WANANCHI wa Kahama, wamesema walimzomea Mbunge wao, James Lembeli (CCM), kwa kuwa alishindwa kuzungumzia sakata la utiaji saini mkataba wa uchimbaji wa dhahabu wa Buzwagi, hivyo kukosa imani kwake.
Wananchi hao wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti jana, walisema kitendo cha mbunge huyo kunyamaza kuhusu suala hilo kimewashitua.
Mbunge huyo alizomewa na wananchi hao alipokuwa akitambulishwa na Rais Jakaya Kiwete ambaye yuko katika ziara ya siku nane mkoani Shinyanga.
Hata hivyo katika mkutano huo, neema ilimuangukia Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, ambaye alishangiliwa na wananchi hao alipotambulishwa kwa wananchi, ambaye walimfananisha na Mbunge Zitto Kabwe (CHADEMA), wakidai amefanikisha mgogoro wa Kijiiji cha Kakola, ambapo Rais Kikwete aliwahutubia na kuwahakikishia kuwa hawatahamishwa kama ilivyokuwa imeamriwa na serikali hapo awali.
Wakati wakimzomea mbunge wao, wananchi hao walimtaka Rais Kikwete kuondoka naye, kwa madai kuwa ameshindwa kuwatetea wananchi wa Buzwagi.
Pia wamedai tangu achaguliwe amewagawa katika makundi baadhi ya wawakilishi wao katika halmashauri yao ya wilaya, hasa madiwani, ambapo amekuwa akishinikiza migogoro iliyokwamisha maendeleo ya wilaya yao na kugombana na watumishi mbalimbali wa idara za Serikali kwa chuki binafsi.
Kuzomewa kwa mbunge huyo kumezua mijadala mbalimbali ikiwemo ya kumkumbatia kigogo mmoja wa CCM mwenye tuhuma mbalimbali za makosa ya jinai.
Lembeli alikaririwa akilalamika kuzomewa kwake na kudai kuwa huenda ni njama zilizoandaliwa, ili kumharibia jina mbele ya rais, kwa kuwa aliposimama tu, mtu mmoja alipiga mluzi na ndipo umati mkubwa ulipoanza kumzomea kwa nguvu.