UAMUZI wa Bunge kumsimamisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zubeir Zitto, kwa miezi mitano, umepokewa kwa shingo upande, katika hali ya mshangao, masikitiko na kejeli na wananchi wa kada mbalimbali.
Habari ambazo gazeti hili limezikusanya kutoka katika vyanzo mbalimbali zinaonyesha kuwa, baadhi ya watu wanauona uamuzi huo kuwa umechukuliwa kwa lengo la wabunge wa CCM kuilinda serikali yao kwa gharama zozote zile, pasipo kuangalia kuwa imekosea au la.
Watanzania kadhaa waliowasiliana na gazeti hili ama kwa njia ya ujumbe wa maandishi kupitia simu za mkononi, mtandao wa intaneti, simu na kwa njia ya mazungumzo ya ana kwa ana, wameielezea hatua hiyo ya Bunge kuwa isiyopaswa kuchukuliwa.
Wakati wananchi wakiendelea kuijadili hoja hiyo ya Zitto, wabunge wenzake wa upinzani, jana walifikia hatua ya kumchangia mwenzao huyo kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano (sh 1,500,000) kila mwezi, lengo likiwa ni kumfidia pengo la mapato yake lililotokana na kulipwa kwake nusu mshahara, kipindi chote cha miezi mitano alichosimamishwa.
Uamuzi huo wa wabunge wa upinzani, ulibainishwa jana na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohammed (CUF) alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu.
Zitto mwenyewe, aliieleza Tanzania Daima jana kuwa, alikuwa ameupokea uamuzi huo kwa moyo mweupe akiamini kuwa alikuwa ametimiza wajibu wake ipasavyo kama mbunge.
“Sijuti. Nimeupokea uamuzi huu kwa moyo mweupe kwa kuwa nimetimiza wajibu wangu. Sisi wabunge tunaapa kuwa watiifu kwa Jamhuri ya Muungano na ni jukumu letu kulinda rasilimali za taifa.
“Nasema nimetimiza wajibu wangu kwa sababu kama si mimi, basi Watanzania ninaowatumikia wasingejua kuwa kuna mkataba mpya wa madini ulisainiwa nje ya nchi. Umesainiwa Februari, kama kulikuwa hakuna mambo mengine ya siri kwa nini haukutangazwa hadi mimi niliposema bungeni?” alisema Zitto kwa kujiamini.
Mbunge huyo alisema, alikuwa akitarajia kusafiri kwenda Dar es Salaam keshokutwa Jumamosi na siku hiyo anatarajia kufanya mkutano wa hadhara kabla ya kusafiri kwenda Kigoma kuwaeleza wapiga kura wake hali halisi ya utendaji bungeni.
Taarifa kutoka Makao Makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), zinaeleza kuwa chama hicho kimeandaa mapokezi makubwa kumpokea mbunge wake huyo kiliyemwelezea kuwa shujaa wa taifa, wakati atakapowasili Dar es Salaam.
Taarifa ya Chadema kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Erasto Tumbo, ilieleza chama hicho kinaamini kuwa mbunge wake hakutendewa haki.
Chama hicho kimeelezea kusikitishwa na uamuzi wa wabunge wa CCM kuamua kuitetea serikali na kusahau wajibu wao wa kuweka mbele masilahi ya umma.
Kwa upande wake, Chama cha Wananchi (CUF), kimesema hatua zilizochukuliwa na Bunge dhidi ya Zitto zinalenga kuidhoofisha kambi ya upinzani.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Willfred Lwakatare, alisema sasa umefika wakati kwa vyama vya upinzani kujifunga mkanda kutokana na kukandamizwa.
“Kitendo cha kufungiwa Zitto ni fundisho kubwa kwa kambi ya upinzani kujiandaa kukabiliana na sera za Chama Cha Mapinduzi,” alisema Lwakatare alipozungumza na wanahabari jana.
Alisema tukio hilo pia ni fundisho kwa wananchi ambao wamekuwa na tabia ya kuchagua wabunge wengi kutoka chama kimoja, ambacho kinachukua uamuzi kujiamulia mambo, hata kama hayana masilahi ya kitaifa.
Wakili wa kujitegemea Sambwe Shitambala yeye alisema hata kama Zitto angeshindwa kwa hoja, bado Bunge lisingepaswa kumuita muongo na wala adhabu hiyo isingechukuliwa.
Akitoa mfano, Shitambala alisema, katika mfumo wa mahakama, mabishano ya mawakili kwa hoja umalizwa kwa maamuzi na si kwa kumtuhumu wakili aliyeshindwa kuwa muongo.
“Kwa uamuzi huu wa Bunge, basi mawakili wanaoshindwa wangekuwa wakionekana kuwa ni waongo kila wanaposhindwa kesi.
Alichofanya Zitto kilikuwa ni kuwasilisha hoja na Karamagi akajibu, kwa hiyo kulikuwa hakuna haja ya kuangalia nani mwongo, nani mkweli, bali hoja zingechambuliwa na mshindi kupatikana kwa ajili ya ama kuunda kamati teule au la na si kufikia hatua ya kumuita mmoja muongo na kumuadhibu,” alisema Shitambala.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT), Tundu Lissu, alisema wameshtushwa kwa uamuzi huo na kwamba utaratibu uliotumika kumwadhibu Zitto ni batili.
Alisema adhabu hiyo ni kubwa kinyume na kanuni za Bunge na kusema kuwa, alipaswa kusimamishwa kwa muda wa vikao vitano( yaani siku tano za vikao vya Bunge) na si miezi mitano kama alivyoadhibiwa juzi.
Pia alisema mbunge ambaye anadaiwa kusema uongo, anatakiwa athibitishe ama afute kauli yake (Kanuni ya 50 ya Bunge), kinyume na maagizo ya kanuni hii, Zitto hakupewa fursa ya kuthibitisha kauli yake, wala kupewa fursa ya kufuta kauli yake.
Alisema Bunge limeonyesha udhaifu wa uwajibikaji kama chombo cha umma katika kusimamia shughuli za serikali japokuwa kikatiba lina haki na wajibu wa kusimamia na kuishauri serikali.
“Katika kufanya hivyo Bunge lina uwezo wa kuwawajibisha watendaji wa serikali, kwa mfano kumshitaki rais ama makamu wake; ibara ya 46 na 50 (2), kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu; ibara ya 53A, pamoja na kuunda kamati mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake.
“Kwa kuangalia mazingira ya suala la Zitto, swali la msingi ni kuwa, je, Bunge hili litaisimamiaje serikali endapo mbunge anayeleta hoja anaadhibiwa badala ya hoja yake kufanyiwa kazi? Kwa utaratibu huu, wabunge wataogopa kuleta hoja bungeni na hivyo watashindwa kuisimamia serikali kama ambavyo katiba inaagiza,” alisema Lissu.
Kwa mujibu wa Lissu, maadili katika uendeshaji wa vikao vya Bunge yamekuwa ya utata, kwani vimekuwa vikiendeshwa kiitikadi na si kwa masilahi ya wananchi.
Alisema mfano wabunge wote wa CCM na wabunge wa upinzani wana hoja moja, ikitokea mbunge wa kambi moja ametoa hoja, kwa vyovyote vile hoja yake lazima ipingwe hata pasipo kuzingatia masilahi ya umma.
Lissu alisema kumekuwepo na tabia ambayo imejitokeza ya badala ya Bunge kujadili masuala ya masilahi ya umma, wamekuwa wakijadili kwa kuunga mkono ama kupingwa kwa hoja mbalimbali kwa misingi ya kiitikadi za vyama.
Aidha, baadhi ya wanasheria wa serikali na wa kujitegemea wamelaani uamuzi wa Bunge wa kumsimamisha Mbunge Zitto.
Mwanasheria Augustus Fungo, kwa upande wake alisema kama aliyoyasema Zitto ni tatizo, alistahili kuelezwa mashitaka yake, kujibu na hatimaye kuadhibiwa iwapo ataonekana ana kosa.
“Kumuadhibu Zitto kwa hoja tu ya mbunge aliyetaka aadhibiwe bila kuwa na kikao chochote cha kutoa maamuzi hayo kisheria ni kukiuka kanuni za msingi za utoaji adhabu kwamba mtu asihukumiwe bila kupewa nafasi ya kujitetea.
“Spika Samwel Sitta analijua na kalipuuzia na kutengeneza kosa jipya linaloitwa ‘kutoa hoja binafsi bungeni’ ikipingwa mtoaji ana kosa anastahili adhabu,” alisema Mwanasheria Augustus Fungo.
Wanasheria wengine wa serikali ambao walikataa kutaja majina yao walielezwa kutofurahishwa na uamuzi huo na kuhoji sakata la Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima na mfanyabiashara Reginald Mengi, ambalo lilikuwa halina masilahi ya taifa liliundiwa kamati ya Bunge na kugharimu mamilioni ya fedha za walipakodi, lakini mbunge huyo hakuchukuliwa hatua zozote za Bunge hata baada ya kuthibitika kuwa alilidanganya Bunge.
Taarifa hii imeandaliwa na Martin Malera, Tamali Vullu, Kulwa Karedia, Happiness Katabazi, Nuru Yanga na Deodatus Mkuchu.