BAADHI ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameanza kuonyesha shaka dhidi ya utendaji kazi wa Spika wa Bunge, Samuel Sitta.
Shaka kubwa waliyoionyesha, ni kuhusu uwezo wake kama Spika wa Bunge katika kusimamia hoja za wabunge na kuzitolea maamuzi.
Ingawa kumekuwa na manung’uniko ya chini chini dhidi ya mwenendo wa Spika Sitta kulingana na ahadi zake kabla na baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo, hali hiyo sasa inaonekana kwenda mbali zaidi, baada ya Mbunge wa Manyoni Magharibi, John Lwanji (CCM), kutamka bayana bungeni kuwa, Spika Sitta anaacha hewani hoja nyingi za muhimu.
Akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya makadirio ya matumizi na mapato ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha wa 2007/2008, iliyowasilishwa bungeni juzi na Waziri Zakhia Meghji, Lwanji alisema anatamani Bunge liwe na Spika kutoka nje ya Bunge, tofauti na sasa ambapo ni mmoja kati ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano.
Alisema hali hiyo inatokana na kiti cha Spika (kwa sasa Samuel John Sitta) kuacha hoja nyingi za muhimu za baadhi ya wabunge, akiwemo yeye, bila kutolewa majibu ya uhakika wala kupatiwa ufumbuzi.
Akizungumzia masuala hayo aliyoyaita muhimu ambayo hayajapatiwa ufumbuzi, Lwanji alisema katika jimbo lake kuna tatizo la simba wala watu na hadi juzi wakati anatoa hoja hiyo, mtu mmoja aliripotiwa kuliwa na simba na kubakizwa kichwa ambacho kilizikwa juzi hiyo hiyo.
Alisema mtu huyo alikuwa akitoka katika moja ya vijiji vya Wilaya ya Manyoni kwenda mjini kwa ajili ya kupata huduma za kibenki, na akiwa njiani akiendesha baiskeli, alivamiwa na simba.
Lwanji alieleza kuwa, tatizo la simba wala watu katika wilaya hiyo ni la muda mrefu, na alishaliwasilisha bungeni, lakini hadi sasa halijapatiwa majibu na hata kiti cha Spika kimeliacha tatizo hilo pasipo majibu.
“Manyoni tuna tatizo la benki, watu wanatoka mbali kuja mjini kupata huduma za benki ya NMB, njiani wanakumbana na simba wala watu, nilishatoa malalamiko hapa, hakuna majibu, na Spika ameacha jambo hilo bila kupatiwa majibu.
“Mimi nadhani katiba inaruhusu Spika kutoka nje ya Bunge, labda tunaweza kupata majibu yetu kwa ufasaha, lakini tuliona busara tuwe na Spika kutoka ndani ya Bunge…,” alisema Lwanji.
Wakati akiendelea kulalamikia suala la Spika, Naibu Spika Anna Makinda aliingilia kati na kumtaka mbunge huyo kuwasilisha malalamiko yake katika taratibu zinazotakiwa, na kumtaka aelekeze hoja yake katika wizara iliyokuwa mbele yake.
Lwanji aliendelea, tatizo hilo la simba wala watu katika jimbo lake kuwa lina athari zake kiuchumi, kwamba idadi kubwa ya mifugo inaliwa na simba kila mwaka jambo linalorudisha nyuma juhudi za wananchi wa eneo hilo za kusonga mbele kiuchumi.
Aliitaka Wizara ya Fedha kuhakikisha huduma za benki ya NMB zinawafikia wananchi ili kuwaondolea urasimu wa NMB Manyoni pamoja na kuwaepusha na tatizo la simba.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili juzi katika viwanja vya Bunge, walieleza kuwa Spika Sitta atakabiliana na wakati mgumu katika kutekeleza ahadi zake kwa Watanzania wenye shauku ya kuona mabadiliko aliyoyaahidi baada ya kuyakosa kwa muda mrefu.
Wabunge hao ambao waliomba majina yao yasitajwe, walieleza kuwa Watanzania wengi sasa wanapata habari za Bunge baada ya vyombo vya habari kuanza kurusha moja kwa moja vikao vyake kupitia redio na televisheni.
Kwamba kushindwa kwa Spika kuchukua hatua hata katika masuala ambayo yalikuwa yakilidhalilisha Bunge, ni moja ya mambo ambayo yanapunguza imani ya wananchi dhidi ya Spika kwa kuzingatia ahadi zake alizotoa awali.
Hii si mara ya kwanza Spika Sitta kupingwa hadharani kuhusu mwenendo wa utendaji wake. Mara ya kwanza ni mapema mwaka jana wakati Watanzania wengi walipomshambulia baada ya kutangaza nia yake ya kupigania nyongeza ya mishahara na marupurupu ya wabunge wakati taifa likiwa katika baa la njaa na tatizo la mgawo wa umeme.
Aidha, Sitta pia alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuibuka malumbano kati yake na mbunge kijana wa CCM, Adam Malima, aliyefikia hatua ya kumshitaki kwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.
Wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa walieleza kuwa, Spika Sitta aliamua kutopambana wala kutomuadhibu Malima hata baada ya kubainika kuwa alilidanganya Bunge, kwa kuhofia kupokwa wadhifa wake na kundi la wanamtandao, ambalo linadaiwa lilikuwa limekwishaanza kumtazama kwa jicho la kumuengea.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, juzi alishindwa kujibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini, Siraji Kaboyonga (CCM), aliyetaka kujua fedha za ujenzi wa majengo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Twin Tower, zilikotoka.
Kaboyonga alisema gharama za ujenzi wa Twin Tower hazilingani na thamani ya mtaji wa BoT, hivyo, alihoji mahala zilipopatikana fedha za ujenzi huo, unaolalamikiwa kwa muda mrefu sasa.
Aliposimama kujibu swali hilo, Meghji alijikuta akitoa taarifa ya uchunguzi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akieleza kwamba umebaini kuwa ujenzi wa majengo hayo hauna matatizo kama inavyodhaniwa.
Wakati anakaa kwenye kiti chake, Kaboyonga alirejea tena swali lake. “Nafikiri waziri hajajua swali langu, nasema hivi, mtaji wa BoT ni sh bilioni 20, lakini thamani ya majengo yake, haiendani na mtaji huo, fedha hizo za ujenzi zimetoka wapi?”
Kabla ya Meghji kujibu, Naibu Spika, Anna Makinda, aliingilia kati na akatangaza kuafikiwa kwa kifungu hicho na baadhi ya wabunge kuitikia ‘ndiyo’.
Hata hivyo, katika kujaribu kuondoa kadhia hiyo, baadhi ya maofisa wa BoT waliokuwepo bungeni, walilazimika kutoa majibu ya ziada ambayo Waziri Meghji baadaye aliyasoma bungeni.
Akisoma majibu hayo, Meghji alisema fedha za ujenzi wa Twin Tower zimetokana na faida ya muda mrefu ambayo BoT ilikuwa imejiwekea.
Hata hivyo, hakutaja kiasi cha fedha kilicholimbikizwa hadi kujenga majengo hayo.