MWANAZUONI maarufu hapa nchini na bingwa wa masuala ya sheria, Issa Shivji, amesema moto aliouwasha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), ni kielelezo cha wananchi kuchoshwa na dhuluma inayoendeshwa dhidi ya rasilimali zao.
Shivji ambaye ni profesa mstaafu wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ameyasema hayo katika makala yake ya maandishi iliyosambazwa katika mtandao wa intaneti kuanzia jana alfajiri.
“Zitto aliposema kuwa alikuwa akitaka kutoa hoja binafsi kuchunguza utiaji wa saini wa mkataba wa Buzwagi, aligusa kwa undani kabisa hisia za umma na akaamsha manung’uniko kutoka kwa watu.
“Alichofanya (Zitto) kilikuwa ni kuonyesha wasiwasi wa watu wengi dhidi mfumo wa ubinafsishaji,” anasema Shivji katika makala yake hiyo.
Msomi huyo amekielezea kitendo kilichofanywa na Bunge kumsimamisha Zitto kuwa ni sawa na kumwaga mafuta ya petroli katika moto uliokuwa tayari ukiwaka.
Alisema hatua hiyo ya kumsimamisha ambayo ilichukuliwa kinyume kabisa cha misingi ya kisheria, kanuni na Bunge na haki, iligeuza manung’uniko ya mtu mmoja (Zitto) kuwa hasira kwa jamii kubwa zaidi ya wananchi.
Msomi huyo ambaye jana aliithibitishia Tanzania Daima kwa njia ya simu kuwa makala hiyo ni yake, anasema hali ya mambo inavyokwenda sasa, imesababisha wananchi walio wengi hususan wale wenye kipato cha chini kuishi kwa tabu, huku wakiwa na mikanganyiko mingi ya kimaisha.
Kwa mujibu wa Shivji, hali hii ya mambo, imesababisha kwa upande mmoja, kuwapo kwa kundi dogo la wananchi waroho, lililojilimbikizia utajiri mkubwa wa mali aliloliita ‘walalaheri’.
Aidha, msomi huyo mwenye rekodi iliyotukuka na ambaye kauli zake zimekuwa zikilenga kuwatetea maskini, wakulima na wafanyakazi dhidi ya mfumo wa utandawazi, alisema kundi kubwa la watu wenye hasira ni lile la ‘walalahoi’ wanaoishi katika maisha ya kukatisha tamaa, wakijaribu bila ya mafanikio kuhakikisha kuwa, mioyo yao inakidhi matakwa ya kimwili.
Shivji, ambaye aliieleza Tanzania Daima kuwa makala yake hiyo ilikuwa ikitarajia kuchapishwa katika gazeti la leo la ‘The Citizen’, aliuponda mfumo wa ubinafsishaji na umilikishaji wa mitaji mikubwa kwa kile alichokiita kuwa ni kuwaacha nje ya mfumo huo wakiwa hawana cha kufanya watu wengi.
Akitoa mfano, Shivji anasema katika makala yake hiyo kuwa, wakati wa utawala wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, tofauti ya kipato kati ya kiwango cha chini cha mshahara na cha juu kilikuwa katika uwiano wa 1 hadi 8, tofauti na sasa ambapo uwiano huo umepanda na kufikia 1 na 50.
Shivji katika makala yake hiyo anasema, ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, dhamira mbaya ya kujilimbikizia mali waliyonayo viongozi wengi hivi sasa, imesababisha wafikie hatua hata ya kushindwa kusoma hisia za wananchi walio wengi.
Anasema kushindwa huko kusoma alama za nyakati ndiko ambako kulisababisha washindwe kubaini nguvu ya hoja ya Zitto, jambo ambalo hatimaye limesababisha Bunge lijikute likiwa katika wakati mgumu kabisa wa kujaribu kupoza mambo kwa kutoa taarifa nyingi za kuweka mambo sawa.
Shivji anasema taarifa mbili tofauti za Bunge, ya kwanza ikiwa ni ile iliyotolewa na Katibu wa Bunge na ile ya Naibu Spika wa Bunge, Anne Makinda, zote kwa pamoja zimethibitisha kuwa, uamuzi wa kumsimamisha Zitto haukufanywa kisheria na kihalali.
Akirejea kanuni za Bunge, Shivji alisema uamuzi wa Bunge kutumia kifungu cha 59 (3) kumsimamisha Zitto, ulifanywa kimakosa, kwani utekelezwaji wake ulifanywa pasipo kwanza kukidhi matakwa ya vifungu vingine viwili vya 59(1) na 59(2) ambavyo vilipaswa kutumika kabla.
Msomi huyo pia katika makala yake hiyo, anasema kuwa, uamuzi wa Bunge kumuona Zitto muongo kwa sababu tu ya kukubaliana na maelezo ya Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, nao umeonyesha mapungufu makubwa.
Shivji alisema, hoja kwamba Zitto alikuwa amelidanganya Bunge ama la, ilipaswa kutolewa na Spika, na si Karamagi kama inavyoelekezwa katika vifungu vya 59 (1) na 59 (2) vya kanuni za Bunge.