Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wabunge wa CCM wamsulubu Zitto
Wabunge wa CCM wamsulubu Zitto
By Habari Tanzania | Published  08/15/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Martin Malera, Dodoma


HOJA binafsi iliyowasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ya kuliomba Bunge liunde kamati teule kuchunguza hatua ya Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kusaini mkataba wa madini nje ya nchi, jana iligeuzwa na wabunge wa CCM na kuwa mwiba mkali kwa mbunge huyo kijana aliyesimamishwa Bunge hadi Januari mwakani.

Dalili za wabunge hao wa CCM ‘kumgeuzia kibao’ Zitto zilianza kuonekana mapema jana na taarifa kuwa hali ingekuwa hivyo zilianza kuvuja tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mpasuko miongoni mwa wabunge kiitikadi ulionekana dhahiri wakati Zitto akitoa hoja yake, Karamagi aliposimama kujibu na hata wabunge walipoanza kuchangia hoja hiyo kabla ya jana jioni kuhitimishwa kwa wabunge wa CCM kujipanga kwa ajili ya kutaka kutumia kanuni za Bunge, ambazo Spika wa Bunge Samwel Sitta alipata kuzieleza kuwa zilizopitwa na wakati kumwadhibu mbunge huyo kwa kumsimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge kwa kosa la kusema uongo.

Wabunge wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliochangia hoja hiyo, waliipinga hoja ya Zitto wakati huku wale wa vyama vya upinzani wakimuunga mkono mwenzao kuhusu haja ya kuundwa kwa kamati teule.

Katika hoja yake, Zitto alihoji sababu za Karamagi kusaini mkataba mpya wa madini wa mgodi huo London, Uingereza na kwa nini mkataba huo ulisainiwa wakati serikali ikiendelea kudurusu mikataba kama ilivyoagizwa na Rais Jakaya Kikwete.

Hoja ya Zitto kusimamishwa ubunge ilijengwa na Mbunge wa Nchinga, Mudhihir Mudhihir na Bunge likalazimika kuongeza muda wake ili kutekeleza adhabu hiyo ambayo Zitto mwenyewe alipoambia ajitetee alisema alikuwa tayari kwa lolote.

Awali Zitto wakati akiwasilisha hoja yake hiyo alitaka kujua sababu za kuondolewa kwa kipengele katika sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 1973 kuhusiana na asilimia 15 bila ya kibali cha Bunge.

“Suala ambalo linanipelekea kuomba kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kuchunguza mkataba huo mpya ni kuhusu uharaka uliopelekea Waziri wa Nishati na Madini kusaini mkataba huu,” alihoji Zitto.

Hoja hiyo ilizusha mpasuko ambao ulisababisha mjadala kutawaliwa na jazba, huku wabunge wa CCM wakiwapinga wale wa upinzani kila walipokuwa wakizungumza na kumshangilia kwa nguvu Karamagi kabla na baada ya kumaliza kuwasilisha msimamo wa serikali.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Karamagi alisema tuhuma zilizotolewa na Zitto dhidi yake ni uzushi na zimejengwa katika mazingira yenye malengo makuu mawili.

Alitaja malengo hayo kuwa, moja ni kuchonganisha Bunge na Serikali na pili kuwapotosha wananchi juu ya sheria zinazotungwa na Bunge kwa nia ya kujitafutia umaarufu usiokuwa na msingi.

“Mtoa hoja Zitto Kabwe amedai suala analolizungumzia eti ni la kitaifa na halina hata chembe chembe za itikadi za kivyama. Pamoja na kuwa hoja alizozitoa hazina ushahidi wowote, tayari hoja hizo zimekwisha dakwa na kubebewa bango na Mwenyekiti wa chama chake cha CHADEMA na wamezigeuza kuwa propaganda ya kisiasa kupitia vyombo vya habari. Labda angalizo analolitoa Zitto analilenga kwa chama chake mwenyewe,” alisema Karamagi huku wabunge wa CCM wakishangilia kwa kupiga makofi.

Karamagi ambaye muda mwingi alitumia kuchambua udhaifu wa Zitto na Chama chake cha CHADEMA katika kuwasilisha taarifa hiyo, alizidi kusema: “Kuna msemo wa Kiingereza usemao: No research, no right to speak. (Bila utafiti huna haki ya kuzungumza), hivyo vile vile chama makini kinahitaji kufanya utafiti kabla ya kujihusisha na mambo ya kuzua.”

Alisema hoja ya Zitto imeonyesha mapungufu makubwa ya tafsiri ya sheria alizozinukuu na vifungu alivyovilenga ili kuthibitisha kuwa Serikali imelidanganya Bunge.

Huku akisindikizwa na makofi yaliyomfanya akatishe hoja yake mara kwa mara na kurejea kusoma upya baadhi ya vipengele kwenye hoja yake, Karamagi alipinga hoja ya Zitto kwamba yeye waziri alikuwa amelidanganya Bunge wakati yeye mwenyewe (Zitto) ndiye aliyelidanganya Bunge na umma kwa ujumla.

“Mheshimiwa Spika, mtoa hoja anaomba Bunge lako tukufu kuunda kamati teule ya Bunge ili kamati imfanyie kazi ya kuhalalisha mambo ya kuzua au kumsaidia kumfafanulia sheria ambazo yeye mwenyewe kashindwa kuzielewa. Hii si kazi ambayo Bunge hili linaweza kutumia fedha za walipa kodi kuifanya. Tabia ya namna hii ikiruhusiwa kuendelea inaweza kulipunguzia Bunge lako tukufu heshima na hadhi,” Karamagi alisema.

Waziri Karamagi alisema tuhuma za Zitto dhidi yake ambazo zimedakwa na vyombo vya habari, zimemuathiri binafsi na kumchafulia jina bila sababu za msingi, kwa kutoa taarifa za uzushi, tena uzushi wa hatari kwake.

“Kwa vielelezo na maelezo ya Serikali niliyoyatoa sasa, naomba kupitia kwako Mheshimiwa Spika kuliomba Bunge lako tukufu vilevile liangalie vielelezo alivyovitoa mtoa hoja (Zitto) kama vipo ili Bunge liweze kupima na kuamua ni nani mwongo, ni nani aliyelidanganya Bunge, mimi au Mheshimiwa Kabwe Zubeir Zitto,” alisema Karamagi.

Alisema moja ya hoja ya Zitto ni kulalamikia kuondolewa kwa kipengele katika sheria ya mapato ya mwaka 1973 kuhusiana na nyongeza ya asilimia 15 kwenye mtaji wa uwekezaji ambao haujarejeshwa kwa kila mwaka na kwamba Zitto anadai kuondolewa kwa kipengele hiki kulifanyika bila kupata kibali cha Bunge.

Alisema katika kujaribu kuthibitisha hoja yake, Zitto amenukuu kumbukumbu za Bunge ambazo zinaonyesha marekebisho yaliyofanyika kwenye Sheria ya Fedha ya mwaka 2001 kwa kutaja marekebisho ya sheria ya mwaka 1998 ya madini, kifungu cha 87 ambapo kifungu kidogo cha (3) cha fungu la 87 la sheria ya madini liliongezwa.

Alisema kipengele kinachozungumziwa hakiko chini ya sheria ya madini ya mwaka 1998 bali kipo chini ya sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 1973.

Hata hivyo, alisema ukweli kuhusu suala hilo ni kwamba kipengele cha nyongeza ya asilimia 15 kwenye mtaji wa uwekezaji ambao haujarejeshwa kiliondolewa na Bunge kupitia Sheria ya Fedha ya 2001.

“Kama Zitto angesoma kwa uangalifu Finance Act No 14 of 2001 aliyoinukuu, angebaini kuwa marekebisho ya kipengele hiki yalifanyika,” alisema.

Alisema hoja ya pili, anahoji kusainiwa kwa mkataba mpya wa madini wa mgodi wa Buzwagi kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick na uhalali wa mkataba huo kusainiwa mjini London, Uingereza na pia anahoji kwa nini mkataba huo umesainiwa wakati Serikali bado inadurusu mikataba ya madini kutokana na maagizo ya Rais Jakaya Kikwete.

Akijibu hoja hiyo, Karamagi alisema licha ya kusainiwa nje ya nchi, mkataba huo uliandaliwa nchini na kupitia taratibu zote zinazopaswa kufuatwa, ikiwa ni pamoja na kuidhinishwa na Kamati ya Ushauri ya Madini na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alisema kwa kuwa maandalizi ya kusaini mkataba huo yalikamilika akiwa katika ziara ndefu ya nchi za nje, hakuona busara ya huhatarisha uwekezaji wa mradi huo, jambo ambalo lingeliathiri taifa na faida kubwa iliyotarajiwa kutoka katika mgodi huo.

Alitaja faida hizo kuwa ni pamoja na mrabaha na kodi zinazotarajiwa kufikia kiasi cha dola za Marekani milioni 1988.9 kodi ya Paye, dola milioni 50.3, ujenzi wa laini ya umeme wa matumizi ya umeme wa dola milioni 30, ajira pamoja na ujenzi wa huduma za jamii katika eneo linalozunguka mgodi huo.

Kuhusu mahala mkataba huo uliposainiwa, Waziri Karamagi alisema: “Format ya mkataba wa Buzwagi hauna kipengele anachokiuliza Kabwe. Hiki si kitu cha ajabu kwa mikatba ya siku hizi ambapo mkataba unaweza kusainiwa na pande zaidi ya mbili zikiwa nchi tofauti.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Nsalilwe)
    Rating
    Sheria za bunge inabidi kuangaliwa upya. Kabwe si mwajiliwa wa bunge amechaguliwa na wananchi na yupo pale kuwakilisha wananchi, iweje watu wachache wanaojiita wabunge wamuadhibu? Anae faa kumwadhibu ni wananchi na sio wabunge. Hii sheria iangaliwe upya. Kwa umri wa Kabwe CCM wanampe umaarufu mkubwa sana, wangoje mengi hapo baadae, Kabwe akipata wengine ndani ya bunge mambo yatabadilika.
    Nsalilwe

     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.