ONGEZEKO la kodi katika bidhaa za mafuta si tu limeleta athari katika usafirishaji wa abiria kama ambavyo imethibitika katika jamii, bali pia limesababisha kupanda kwa gharama za mazao yanayouzwa katika masoko katika mikoa mbali mbali nchini.
Hayo yalisemwa bungeni jana na Msemaji Mkuu wa kambi ya Upinzani, Wizara ya Fedha, Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF), wakati akitoa maoni ya kambi hiyo kuhusu muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2007 pamoja na marekebisho yake.
Hotuba hiyo iliyosomwa kwa niaba yake na Grace Kiwelu (Viti Maalumu-CHADEMA), alisema kuondoa ongezeko la ushuru katika mafuta ya taa na kuliweka katika dizeli na petroli ni sawa na kiini macho au mchezo wa kuigiza, ikilenga kuwarubuni wananchi kuwa Serikali haijaongeza bei ya mafuta ya taa.
Alisema kwa sasa, matokeo haya si nadharia tena, kwani yamekwisha kuonekana, maana bei za mafuta zimepanda sana na kuleta shida kubwa kwa wananchi wa kawaida.
“Kilio cha kupanda bei ya mafuta kilikuwa kikubwa juzi katika mabango ya wafanyakazi walioandamana jijini Dar es Salaam. Kwa vyovote vile mabango kama hayo yataonekana katika maandamano yatakayofanyika huko Mwanza Jumamosi ijayo.
“Kambi ya upinzani inataka Serikali iwaeleze Watanzania kuwa shida hizi zitaisha lini? Je, marekebisho ya Sheria ya EWURA na ile ya Petroli ambayo ni sehemu ya muswada huu yatashusha bei zilizopanda?” alihoji Kiwelu.
Akitolea mfano wa kupanda kwa bei ya bidhaa, Kiwelu alisema bei ya mfuko wa simenti imepanda kutoka sh 10,500 hadi sh 14,000 kwa Dar es Salaam, Bukoba sh 14,000 hadi sh 18,000 na hali ni hivyo katika mikoa mingine nchini.
Alisisitiza kuwa utafiti huo umethibitisha ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Julai mwaka huu kuwa mfumko wa bei umepanda kutoka asilimia 5.0 wakati bajeti inasomwa mpaka asilimia 5.9.
“Kiuchumi na hasa thamani ya pato la mwananchi, upandaji huu wa asilimia 0.9 ndani ya mwezi mmoja ni mkubwa mno. Hii ina maana kuwa shilingi 100 ya mwezi Juni 2007, ilishuka na kuwa sh 99.1 ilipofika Julai 2007. Hali ni mbaya zaidi kwa mfumko wa bei katika vyakula kwani, wakati mwezi Juni mfumko ulikuwa asilimia 2.8, mwezi Julai mfumko wa bei za vyakula ulipanda na kufikia asilimia 4.6 ambayo ni takriban maradufu. Hii ina maana kuwa chakula alichokuwa akinunua mwananchi kwa shilingi 100, mwezi mmoja tu baada ya bajeti ananunua kwa shilingi 122,” alisema Kiwelu.
Alisema mabadiliko yanayopendekezwa na Serikali katika sheria ya fedha yataumiza zaidi wananchi na kwamba kambi ya upinzani inashauri yasifanyike.
Kuhusu magunia ya katani, kambi ya upinzani ilimtaka Waziri wa Fedha kuweka kipengele cha sheria kinacholazimisha matumizi ya magunia ya katani kwa bidhaa muhimu ili kulinda viwanda vya magunia ya katani nchini na pia zao la katani kwa ujumla wake.
Akifanya majumuisho ya hoja hiyo pamoja na wabunge waliochangia, Waziri Meghji alisema suala la kupanda kwa bei ya mafuta ni la muda tu na kwamba tayari bei ya mafuta imeanza kushuka katika maeneo kadhaa nchini.