KIWINGU cha hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini aliyesimamishwa, Kabwe Zubeir Zitto (Chadema), ya kupinga utiaji saini wa mkataba wa uchimbaji madini kati ya Kampuni ya Barrick Gold Mine na Waziri wa Nishati na Madini, sasa linaonekana kupanda juu na kumfikia Rais Jakaya Kikwete.
Hali hiyo ilijionyesha jana wakati Rais Kikwete alipokuwa ndiyo kwanza ameanza ziara yake ya kikazi mkoani hapa, kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo, zikiwamo zile za madini.
Akizungumza mbele ya Rais Kikwete, Mkurugenzi wa Barrick, Deo Mnyika, alisema kampuni yake ilikuwa imesikitishwa na hoja hiyo ya Zitto ambayo mbali ya kumuelekeza Waziri Nazir Karamagi, ilikuwa ikigusa moja kwa moja maslahi yao pia.
Kikwete alikutana na ujumbe huo wa Barrick wakati alipotembelea mgodi wa Bulyanhulu, ambao ni moja kati ya miradi minne ya uchimbaji wa madini inayoendeshwa na kampuni hiyo, mbali ya ule wa Buzwagi ambao ndiyo uliozaa hoja ya Zitto, hata kusababisha Bunge lifikie hatua ya kumsimamisha kwa miezi mitano.
Mnyika, alisema utiaji saini wa mkataba huo ulizingatia taratibu zote, na kwamba ulilazimika kusainiwa Uingereza kwa kuwa muda wa kufunga mkataba ulikuwa umewadia.
Alisema wao ndio waliomfuata Waziri Karamagi nchini Uingereza ambaye alikuwa katika ziara na Rais Kikwete.
Mnyika alisema wao hawana ofisi nchini Uingereza, bali makao makuu ya kampuni hiyo ya Barrick yapo Toronto, nchini Canada.
Kuhusu kulipwa fidia kwa wananchi wanaoishi jirani na eneo la mgodi wa Buzwagi, mkurugenzi huyo, alisema kuna makundi mawili ya wananchi (kundi la watu 25 na 12), ambao wamegoma kuhama kwa madai kuwa kiwango cha fidia hakilingani na thamani ya mali zao zilizopo.
Aidha, katika Kijiji cha Kakula, kilicho jirani na mgodi wa Bulyanhulu, Rais Kikwete alikutana na mabango ya wananchi waliokuwa wamebeba mabango mbalimbali wakiomba wasihamishwe katika eneo hilo.
Pia wananachi hao katika mabango yao hayo, walieleza matatizo yanayowakabili ambayo ni tatizo la umeme, ajira na barabara.
Akijibu ujumbe wa mabango hayo, alipowahutubia jana, Rais Kikwete, aliwahakikishia wananchi hao kwamba hawatahamishwa.
Kuhusu suala la ajira, alisema kampuni hiyo imeshatoa ajira 1,500 na kwamba itaendelea kutoa ajira kulingana na mahitaji yao.
Ingawa rais alipopata fursa ya kuhutubia katika eneo hilo, hakugusia kuhusu malalamiko hayo ya Barrick kuhusu hoja ya Zitto, aliishukuru kampuni hiyo kwa kuboresha huduma za kijamii, ikiwamo kuwajengea nyumba bora wananchi wa Bulyanhulu.
Rais aliwataka wawekezaji wengine nchini, kuhakikisha wanaiga mfano wa Barrick katika kuwajali wananchi kwa kuwapatia huduma bora wanazohitaji.
Kwa mara ya kwanza, hoja ya Zitto kuhusu mkataba wa Buzwagi, ambao kwa wiki moja sasa imekuwa ndiyo ajenda kuu katika vyombo vya habari, ilianza Julai 17, mwaka huu, siku Waziri Karamagi alipowasilisha makadirio na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2007/08.
Zitto katika hoja yake hiyo, aliahidi kuwasilisha hoja ya maandishi akilitaka Bunge kuunda kamati teule ya kuchunguza uamuzi wa Karamagi wa kusaini mkataba huo London, Uingereza na tena baada ya rais kutangaza kuwa, serikali ilikuwa imesitisha mikataba mipya ya madini hadi baada ya kamati aliyoiunda kuhusu utata uliopo katika mikataba hiyo kumaliza kazi yake.
Zitto, mbunge mdogo kuliko wote wa kuchaguliwa, alitoa rai hiyo muda mfupi baada ya Bunge kupitisha bajeti ya wizara hiyo, jioni ya siku hiyo hiyo.
Kikubwa kilichomfanya mbunge huyo afikie uamuzi huo wa kutaka kuchunguzwa kwa Karamagi, kilikuwa ni majibu ya waziri huyo kuhusu uamuzi wake wa kusaini mkataba wa madini kati ya serikali na kampuni ya madini ya Barrick nje ya nchi.
Zitto aliielezea hatua hiyo ya Karamagi kuwa inayokwenda kinyume na maelekezo ya Rais Kikwete ya kutosainiwa kwa mkataba wowote mpya kabla ya kazi ya kuhakiki mikataba ya zamani haijakamilishwa na ripoti kuwasilishwa na kamati maalum.
Aidha, mbali ya hilo, Zitto, mmoja wa wabunge machachari wa upinzani, aliliambia Bunge kuhusu kutoridhishwa kwake na majibu ya waziri huyo, juu ya uamuzi wake wa kusaini mkataba huo wa madini, Uingereza badala ya Dar es Salaam.
Alisema kuwa, sababu alizozitoa Karamagi kuhalalisha kuusaini mkataba huo nje ya nchi, bado hazijitoshelezi, hivyo upo umuhimu mkubwa wa suala hilo kuchunguzwa kwa kina na Bunge kama chombo huru kinachoisimamia serikali.
“Majibu kuhusu mkataba huo si sahihi. Waziri amedanganya katika majibu yake, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu, kwamba nitawasilisha hoja ya kimaandishi kutaka hoja hiyo iundiwe kamati teule ya kuchunguza,” alisema mbunge huyo Julai 17.
Akijibu hoja hizo za Zitto kwa mara ya kwanza hiyo Julai, Karamagi alikiri kusaini mkataba huo huko London, akisema alifanya hivyo kwa nia njema, akirejea historia yake ya kutokea katika sekta binafsi ambayo inamfanya aone suala la muda kuwa ni jambo muhimu.
Hata hivyo, alisema wakati akisaini mkataba huo, tayari ulikuwa umeshapitiwa na kuhakikiwa na timu ya wataalamu wa wizara yake, Mwanasheria Mkuu na Kamati ya Ushauri wa Madini kama taratibu zinavyotaka.
Jumanne iliyopita, baada ya kupata baraka za Spika wa Bunge, Zitto aliwasilisha hoja yake binafsi ya kutaka kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza utiaji saini huo.
Hata hivyo, baada ya Karamagi kupata fursa ya kuandaa majibu ya serikali kuhusu madai hayo, mjadala kuhusu hoja hiyo ya Zitto ulimalizika kwa Bunge kufikia uamuzi wa kumsimamisha ubunge kwa miezi mitano, akituhumiwa kusema uongo bungeni.
Uamuzi huo wa Bunge umepokelewa kwa malalamiko mengi kutoka kwa wanasiasa, hususan wale wa upinzani, wanaharakati na wanasheria mbalimbali ambao wanaiona hatua hiyo ya Bunge kuwa iliyochukuliwa kisiasa zaidi badala ya kikanuni na kisheria.
Tangu Bunge lipitishe uamuzi wake huo, umaarufu wa Zitto umepanda kwa haraka hadi kufikia hatua ya kumfanya awe ndiye gumzo kuu la kisiasa kwa kipindi chote hicho.