CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetangaza kurejea katika meza ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa visiwani Zanzibar.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalimu Seif Sharrif Hamad, alitangaza uamuzi huo jana katika kongamano la siku moja la kujadili hali ya kisiasa visiwani humo, lililofanyika katika Hoteli ya Peacock, katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza mbele ya viongozi wakuu wa vyama vya upinzani, wasomi na wanaharakati, Maalim Seif alisema CUF imekubali kurejea katika meza ya mazungumzo kufuatia kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kutaka kuona mazungumzo hayo yanakamilishwa haraka kwa mafanikio.
Alisema CUF inarejea katika mazungumzo ikiamini kuwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitayapa mazungumzo hayo umuhimu unaohitajika ili kuondoa dhana iliyopo sasa kwamba hakina nia njema na utashi wa kweli wa kupata ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
“Uamuzi uko mikononi mwa Rais Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM. Tunaamini wakati umefika sasa atumie nafasi na madaraka yake kuhakikisha ufumbuzi wa tatizo hili unapatikana ili tujenge mustakabali mwema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” alisema Hamad.
Hata hivyo, alikanusha kauli ya Rais Kikwete kuwa, CUF ina nia ya kujiondoa katika mazungumzo na CCM, kwa kauli iliyoitoa mapema wiki hii.
“CUF inasisitiza kauli ya Rais kuwa, mazungumzo ni lazima yawe na ukomo, hivyo tunatarajia kikao cha mwanzo kitakachofanyika baada ya mazungumzo haya kuanza tena, kitaweka utaratibu wa hatua kwa hatua wa kuyakamilisha,” alisema Hamad.
Aliwalaumu viongozi wa CCM kuwa baadhi yao, kwa kipindi kirefu sasa wamekuwa wakifanya jitihada za kukionyesha CUF kama chama kisicho na subira na ustahimilivu.
Awali kabla ya Hamad hajatoa tamko hilo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid, aliwaeleza washiriki wa kongomano hilo kuwa tangu mazungumzo hayo yalipoanza hadi yalipofikia, pande zote mbili zilikubaliana yawe ya siri, lakini CCM kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Yusuf Makamba, aliamua kuanika yanayozungumzwa katika vikao hivyo.
“Hadi sasa tumeishafanya vikao 12, mazungumzo hayajamalizika, ikabidi tuanze kuhoji, lini mazungumzo haya yatamalizika? Manake tulikubaliana yamalizike Agoti15 mwaka huu na yafanyike kwa siri,” alisema Rashid.
Kuhusu makubaliano ya awali yaliyokwisha kufikiwa katika mazungumzo hayo, alisema CCM ilikubali ifikapo mwaka 2010 kuundwa kwa serikali shirikishi, lakini baadaye ilianza kuipiga danadana ahadi yake hiyo.
Katika hatua nyingine wanaharakati, viongozi wadini, na wasomi wakizungumza katika kongamano hilo, waliilaumu CCM kwa kuonyesha kutokuwa na dhamira ya dhati ya kumaliza mazungumzo.
Wakili Mabere Marando, ambaye ni mmoja wa wanasheria waliotoa maoni yao katika kongamano hilo, alisema CCM hawataki mazungumzo hayo bali wanachokifanya ni kuihadaa CUF na wananchi kwa ujumla kuwa wanataka mwafaka.
Aliwataka viongozi wa vyama vya upinzani kutambua kazi kubwa iliyo mbele yao ya kuwahamasisha Watanzania kuiasi CCM, ili ishtuke na kuwa makini kutekeleza madai ya wananchi.
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Augustine Lyatonga Mrema, alisema chama chake hakioni kama CUF ina mgogoro na CCM, bali mgogoro uliopo ni kati ya CUF na Serikali ya Tanzania.
Alisema hili linathibitishwa na matumizi ya vyombo vya dola yanayofanywa na serikali zote mbili, ya Zanzibar na Tanzania Bara katika chaguzi mbalimbali zilizokwisha kufanyika.
“Nashauri mazungumzo yawe ya CUF na serikali hizo mbili. Nyie CUF mnataka nini kwa CCM? Nawaambieni CUF, mtaendelea kusanifiwa na kugeuzwa mwanasesere na CCM hadi mshike adabu, kwanza mazungumzo gani haya yamechukua karibu miaka 12 hayapatiwi ufumbuzi,” alisisitiza Mrema.
Msimamo huo wa CUF umekuja siku chache baada ya kutangaza kwamba, mwafaka na CCM umeshindikana. Ilitangaza hivyo baada ya kuona juhudi za kumaliza mazungumzo zikielekea kukwama, licha ya awali kuwapo dalili kuwa makubaliano yangefikiwa Agosti 15, mwaka huu.