SIKU moja baada ya kufanyika maandamano makubwa ya kumpokea Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zuberi Zitto, yaliyohusisha vyama vya upinzani, Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila ameibuka na kusema kuwa anafikiria kufungua kesi juu ya hoja iliyosababisha mbunge huyo kusimamishwa.
Hata hivyo, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa maandamano ya kumpokea mbunge huyo yalikuwa ya kisiasa zaidi yakilenga kuvitangaza vyama hivyo badala ya kuzungumzia madai ya msingi.
Alisema kwamba yeye akiwa kama mmoja wa waanzilishi wa sakata la kashfa ya BoT angepaswa kupewa mwaliko ili awaeleze wananchi yale aliyonayo na badala yake vyama hivyo havikufanya hivyo na hata alivyowapigia simu walimjibu kuwa ni kweli kuwa mialiko wameituma kwa kila mhusika.
“Jambo hili lilisababisha kamati ya chama kuniweka chini na kuniambia kuwa kama hawajakualika haina haja ya wewe kwenda kwani kwa kufanya hivyo utakuwa sawa na kujikomba,” alisema.
Aidha, Mtikila aliponda uamuzi wa Chama cha Mawakili wa Afrika Mashariki kutaka kumpatia Zitto msaada wa kisheria na kusema kuwa mawakili hao wanashabikia siasa.
Alitoa mfano wa baadhi ya viongozi ambao wameshawahi kufukuzwa bila watu kufanya maandamano kama hayo kuwa ni Mbunge wa Chadema, Philemon Ndesamburo na Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema.
“Nilitegemea maandamano hayo yangefanywa kwa kupinga kanuni za Bunge ambazo zinaonekana kuwanyima wabunge kuwasilisha hoja ambazo wananchi wanataka kujua ukweli wake.
“Ningekuwa mimi ningewaoongoza wananchi hadi Ikulu kwenda kudai uhuru upya kwa sababu mpaka sasa nchi imeshauzwa ambapo wabunge tuliowatuma bungeni wanaonekana kutetea zaidi matumbo yao badala ya maslahi ya wananchi ambao wamewachagua. Bunge limekuwa la kupiga mihuri ya kuuza rasilimali za nchi,” alisema.
Aliyataja mambo ambayo atayadai kupitia kesi hiyo ni Bunge kukataa kuundwa kwa tume ya kuchunguza BoT, kuangaliwa upya kwa kanuni za Bunge na kuwachukulia hatua kali wale ambao wanazitumia kanuni hizo vibaya.
Aidha, katika kesi hiyo Mchungaji Mtikila atahusisha pia suala la serikali kukataa kupeleka mikataba ya uwekezaji bungeni.
Wakati huo huo, Mtikila alielezea kuhusu tukio la kuwekewa kitu anachodhani kuwa ni dawa za kulevya katika begi lake wakati akiwa safarini kutoka Mwanza kuja Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
Akielezea tukio hilo, alisema wakati akiwa Mwanza kwenye nyumba ya kulala wageni aliyoitaja kwa jina la Victoria Annex, aliacha begi lake sehemu ya mapokezi na kwenda kutafuta taxi.
Lakini baada ya kurudi hakulikuta begi hilo, kitendo kilichomfanya kumhoji mhudumu aliyekuwa mapokezi hapo ambapo alipolitafuta kwa muda mfupi alilipata.
“Bila ya mimi kutia shaka yoyote nilichukua begi langu na kutoka nalo nje, lakini kabla ya kulipakiza kwenye taxi niliyoikodi ndipo akaja mtoto wangu na gari jingine na nikamuambia dereva wa taxi aondoke.
Anasema kabla ya taxi ile kuondoka, aliona gari lenye rangi nyekundu likiwa na watu wawili ndani likioondoka kwa mwendo wa kasi katika eneo hilo, jambo ambalo alikuja kuhisi baadaye kuwa huenda ndio waliochukua begi lake na kumwekea dawa hizo bila ya yeye kujua.
Alisema dawa hizo ziligunduliwa katika begi na mkewe wakati akitoa vitu baada ya kuwasili nyumbani ambapo ilibainika pia kuwa zipu ya pembeni ilikuwa imefunguliwa na walipokung’uta ulitoka ungaunga.
“Baada ya mke wangu kuona vile akaja nalo sebuleni ambapo nilikuwa nina maongezi na wageni waliokuja kunitembelea na tulipolifungua tukakuta kimfuko cha nailoni kikiwa na unga mweupe, katika kimfuko cheusi ambacho chenyewe kilikuwa kimefungwa.
“Baada ya kuona vile mimi na wageni wangu tukashauriana kuupeleka unga huu leo kwa Mkemia Mkuu, Shirika la Viwango na chuo kikuu kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema.