SIKU moja baada ya maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam kumpokea kwa kishindo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zuberi Zitto (CHADEMA), Bunge la Jamhuri ya Muungano limeibuka na kusema kuwa hoja ya msingi iliyotolewa na mbunge huyo na kusababisha kusimamishwa bado ina nguvu.
Hayo yalibainishwa na Naibu Spika, Anne Makinda, katika mkutano wa waandishi wa habari, uliotishwa jana kutoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na sakata la kusimamishwa kwa mbunge huyo kijana na mabadiliko yanayofanyika kuhusiana na kanuni za Bunge.
Zitto alisimamishwa na Bunge hadi Januari mwakani kutokana na hoja yake, iliyolenga kulitaka Bunge kuunda kamati teule, kuchunguza kutiwa saini kwa mkataba wa mgodi wa Buzwagi mkoani Shinyanga.
Zitto aliijenga hoja hiyo katika mazingira ya kutia shaka kutokana na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kusaini mkataba huo nje ya nchi, wakati ambapo kulikuwa na mchakato wa kupitia mikataba ya madini kutokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete.
Akifafanua, Makinda alisema kuwa kilichosababisha Zitto asimamishwe si hoja hiyo, bali lugha aliyoitumia wakati anawasilisha hoja yake.
Alisema kutokana na hali hiyo, mbunge huyo au mwingine anaweza kuleta tena hoja hiyo bungeni na ikajadiliwa, na iwapo kutakuwepo ushahidi wa kutosha, Bunge linaweza kuridhia kuundwa kwa kamati hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge, jijini Dar es Salaam, Naibu Spika, alisema kilichosababisha Zitto kusimamishwa kujishughulisha na kazi ya ubunge ni kutokana na kitendo chake cha kusema Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi ni muongo.
“Si hoja (ya kutaka kamati teule) ndiyo iliyosababisha Zitto asimamishwe, ni maneno yake ya kusema waziri amesema uongo,” alisema Naibu Spika ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Kusini (CCM).
Akifafanua zaidi, Makinda alisema Zitto alikuwa na nafasi na iwapo alipopewa nafasi ya kujitetea angeweza kuomba muda zaidi wa kutafuta ushahidi kuhusu suala hilo, Bunge lisingefikia uamuzi wa kumsimamisha.
Alisema kanuni ya 50 ya Bunge inapiga marufuku kwa mbunge kusema uongo, kukashifu, hivyo kutokana na hoja ya Zitto, siku hiyo walitarajia angebainisha uongo wa Waziri Karamagi.
Akaongeza kwamba kanuni ya 59 (3) inaeleza kwamba iwapo mbunge atathibitika amesema uongo na udhalilishaji ni mkubwa, mbunge yeyote anaweza kutumia kifungu hicho kuomba Bunge kumsimamisha kufanya kazi ya uwakilishi kwa muda atakaopendekeza.
Naibu Spika ambaye aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Wilson Masilinngi na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Biashara, Harrison Mwakyembe, alisema kutokana na hali hiyo, Zitto amesimamishwa siku 18 kuhudhuria vikao vya Bunge na hajakatazwa kufanya kazi katika jimbo lake.
Akielezea uzoefu wake bungeni, alisema wakati wa Bunge la chama kimoja kulikuwapo na wabunge kama Zitto akiwamo yeye (Anne), lakini walikuwa wakiikosoa serikali kwa hoja na si kwa kutoa lugha ya matusi.
“Tatizo hapa ni jinsi ya kutumia lugha bungeni. Kuna wakati nilimwita Zitto kumuasa, kwani maneno ya aina hiyo hayana msingi wowote na kwa kipindi kirefu alitii na imekuja kutokea juzi (Agosti 14).
“….wakati wa Bunge la chama kimoja (Waziri Mkuu Edward) Lowassa, alikuwa mbunge wa kwanza kuchachamalia suala la madini bungeni,” alisema.
Akionekana kuhusisha maoni ya wananchi waliyoyatoa baada ya tukio la kusimamishwa kwa Zitto, Makinda alisema inaonekana wnanchi wengi hawafahamu jinsi Bunge linavyoendeshwa.
Kutokana na hali hiyo, alisema upo umhimuwa na Ofisi ya Bunge inatarajia kuanzisha rasmi vipindi vya radio na televisheni kuwaelimisha wananchi jinsi Bunge linavyoendeshwa.
Hata hivyo, alisema kutokana na maoni ya wananchi baada ya tukio hilo, Bunge limepata changamoto na hivyo linatarajia kubadili kanuni zake ili katika kikao cha Oktoba zianze kutumika kanuni mpya, kwani zilizopo zilitengenezwa miaka 10 iliyopita.
Kuhusu adhabu kwa mbunge atayethibitika kusema uongo, Naibu Spika alisema katika kanuni zijazo wanatarajia adhabu hiyo kuwa kali zaidi, kwani wasipofanya hivyo watu hawataacha kulichezea Bunge.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Naibu Spika alisema suala la Zitto na Malima ni tofauti, kwa kuwa suala la Malima si hoja ya Bunge.
“Suala la Malima ni tofauti na Zitto. Suala la Malima si hoja ya Bunge na kutokana na malalamiko yaliyokuwapo kutoka kwa mlalamikiwa, Spika aliamua kuunda kamati kuchunguza madai hayo.
“Kulingana na kanuni zilizopo, mbunge akithibitika alichosema ni uongo na ni kosa lake la mara ya kwanza, Spika anaweza kumsamehe kama alivyofanya kwa Malima na Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe,” alisema.
Aidha, alisema yaliyozungumzwa juzi katika viwanja vya Jangwani na Zitto na Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA) hayakuligusa Bunge na kwamba endapo wangetumia jukwaa hilo kulikashifu Bunge, wangechukuliwa hatua kali zaidi.
Hata hivyo, alionya kuwa hata wanaharakati na wananchi wa kawaida ambao wanalizungumzia suala hilo, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria iwapo watabainika kutumia maneno ya kejeli dhidi ya Bunge na mawaziri.
Wakati huo huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, Harrison Mwakyembe, alisema kuwa kamati hiyo imeomba mkataba wa Richmond ujadiliwe bungeni, na kwamba anatarajia suala hilo litajadiliwa katika kikao kijacho cha Bunge.
Aidha, alisema kuwa baada ya kuuona mkataba huo na kuupitia, kamati hiyo itaomba pia kupatiwa mikataba ya madini wakati wa kufanya hivyo utakapofika.
Wakati huo huo, suala la kusimamishwa Zitto linazidi kuchukua sura mpya kila siku na sasa wito umetolewa na kiongozi mmoja wa dini kulitaka Bunge kuangalia upya kanuni zake.
Fatma Gaffus anaripoti kutoka Dodoma kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma, Dk. Peter Mwamasika, amelitaka Bunge kuziangalia upya kanuni zake na kuzifanyia marekebisho yanayopaswa ili ziwe za kidemokrasia zaidi.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Dk. Mwamasika aliwataka wananchi wasione kuwa Zitto ameonewa, bali tatizo lipo katika kanuni zinazoongoza shughuli za Bunge.
Alisema kuwa hata wanaomlaumu Spika, Samuel Sitta, hawamtendei haki kwani hata yeye analiongoza Bunge hilo kwa kufuata kanuni hizo na si matakwa yake binafsi.
Akizungumzia matukio tangu kusimamishwa kwa mbunge huyo, askofu huyo aliitaka serikali kutafakari kuungwa mkono kwa Zitto kunatokana na nini na kueleza kuwa kuungwa mkono kwa mbunge huyo ni changamoto kubwa kwa serikali.
Alisema mambo hayo yasingefika hapo yalipofika iwapo kungekuwa na utaratibu unaoeleweka na kukubalika unaoruhusu wazawa nao kushirikishwa na wawekezaji wakubwa katika sekta ya madini.