo zinadaiwa kufanywa na baadhi ya wagombea, kufanya vitendo hivyo.

Alisema habari zaidi zinadai viongozi hao watarajiwa wamekuwa wakienda kwa wajumbe saa za usiku kuwashawishi wajumbe kuwapigia kura kwa njia ya kuwapa kushwa kama moja ya njia ya kuwashukuru.

Alisema kutokana na taarifa hizo chama hicho kitamemchukulia hatua mgombea atakayebainika kutoa rushwa kwa wajumbe, ili wamchague, atasimamishwa kushiriki katika shughuli za chama ambapo kitajadili ni kwa muda gani.

Habari kutoka Arusha zinaeleza kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Yona Nko (Ng’ara), amekerwa na tabia ya baadhi ya wanachama wa chama hicho wilayani Arusha kutaka kuchagua viongozi kwa kutumia vigezo vya ukabila badala ya kuzingatia uwezo wa mwanachama.

Nko, alisema iwapo wajumbe hao wataukumbatia utaratibu huo wa kihuni wa kuchagua viongozi kwa kutumia ukabila badala ya kuzingatia jinsia na uwezo, unakisambaratisha na unakiua chama hicho ambacho kimejengwa katika misingi imara ambayo hairuhusu ubaguzi wa aina yoyote ile kwa wanachama.

“Tunapofanya uchaguzi wa viongozi wetu lazima tuzingatie misingi ya chama ambayo ni umoja, na tambueni kuwa ubaguzi wa aina yoyote ile ndani ya chama kuwa hauna nafasi, hivyo chonde chonde ninawaomba wajumbe msitumie ukabila wala ubaguzi wa aina yoyote ile, chagueni mtu kwa uwezo wake,” alikaririwa Nko.

Aliwaonya wanachama hao wasiwe kama wenzao wa Mkoa wa Mara ambao wametishia kupiga kura za maruhani na kuhoji wanamkomoa nani.

Wakati huohuo, habari kutoka Tanga, zinaeleza kuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Yusuph Makamba, amewataka viongozi wa chama hicho kutokuogopa kupoteza nafasi zao kwa kuwashawishi wapinzani na wanachama wapya kujiunga na CCM, badala yake wafanye kazi hiyo kwa masilahi ya chama.

Makamba, alitoa wito kwa wanachama ikiwa ni pamoja na viongozi wa chama hicho waliowahi kushika madaraka kutokujihusiha na vitendo vya kutumia fedha, ili kuweza kupata uongozi kwa madai kwamba vitendo hivyo ni rushwa.

Alitoa msimamo wake huo wakati akizungumza na wanachama wa CCM ambapo alisema kuchaguliwa kwa viongozi wa namna hiyo ni kupoteza ridhaa yao ya kupata viongozi wasio thabiti wenye nia ya kuwaletea Watanzania haki na usawa katika hali zote.

Aliwataka wanachama wa CCM kuwanyima kura watu wanaotumia njia kama hizo na kubainisha kwamba dawa yao ni kuwanyima kura siku ya uchaguzi, kwani hawana nia ya kukisaidia chama bali wanaangalia masilahi binafsi.

Taarifa hii imeandaliwa na Osoro Nyawangah, Riziki Mwakyoma, Mustafa Leu, Mashaka Kibaya na Mwandishi Wetu kutoka Zanzibar


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.