RAIS Jakaya Kikwete, amesema sasa mji wa Dodoma unaanza kupata sura na heshima ya kuwa makao makuu ya nchi inayostahili.
Alisema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la Hospitali ya Rufaa ya Dodoma Christian Medical Centre (DCMC), inayojengwa kwa ufadhili wa Kanisa la Marekani la Calvary Lutheran, eneo la Ntyuka nje kidogo ya Mansipaa ya Dodoma.
Rais Kikwete alisema ni zawadi ya thamani kubwa si kwa watu wa Dodoma tu, bali kwa mikoa ya Kanda ya Kati na Tanzania kwa ujumla.
Alisema heshima hiyo inaanza kuonekana, kwa sababu hospitali hiyo imeanza kujengwa karibu na maeneo ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
“Mapema mwezi huu tukafungua jengo jipya na la kuvutia la Bunge hapa Dodoma, leo tunaweka jiwe la msingi la Hospitali ya Rufaa,” alisema Rais Kikwete.
Alisema serikali inatambua na kuthamini mchango wa mashirika ya dini katika utoaji wa huduma za afya nchini kwani kwa sasa asilimia 40 ya huduma za afya, inatolewa na mashirika ya dini.
Rais alisema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri zaidi kwa mashirika ya dini na wadau wengine, ili kurahisisha uwekezaji katika huduma za afya na elimu.
“Hivyo mkimaliza ujenzi Dodoma, basi jengeni sehemu nyingine,” alisema Rais Kikwete.
Alisema wafadhili hao hawakujenga hospitali hiyo kwa sababu ya uwezo wa kusaidia, bali kwa ukarimu wao uliorutubishwa na mafunzo ya Bwana Yesu Kristo.
Alisema hospitali hiyo kujengwa mkoani Dodoma ni muhimu, kwa kwa sababu mahitaji ya huduma za afya kwa mkoa ni makubwa, kwani Wilaya ya Kongwa na Mpwapwa zinaongoza kwa vifo vya watoto na kina mama wakati wa uzazi.
“Tanzania ina hospitali za rufaa nne, zilizogawanyika kikanda, lakini kwa Kanda ya Kati haikuwapo ya rufaa, hivyo hospitali hii itapunguza kero na aibu,” alisisitiza Kikwete.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dk. Samson Mushemba, alisema hospitali hiyo itasogeza huduma ya afya kwa karibu zaidi na kushughulikia matatizo sugu katika kanda hii.
Ujenzi wa hospitali hiyo unatarajiwa kugharimu dola milioni 7 hadi kukamilika kwake. Kwa sasa Mkoa wa Dodoma una hospitali sita, vituo 17 vya afya na zahanati 204, ambazo bado hazikidhi haja ya huduma ya afya.