Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kishindo cha Zitto kikubwa
Kishindo cha Zitto kikubwa
By Marshy Abdu | Published  08/18/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
Kishindo cha Zitto kikubwa
na Mwandishi Wetu


KISHINDO cha uamuzi wa Bunge kumsimamisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zubeir Zitto (CHADEMA) kwa miezi mitano, bado kinaendelea kusikika kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Ukubwa wa kishindo hicho unatarajia kudhihirika leo jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya mbunge huyo, yaliyoandaliwa kwa pamoja na vyama vya upinzani, vinavyoungwa mkono na wanaharakati wa makundi mbalimbali.

Imefahamika kuwa, kati ya watu watakaoshiriki mapokezi hayo, ni viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani, wanaharakati, wananchi wa kawaida pamoja na wachimbaji wadogo wadogo na wafanyabiashara wa madini ya tanzanite, kutoka eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.

Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu Zitto akumbwe na mkasa huo, ambao sasa umechukua sura ya kitaifa, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, alisema amelazimika kukatisha ziara yake ya kibiashara nchini China na kurejea nyumbani ili kuweza kushiriki katika mapokezi hayo, ambayo yatatoa fursa kwao kuwaeleza wananchi kuhusu mwelekeo wa taifa hili.

Mbowe, ambaye alilieleza gazeti hili kuwa alirejea nchini jana, alisema awali alikuwa amepanga kukaa China hadi Agosti 25, mwaka huu kabla ya kubadilisha ratiba baada ya kupata taarifa hizo za kushtua za Zitto, moja ya vijana aliowakuza kisiasa.

Taarifa zinaonyesha kuwa, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana alikuwa ametoa kibali cha maandamano hayo ambayo yataanzia eneo la Ubungo Maji, majira ya saa 7:00 mchana na kuishia viwanja vya Jangwani, ambako kutafanyika mkutano wa hadhara.

Katika mkutano huo wa hadhara, ambao utahusisha viongozi wote wa upinzani, mbali ya suala hilo la Zitto, mada nyingi zitakazozungumzwa hapo ni kuhusu haja ya kufikiwa kwa haraka kwa muafaka wa kisiasa wa Zanzibar na ile inayohusu sakata ya Benki Kuu (BoT).

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Karatu, Dk. Willibroad Slaa, anatarajia pamoja na mambo mengine kuweka hadharani jinsi hoja yake ya kutaka kuundwa kwa tume ya kuchunguza kashfa za Benki Kuu (BoT), lilivyozungushwa na Spika kiasi cha kusababisha yeye kuiondoa.

Mbali ya viongozi hao wa kisiasa, kundi la wachimbaji wadogo wa madini ya tanzanite, ambalo limetangaza kumuunga mkono Zitto, limekodisha ndege maalumu kutoka Arusha hadi jijini Dar es Salaam kushiriki mapokezi yake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wachimbaji hao walieleza kusikitishwa na msimamo ulioonyeshwa na wabunge wa CCM katika kujadili hoja hiyo, kiasi cha kuonyesha wanachojali ni maslahi yao binafsi na chama chao, badala ya wananchi waliowaweka madarakani.

“Kibaya zaidi ni kwamba, hata wale wabunge ambao majimbo yao yana sehemu zenye migodi ambayo mikataba yake ina utata, waliamua kuwasaliti wapigakura wao kwa kuunga mkono mikataba mibovu inayolalamikiwa kila siku.

“Hata Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani, alikiri hadharani juu ya ubovu wa mikataba hii, kiasi cha kuahidi kuipitia upya, sasa hawa wabunge wa CCM wanamsaliti hata rais na mwenyekiti wao?” alihoji mchimbaji Augustine Mcharo.

Mchimbaji mwingine, Abubakar Mohamed, alionyesha mshangao mkubwa kwa wabunge kushindwa kumbana waziri aeleze utaratibu na watu waliotumika kufanyia mapitio suala la mikataba ya madini, ambayo Watanzania walidhani haijakamilika kumbe tayari kazi imeisha.

“Kibaya zaidi, kazi hiyo imekamilika na wahusika kukaa kimya hadi hoja ilipotolewa na Zitto ndipo waseme. Huu ni ubabaishaji unaofanywa na watendaji serikalini kwa maslahi yao,” alisema Mohamed.

Wanaharakati wengine wa sekta za madini, mazingira, jinsia, mifugo na haki za binadamu, wametoa wito kwa Spika Samwel Sitta kufuta maamuzi ya kumsimamisha ubunge Zitto katika kipindi cha siku 30, vinginevyo wataendesha kampeni nchi nzima kushawishi wananchi kuondoa imani kwa Bunge.

Akisoma tamko la pamoja la mitandao hiyo kwa waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Wafanyakazi Migodini, Amani Mustafa, alisema licha ya kumtaka Spika kufuta uamuzi huo, pia arejeshewe mshahara wake wa ubunge, na serikali pia iache kutumia vitisho dhidi ya wabunge wanaotimiza haki zao za kikatiba kuhoji utendaji wake.

Aidha, mitandao hiyo pia imechanga sh 500,000 kuchangia mfuko wa kumsaidia Zitto ulioanzishwa na wabunge wa kambi ya upinzani na kutoa wito kwa wananchi wote wapenda maendeleo kujitokeza kuuchangia mfuko huo.

“Kwa Bunge kuzuia kuundwa kwa tume kumchunguza Karamagi, ni sawa na kuficha ukweli kwa kutumia mabavu na kuweka kiwingu kizito kwenye taratibu zilizouzunguka mkataba uliosainiwa na waziri huyo jijini London,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Mashirika ya wanaharakati yaliyohudhuria na kutoa tamko hilo la pamoja ni, Shirika la Mtandao wa Jinsia Mkoa wa Arusha na Manyara (IGN), Shirika la Maendeleo ya Wafanyakazi Migodini (Haki Madini), Muungano wa vyama vya wafugaji Tanzania (TAFGO), Arusha NGOs Network, LHRC Arusha na Arusha Caucus for chirdren Rights.

Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wanaharakati ambaye ni mchimbaji wa madini ya tanzanite katika mji wa Mirerani, Mushi Ngao, alisema wachimbaji wote wa madini nchini wamesikitishwa na kitendo cha Bunge kumdhibiti mbunge aliyekuwa anataka kutetea maslahi ya taifa.

Alisema hali ya usiri wa mikataba ya madini nchini ndiyo inasababisha kuongeza umasikini kwa wananchi wa Tanzania na pia kuwapa kiburi wawekezaji wa sekta ya madini katika migodi mbalimbali nchini, na kufikia kuwanyanyasa hata wachimbaji wadogo.

Wakati huohuo, wanaharakati wa haki za binadamu wa mitandao ya jinsia na maendeleo Tanzania (FemAct), wamemtaka Waziri Karamagi kujiuzulu kwa kuwa alikiuka maagizo ya rais ya kwenda kusaini mkataba nje ya nchi, wakati kuna mikataba mingine bado haijapitiwa.

Wanaharakati hao walifanya maandamano jana katika viwanja vya TGNP, Dar es Salaam yenye lengo la kupinga adhabu aliyopewa Zitto.

Katika maandamano hayo, wanaharakati hao walikuwa wamebeba mbabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali, ambayo miongoni yalikuwa wameandikwa; ‘Samwel Sitta ajiuzulu hajatenda haki’; ‘Ahadi ya rais ya madini iko wapi?’; ‘Michezo ya kuigiza bungeni mwisho.’

Mabango mengine yalikuwa na ujumbe unaosomeka; ‘Wabunge wekeni maslahi ya wananchi mbele’; ‘Sitta acha ubabe bungeni’; ‘Mawaziri wasiwe wabunge’; ‘Hukumu ya Zitto iangaliwe upya kwa makini’; ‘Mfumo wa uchumi umefanya wananchi mataahira na iwe isiwe, ukweli utakuwa kweli daima.’

Aidha, wanaharakati hao walimtaka Rais Kikwete kuvunja Bunge, kwa kuwa wabunge wameshindwa kutetea maslahi ya wananchi na kutanguliza maslahi yao mbele.

Mwanaharakati mwingine, Mohamed Tibanyendela, alisema Bunge limefikia hatua mbaya ya kuikanyaga katiba na kuitupa pembeni.

Alisema Ibara ya 18 inazungumzia jinsi ya kutoa haki na uhuru wa kujieleza, ambayo wanaharakati kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiipigia kelele bila mafanikio.

Aidha, mwanaharakati, Beatrice Ezekiel, alipendekeza kuwepo na sheria za uwakilishi bungeni usiopungua kipindi cha miaka 10, kwani kukaa muda mrefu wabunge hujisahau na kujiona kama wako nyumbani kwao.

Kwa upande wake, Elizabeth Masanja, alisema umefika wakati kwa Watanzania kuamka na kutetea haki zao badala ya kubaki kunung’unika kwa kutingisha vichwa wanapoona habari mbaya za wawakilishi wao zinazoandikwa kwenye vyombo vya habari.

Wanaharakati hao wamemtaja Zitto kuwa ni jabali linalofaa kuigwa, kwani kama si yeye, wasingejua mikataba hiyo na kuponda kuwa, kuna wabunge waliokaa zaidi ya miaka 20 bungeni hawajawahi kufichua siri nzito kama hiyo.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, wabunge kadhaa wa CCM wametoa dukuduku lao kuhusu uamuzi wa Jumanne wiki hii wa kumsimamisha ubunge Zitto.

Habari kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM kilichokutana kuanzia juzi alasiri mjini Dodoma zinaeleza kuwa, mabishano makali yalitokea wakati wa mkutano huo kuhusu uamuzi huo.

Kwa mujibu wa habari hizo, baadhi ya wabunge walifikia hatua ya kutaka Waziri Karamagi awajibike kutokana na kuhusishwa katika tukio lililosababisha Zitto asimamishwe.

Aidha, habari nyingine zinaeleza kuwa, mmoja wa vigogo alifikia hatua ya kutishia kujiuzulu wadhifa wake, iwapo angeendelea kusakamwa na wabunge wenzake kuwa chanzo cha zahama hiyo, ambayo sasa inaonekana kumpa Zitto umaarufu mkubwa.

Katika hatua nyingine, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana lililazimika kutoa taarifa ya kufafanua kuhusu kusimamishwa kwa mbunge huyo.

Taaarifa hiyo kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Bunge, Damian Foka, imewatahadharisha watu wote wanaojiita wanaharakati wa haki za binadamu kuwa makini na matamshi yao.

Foka, alisema kutoa madai ya kupotosha umma kuhusu uamuzi huo wa Bunge wa kumsimamisha Zitto kufanya kazi za Bunge ni kukiuka Sheria ya Madaraka, Kinga na Haki za Bunge ya mwaka 1988, hivyo Bunge halitasita kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria hiyo.

Alisema kanuni za Bunge zinaweka utaratibu wa kufuatwa kwa ajili ya uendeshaji bora wa shughuli za Bunge, na kwamba kanuni hizo zilizingatiwa na kufuatwa kikamilifu katika kushughulikia suala la uongo uliosemwa bungeni na Zitto.

“Mheshimiwa Kabwe Zitto alipewa nafasi ya kutosha kuthibitisha tuhuma kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Karamagi alisema uongo bungeni, lakini Mheshimiwa Kabwe akashindwa kuthibitisha.

“Katika kujadili hoja ya kumsimamisha kazi Mheshimiwa Kabwe, Bunge liliafiki kwa kauli moja kuwa, uongo uliosemwa na mbunge huyo ulikuwa ni mkubwa kiasi cha kuathiri heshima ya Bunge,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hii imeandaliwa na Tamali Vullu, Mosses Kissa, Ramadhani Siwayombe, Lucy Ngowi, Nasra Abdallah na Martin Malera.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Marc)
    Rating
    Poa sana
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.