KAMPUNI mbili kongwe zinazojishughulisha na ununuzi wa pamba, Nyanza Cooperative Union (1984) Ltd ya mkoani Mwanza na Mara Lint Industries Ltd ya Mkoa wa Mara, zimeshindwa kuhimili uashindani wa bei ya pamba wilayani Magu mwaka huu na kushindwa kununua hata kilo moja, imefahamika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mbele ya baraza la madiwani wa Halmshauri ya Wilaya ya Magu jana, kampuni hizo ni miongoni mwa kampuni 17 zilizoomba na kukubaliwa kununua zao hilo msimu huu.
Akiwasilisha taarifa ya ununuzi wa zao hilo toka msimu wa ununuzi ulipofunguliwa Juni 25 mwaka huu, Mkaguzi wa Pamba wa Wilaya, Emmanuel Kileo, alisema kuwa kampuni hizo zimeshindwa kuhimili soko la zao hilo kutokana na bei kupanda kutokana na ushindani mkubwa uliojitokeza.
“Bei ya pamba ilianza ikiwa sh 380 kwa kila mwanzo wa msimu, lakini ikapanda kwa kasi ya ajabu na kufikia sh 530 hali ambayo imeyaondoa baadhi ya makampuni kwenye ununuzi na kuwa watazamaji,” alisema Kileo na kuongeza kuwa hali hiyo imetokana na kampuni hizo kujiwekea kiwango maalumu cha bei.
Alisema kuwa jumla ya kilo 11, 299,970 za zao hilo tayari zimenunuliwa na kampuni 15 zilizosalia na kilo 9,605,232 zimewasilishwa viwandani na kiasi kilichobakia bado kipo kwenye vituo vya ununuzi.
“Kampuni ya Olam (T) Ltd, ndiyo inayoongoza kununua pamba wilayani Magu ikiwa tayari imenunua kilo 2,109,550 ikifuatiwa na Mwatex (2001) Ltd iliyonunua kilo 689,000 huku kampuni nyingine zikiwa zimenunua kiasi cha kutosha na ununuzi unaendelea,” alisema.
Hivi karibuni kulikuwa na juhudi za kampuni zinazonunua zao hilo Kanda ya ziwa kudhibiti bei ili kuziwezesha kununua kwa bei ya chini lakini juhudi hizo ziligonga mwamba.