WAFANYAKAZI wa Mkoa wa Dar es Salaam, wamemtumia malalamiko mazito, Rais Jakaya Kikwete, kuhusu hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo, na wamemtaka awajibu ndani ya siku 30.
Wamemtuma Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Nestory Ngulla, kuwasilisha malalamiko yao hayo kwa Rais Kikwete na kurejesha majibu ndani ya siku 30, ili wasichukue hatua kali zaidi za kudai maslahi bora ya kazi.
Ngulla alipewa kazi hiyo jana katika kilele cha maandamano makubwa yaliyoandaliwa na TUCTA Mkoa wa Dar es Salaam, ya kuishinikiza serikali kuongeza mishahara yao.
Katika risala yao kwa Ngulla aliyekuwa mgeni rasmi, wafanyakazi waliishutumu Serikali ya Rais Kikwete, kuwa imekosa huruma na haitambui tena kuwa ni wafanyakazi na wakulima waliodai uhuru wa taifa hili.
Waliilamu serikali kwa kuwajali zaidi wafanyabisahara matajiri kama mhimili wa kusimamia sera, uchumi na siasa za nchi na kwamba serikali sasa inapuuza hata sheria zilizotungwa kusimamia na kulinda maslahi ya wafanyakazi.
Katika risala yao hiyo, pia wanamtaja Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia utumishi, Hawa Ghasia, kama mtu aliyeamua kupuuza utawala wa sheria na kuanzisha ukurasa mpya kwa kupanga mishahara ya wafanyakazi kwa matakwa yake.
Katika kile kinachoonyesha kukerwa na ongezeko kubwa la mishahara na marupurupu ya wabunge, walieleza kuwa kiwango cha mshahara cha sh 84,000 ni sawa na asilimia 50 au nusu ya posho ya mbunge anayopata katika kikao cha siku moja bungeni.
“Mshahara wa mbunge wa mwezi mmoja ambao ni sh 2,300,000, unaweza kumlipa mfanyakazi kwa miezi 17. Inasikitisha kiasi cha kujenga hasira mbaya katika jamii ya watanzania.
“…Tunajiuliza ni kwa namna gani uchumi au mapato ya nchi yanagawanywa? Wanaopewa mishahara mikubwa kiasi hicho wananunua chakula mbinguni au nchi za ng’ambo? Maswali yanazaliwa kutokana na pengo kubwa linaloonekana kwa baadhi ya wenzetu tuliowapa nafasi za maamuzi katika nchi, ndio wameweka pazia, wanaoona kinyaa kuangalia walikotoka,” inasomeka sehemu ya risala hiyo.
Inasisitiza kuwa, iwapo mishahara haitaongezwa, wafanyakazi hawatashiriki vita dhidi ya ukimwi wala rushwa, kwa vile serikali inachochea na kushawishi rushwa idumu kwa kulipa mishahara isiyowezesha mfanyakazi kuishi kwa siku 30 za mwezi.
Risala hiyo ilitaja athari nyingine zitakazojitokeza iwapo serikali itaendelea kukaidi kuongeza mishahara kuwa ni pamoja na kupotea kwa nidhamu ya kazi kwa vile wafanyakazi watalazimika kutumia muda mwingi katika mapumziko haramu yatokanayo na unyonge wa kukosa kazi na ujinga na maradhi kuongezeka.
Aidha, katika risala hiyo walieleza kuwa iwapo serikali itakubali madai yao na kuongeza mishahara, wataongeza ari ya kazi na kuwa walinzi wazuri wa uchumi wa taifa.
“Tunapenda kukujulisha kuwa wafanyakazi tukiongezewa mishahara, tutaongeza ari ya kazi, tutakuwa walinzi wazuri wa uchumi wa taifa. Tunakutuma uyafikishe malalamiko yetu kwa Mheshimiwa Rais ndani ya siku 30 na uturudishie majibu ili kuzuia hatua nyingine zaidi ambazo tutazitumia kudai mishahara hiyo,” alieleza risala hiyo.
Akizungumza baada ya kupokea risala hiyo, Ngulla alisema anakubaliana na malalamiko hayo ya wafanyakazi na atayafikisha kwa rais kama alivyotakiwa.
“Tunayo silaha ya kutumia kama kilio chetu kikipuuzwa,” alisema huku wafanyakazi hao wakishangilia na kudai kuwa mgomo pia ni haki yao katika kudai haki zao.
Ngulla alisema wafanyakazi wananyanyasika kwa kulipwa kiwango kidogo cha mshahara kulinganisha na wanasiasa na walio katika makundi mengine katika jamii.
Naye Profesa Issa Shivji, akizungumza wakati wa kupokea maandamano hayo katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, alisema nchi inagawanyika kwa kuwa na kundi la watu wachache wenye nazo na walalahoi, ambao ndio kundi kubwa.
Prof. Shivji alisema serikali imewakumbatia wafanyabiashara na kuwasahau wakulima na wafanyakazi, ambao ni walalahoi na ndio mhimili wa uchumi wa nchi, kitu ambacho watawala wanakifumbia macho.
Alisema wasomi nao wamepotoka kwa kuwashabikia wageni ambao wanawaita wawekezaji, lakini kimsingi ni walimbikizaji wa rasilimali za walalahoi na kudai kuwa walio wengi wanachokisema sicho anachomaanisha.
“Wasomi wamepotoka, walio wengi wanawakumbatia walaji, huku wakidai kuwa wanawapigia debe walalahoi,” alisema huku akishangiliwa na waandamanaji ambao walianza maandamano yao Makao Makuu ya TUCTA.
Wafanyakazi hao waliandamana huku wakiwa na mabango yenye ujumbe tofauti na yapo ambayo yalisomeka kuwa, mashangingi yauzwe kiongezwe kima cha mshahara, mengine yakitaka posho ya kufundishia irudishwe kwa walimu na mengine yakihoji wabunge kulipwa sh 120,000 kwa siku ilhali mishahara ya kima cha chini ni sh 84,000 kwa mwezi.
Ngulla alisema kuwa, kilio kimesikika na atakipeleka mbele zaidi na kama ikishindikana, wafanyakazi hao watatumia sialaha yao ya mwisho kudai haki yao.
Kilio cha wafanyakazi hao kimekuja baada ya kuona ndoto zao za kuingia katika maisha bora kama ilivyokuwa imeahidiwa na Rais Kikwete, zikielekea kuyeyuka, kwani tangu aingie madarakani mwishoni mwa mwaka 2005, hakuwahi kuongeza mshahara, hadi Juni mwaka huu wakati Waziri wa Nchi (Utumishi), Hawa Ghasia alipowasilisha bungeni makadirio ya wizara yake na kuonyesha kwamba, kutakuwa na ongezeko la mshahara la asilimia 17, ambako kwa kima cha chini, ni sawa na nyongeza ya sh 9,000. Kima kipya cha mshahara kwa mujibu wa mabadiliko hayo ni sh 84,000 kilichopanda kutoka sh 75,000.