Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Waziri wa JK matatani
Waziri wa JK matatani
By Habari Tanzania | Published  08/26/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Adili Gurumo na Robert Hokororo


WAFANYAKAZI mkoani Dar es Salaam kupitia Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), wametishia kuandamana kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete kumwondoa madarakani Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia.

Wametoa tishio hilo kwa kile walichodai kwamba, waziri huyo amewadharau kutokana na kuyapuuza madai yao ya nyongeza ya mishahara na kukebehi maandamano yao ya amani hivi karibuni.

Msimamo wa wafanyakazi hao ulitolewa jana na Mwenyekiti wa wafanyakazi hao, Bohari Semvua, alipozungumza na waandishi wa habari katika Idara ya Habari (MAELEZO).

Semvua, amesema waziri huyo amewadharau kwa kutoa kauli kuwa wafanyakazi ni sehemu ndogo katika jamii ya Watanzania.

“Waziri alikosa upeo wa kutosha kuchambua umuhimu na maana ya wafanyakazi, kwani wafanyakazi wa nchi wakisaidiana na wakulima ndio waliojitoa mhanga katika harakati za kudai uhuru, hivyo hiyo ni dharau kubwa kwetu,” alisema.

Alisema lengo la maandamano yao yaliyofanyika Agosti 11 mwaka huu ni kuijulisha serikali kuwa hawatoshelezwi na nyongeza ya mishahara iliyoko kwenye bajeti ya mwaka, kwani mshahara huo hautoshelezi mahitaji ya mtumishi wa kawaida kwa mwezi mzima.

“Lengo la maandamano lilikuwa ni kuijulisha serikali wafanyakazi hawaridhishwi na nyongeza hiyo ya mishahara kutoka sh 75,000 hadi sh 84,000 ambayo haitoshi. Tunahitaji angalau sh 315,000 kwa mwezi, ili tuweze kujikimu na ukali wa maisha,” alisema Semvua.

Semvua, alisema iwapo waziri huyo asipowaomba radhi, wataandamana hadi kwa Rais Kikwete, kumshinikiza amuondoe, kwani inaonekana hafai.

Pia wafanyakazi wameleeza kushangazwa na serikali katika kufanya maamuzi hayo ya kupanga nyongeza hiyo ya mishahara bila kuwashirikisha, kwani ni kitendo cha kuwanyanyapaa.

Mwenyekiti huyo alisema Rais Kikwete, alimteua waziri huyo ili amuwakilishe na kuwatumikia wananchi hata kama angekuwa anamtumikia mtu mmoja anapaswa kuheshimu na kujali utu wake ili kuongeza tija.

Alisema wafanyakazi wanapenda kumjulisha kuwa hata kama anajiamini kwa sababu yoyote ile kama kinga kwake, kinga hiyo haiwezi kuzishinda nguvu za wananchi kwa msukumo wa watu watakaosema hapana, kwani yamejitokeza sehemu nyingi duniani na wafanyakazi wa Tanzania wanalazamika kufanya hivyo na viongozi wenye tabia kama zake.

Aidha, wafanyakazi hao wameonyesha kusikitishwa na kauli ya Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, John Chiligiti, kuwa walioandamana walishauriwa na kikundi cha watu wachache na haoni athari za maandamano hayo, kwa kuwa mgomo ulifanyika Jumamosi.

Pia walimtaka Waziri Chiligati kutambua kuwa yale yalikuwa ni maandamano na si mgomo kama alivyouita wakati akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni.

Semvua alisisitiza kuwa wao walitumia ustaarabu wa hali ya juu kuandamana Jumamosi ambayo ni siku ya mapumziko, ili kudai masilahi yao bila kuathiri shughuli nyingine na pia kumtahadharisha Chiligati kuwa kama anahitaji kuona migomo na maandamano ya katikati ya wiki, asubiri baada ya Septemba 20 atashuhudia migomo hiyo.

“Labda Waziri angependa ufanyike mgomo wenye kuathiri huduma kwa wananchi na uchumi ndipo angesikia uchungu na hata kujadiliana na wafanyakazi kama anachotaka ni kushuhudia hayo basi asubiri baada ya Septemba 20 tutafanya hivyo,” alisema Semvua.

Wafanyakazi mkoani Dar es Salaam, Agosti 11 mwaka huu walifanya maandamano ya amani, ili kuikumbusha serikali kuhusu matatizo wanayoyapata kutokana na mishahara midogo na kuipa serikali siku 30 kutimiza matakwa yao.

Katika mkutano huo, wafanyakazi hao, walimtuma Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Nestory Ngulla, kuwasilisha malalamiko yao hayo kwa Rais Kikwete na kurejesha majibu ndani ya siku 30, ili wasichukue hatua kali zaidi za kudai masilahi bora ya kazi.

Kilio cha wafanyakazi hao kimekuja baada ya kuona ndoto zao za kuingia katika maisha bora kama ilivyokuwa imeahidiwa na Rais Kikwete, zikielekea kuyeyuka, kwani tangu aingie madarakani mwishoni mwa mwaka 2005, hakuwahi kuongeza mshahara, hadi Juni mwaka huu wakati Waziri Ghasia alipowasilisha bungeni makadirio ya wizara yake na kuonyesha kwamba, kutakuwa na ongezeko la mishahara la asilimia 17, ambako kwa kima cha chini, ni sawa na nyongeza ya sh 9,000. Kima kipya cha mshahara kwa mujibu wa mabadiliko hayo ni sh 84,000 kilichopanda kutoka sh 75,000.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.