SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kukitaka Chama cha Wanachi (CUF) kutosusia mazungumzo ya kusaka muafaka kati yake na Chama Cha Mapinduzi (CCM) juu ya hali ya kisiasa kisiwani Zanzibar, chama hicho kimesema kitaweka hadharani ukweli wa mambo keshokutwa Jumamosi.
Akizungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho Buguruni, Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), Wilfred Lwakatare, alisema siku hiyo chama hicho kitaweka wazi msimamo wake kuhusu masuala yote kuhusu Zanzibar.
“Tumekubaliana kuwa siku ya Jumamosi CUF itatoa kile kilichokuwa kikijadiliwa kwa muda wote huo, na hatua za kuchukua baada ya Agosti 15 ambayo tulikuwa tumekubaliana kupita bila makubaliano,” alisema Lwakatare.
Alisema hatua ya Rais Jakaya Kikwete aliyochukua kwa ajili ya kunusuru mazungumzo hayo imeonyesha ushapavu na nia ya mshikamano alionao juu ya mazungumzo hayo ambayo lengo lake ni kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la Zanzibar.
“Sisi tunaiunga mkono nia ya Rais Kikwete ya kunusuru mazungumzo haya na kuipongeza kwa nguvu zetu kwa vile imeonyesha wazi kwamba, yeye mwenyewe ameguswa na suala hili ambalo ni muhimu kwa pande zote mbili,” alisema Lwakatare.
Alisema uamuzi wake wa juzi, Rais Kikwete anaweza akawa ameondoa wingu zito lililokuwa limetanda katika mazungumzo hayo ambayo ilifikiwa wakati yakaonekana dhahiri kudorora na kupoteza mwelekeo.
“CUF tunaamini kwamba hatua hii imetokana na msukumo alioutoa Mwenyekiti wetu Profesa Ibrahim Lipumba Agosti 7 mwaka huu kwamba chama chetu kinaweza kujitoa baada ya Agosti 15 ambayo ndiyo siku ya makubaliano iliyokuwa imefikiwa na pande zote mbili,” alisema Lwakatare.
Aidha, alisema katika taarifa ya Rais Kikwete imeonyesha mambo yote yaliyokuwa yakizungumzwa na pande zote, hivyo CUF nayo sasa ina wajibu wa kueleza ukweli wa mambo kwa wananchama wake ambao wamekuwa wakisubiri kwa hamu kubwa makubaliano hayo.
Alisema suala la kuendelea au kutoendelea na mazungumzo hayo litajulikana Jumamosi baada ya maamuzi yatakayokuwa yamefikiwa katika kongamano hilo.
Alisema katika kongamano hilo, CUF imealiaka wabunge wote wa vyama vya upinzani, viongozi wa dini, wasomi maarufu, taasisi zisizo kuwa za kiserikali (NGOs na wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho.
Wakati huo huo, Mwandishi Wetu kutoka Zanzibar anaripoti kuwa, tamko la Rais Kikwete kuitaka CUF iendelee kubaki katika mazungumzo ya muafaka na CCM limepokewa kwa kihoro na wananchi mbalimbali wa huko.
Hayo yamebainika jana baada ya viongozi wa vyama vya siasa na wananchi waliokuwa wakihojiwa katika mitaa mbali mbali Zanzibar, ikiwa ni siku moja tangu kutolewa kwa tamko hilo.
Viongozi wa Chama cha TADEA, UPDP, NCCR - Mageuzi na CUF walisisitiza haja ya kuwapo kwa ukomo katika mazungumzo hayo, ili kujenga imani kwa wananchi kwamba, kweli mazungumzo hayo yana nia thabiti.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa UPDP, Haji Othman, alisema kwamba, kuwepo kwa kikomo katika mazungumzo ndiko kutakakosaidia kurejesha imani kwa wananchi.
Alisema kwamba wananchi wengi hivi sasa Zanzibar hawana imani na mazungumzo hayo, kwa vile wanahisi CCM inatumia mtaji wa kuvuta muda kama ilivyotokea katika miafaka miwili ya awali.
“Mazungumzo haya yasiwe kama ya Mashariki ya Kati, lazima kuwepo na muda wa kikomo, vinginevyo wananchi watapoteza imani na gharama yake itakuwa kubwa kama yatavurugika,” alisema.
Othman alisema hadi sasa chama chake kina imani na Rais Kikwete kwamba, ana nia thabiti ya kuondoa tatizo, lakini tatizo lipo kwa CCM Zanzibar na serikali yake kutokuwa tayari kufanya kazi pamoja na wapinzani.
Alisema kwamba kama nia njema ipo mgogoro wa kisiasa ungekuwa umekwisha kumalizika Zanzibar tangu mwaka 1999, ulioanzishwa muafaka na Jumuiya ya Madola, lakini ubinfsi wa watu ndio uliosababisha Zanzibar ifikie ilipo sasa.
Katibu Mkuu wa Chama cha TADEA, Juma Ali Khatib, alisema kwamba tamko la Rais Kikwete linaleta faraja kwa wananchi Zanzibar, lakini muda wa utekelezaji unapaswa kuzingatiwa ili kujenga imani kwa viongozi wa vyama na wananchi wote.
Alisema kwamba ili kuboresha mazungumzo hayo, vyama vyote vya siasa nchini vishirikishwe, ili kuangalia ni upande gani umekuwa ukichechemea katika kufikia muafaka wa kudumu.
Alisema kwamba pamoja na tamko zuri la Rais Kikwete, lakini alipaswa kueleza mambo muhimu ambayo tayari wamefikia makubaliano, badala ya kueleza muhtasari wa ajenda kama ilivyojitokeza katika hotuba yake.
Alisema kwamba mfumo wa utawala hivi sasa Zanzibar umeacha ufa mkubwa katika umoja wa kitaifa kwa vile hakuna uwiano katika nafasi ya uongozi kati ya wananchi wa Pemba na Unguja.
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma na Haki za Binaadamu wa CUF, Salim Bimani, alisema, chama chake kimepokea tamko hilo na kinaendelea kulifanyia kazi kabla ya kutoa taarifa maalumu.
Bimani alisema kwamba lengo la CUF ni kuona mgogoro wa Zanzibar unapatiwa ufumbuzi kwa njia ya amani na utulivu na ndiyo maana CUF ikaingia katika mazungumzo hayo licha ya muafaka wa 1999 na 2001 kutotekelezwa.
“Sisi ni watu wazima, tamko hilo tumelipokea. Litajadiliwa na chama kitatoa msimamo wake, lakini hatutakubali kuchezewa michezo ya kisiasa kwa masilahi ya demokrasia nchini,” alisema Bimani.
Wakati huohuo, wananchi wengi wa Zanzibar jana walionekana wakifuatilia tamko la Rais Kikwete wakiwa wamegawanyika makundi mawili, huku baadhi wakisema mazungumzo hayo hayana faida tena na wengine kutaka CUF iendelee nayo.
Baadhi ya wachuuzi katika Soko Kuu la Darajani walionekana kuacha shughuli zao na kuingia katika mabishano juu ya tamko la Rais Kikwete kuwataka CUF waendelee na mazungumzo hayo.
Sehemu kubwa ya maduka jana yalionekana yakiwa yamefungwa na baadhi ya askari walionekana wakifanya doria katika maeneo ya Jang’ombe, Mlandege na Mji Mkongwe ambapo kuna taarifa za watu kadhaa kukamatwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakari Khatib Shaaban, alisema hakuna operesheni yoyote maalumu iliyoanzishwa, lakini atafuatilia maeneo yanayodaiwa kukamatwa watu waliokuwa katika mazungumzo yao ya kawaida na wengine wakinywa kahawa.