Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Dalili mbaya Zanzibar
Dalili mbaya Zanzibar
By Marshy Abdu | Published  08/11/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
Dalili mbaya Zanzibar
Wabunge 31 wa CUF waondoka Dodoma

na Mwandishi Wetu


HALI ya kisiasa ya Zanzibar imeendelea kuwa ni ya wasiwasi mkubwa kutokana na matukio yaliyoanza kujitokeza katika kipindi cha siku za hivi karibuni.

Baada ya viongozi mashuhuri wa kitaifa na kimataifa kuanza kueleza wasiwasi wao kuhusu mwenendo wa mambo visiwani Zanzibar, sasa ni dhahiri utete wa kile Rais Jakaya Kikwete alichopata kukielezea kuwa ni mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar, umeanza kubainika hatua kwa hatua.

Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka Unguja na Pemba, zinaonyesha kuwa, tayari wananchi wa visiwani humo wameshaanza kuonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu kuanza tena kuzorota kwa hali ya mambo visiwani huko, tangu Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba autangazie ulimwengu kuwa, mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa visiwani humo yalikuwa yamekwama.

Wakati hayo yakitokea, mjini Dodoma kunakoendelea vikao vya Bunge la Bajeti, habari zinaeleza kuwa, chama hicho cha upinzani kilikuwa kimewaamuru wabunge wake wote kuondoka huko na kuelekea Zanzibar kwa ajili ya vikao maalumu ya kujadili hali ya kisiasa Zanzibar.

Habari ambazo zilithibitishwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed, zinaeleza kuwa, hadi kufikia jana saa 5:00 asubuhi chama hicho kilikuwa kimembakiza mbunge wake mmoja tu, Fatuma Fereji kwa ajili ya kukamilisha shughuli za kibunge.

Hamad Rashid alilieleza Tanzania Daima kwa njia ya simu jana jioni kuwa, Fereji alikuwa akitarajiwa kuondoka Dodoma leo hii na kuungana na wenzake wengine katika vikao maalum vitakavyofanyika Unguja na Pemba.

Hamad, mmoja wa wabunge wenye ushawishi mkubwa, alilithibitishia gazeti hili kuwa, ajenda kuu katika vikao vyao hivyo, vitakavyowashirikisha wabunge na wawakilishi wote wanaotokana na chama hicho itakuwa ni kutathmini mwenendo wa mambo yanayozingira mazungumzo kati ya chama hicho na mahasimu wao wakuu wa kisiasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Ni kweli tumeondoka wote leo tukamuacha Fatuma Fereji bungeni, ambaye naye ataondoka kesho (leo). Tumeomba ruhusa kwa Spika kwa ajili ya shughuli maalum ya chama,” alisema Hamad alipopigiwa simu na gazeti hili jana.

Bila ya kuingia kwa undani, Hamad alisema kuwa, walikuwa wakitarajia kurejea Dodoma kati ya kesho Jumapili au Jumatatu asubuhi kwa ajili ya kuendelea na vikao vya Bunge.

Hata hivyo, habari nyingine ambazo Tanzania Daima ilizipata jana asubuhi, zilikuwa zikieleza kuwa, mkakati wa awali uliojumuisha wabunge wote wa upinzani ulitaka kuona suala hilo la Zanzibar likiwashirikisha wote na si wabunge 32 tu wa CUF.

Kwa mujibu wa habari hizo ambazo hata hivyo Hamad Rashid alikataa kuzithibitisha, chini ya makubaliano hayo, wabunge wengine wote wa vyama vya upinzani kutoka vyama vya Chadema, TLP na UDP, nao walikuwa wakitarajia kuondoka bungeni kuanzia Jumatatu, nia ikiwa ni kuwaunga mkono wenzao wa CUF.

Mbunge mmoja wa upinzani asiye wa CUF aliyezungumza na gazeti hili jana kutoka Dodoma, alithibitisha kuhusu kuwapo kwa nia ya kuwaunga mkono wenzao wa CUF, wakitambua kuwa tatizo wanaloshughulikia lina maslahi ya kitaifa zaidi kuliko chama kimoja tu cha siasa.

Hamad Rashid kwa upande wake, alisema anachokijua yeye ni kuwa, wabunge wote wa CUF watarajea kati ya kesho na keshokutwa na iwapo kutakuwa na mabadiliko yoyote katika suala hilo, basi taarifa zitatolewa.

Wakati CUF ikionekana kujipanga kwa ajili ya kufikia uamuzi wa mwisho kuhusu hatima ya mazungumzo yao na wenzao wa CCM, huko Zanzibar, ile desturi ya watu wasiojulikana kusambaza vikaratasi vyenye maneno makali makali, ilionekana kujirudia kuanzia usiku wa kuamkia jana.

Mwandishi wetu aliye Zanzibar alilieleza gazeti hili kuwa, moja ya vikaratasi hivyo vilivyokuwa vimeandikwa kwa wino mwekundu, kilikuwa kina maneno yaliyokuwa yakieleza kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa baada ya kukwama kwa mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu tatizo la kisiasa la Zanzibar.

Kwa mujibu wa mwandishi wetu huyo, vikaratasi hivyo vimesababisha hali ya wasiwasi miongoni mwa Wazanzibari kadhaa, ambao wamekaririwa wakiomba Mungu visiwa hivyo visikumbwe tena na matukio ya vurugu kama zile zilizotokea mwaka 2001.

Mambo yote hayo yanakuja siku chache tu baada ya Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim na Balozi wa Marekani hapa nchini, Michael Ratzer, kusisitiza kuhusu haja ya kuendelea kwa mazungumzo hayo, na kufikiwa kwa ufumbuzi wa kudumu.

Aidha, matukio hayo yanayoweza kuviingiza visiwa hivyo ambavyo tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 havijatulia kisiasa, kuingia tena katika vurugu za kisiasa.

Hivi majuzi, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba, alieleza wasiwasi wake kuhusu kukwama kwa mazungumzo hayo na akailaumu CCM akisema ndiyo inayopaswa kulaumiwa.

Akizungumza na wanahabari katika ofisi za makao makuu ya CUF, Buguruni, jijini Dar es Salaam, Lipumba alisema, kukwama kwa mazungumzo haya kumetokana na CCM kuingia katika mzungumzo haya ikiwa na haina dhamira ya kweli ya kuupatia ufumbuzi mpasuko wa kisiasa ulioko Zanzibar.

Profesa Lipumba aliitaja sababu nyingine inayoonyesha kukwama kwa mazungumzo hayo kuwa ni Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kushindwa kusimamia ipasavyo mazungumzo hayo na kutoa mwongozo wa kisiasa unaohitajika.

“Imeonekana lengo pekee la CCM katika mazungumzo haya lilikuwa kuwahadaa Watanzania na jumuiya za kimataifa kwa kujaribu kuidhibiti CUF kupitia utaratibu wa kuwapa matumaini ya uongo na kuyarefusha mazungumzo kadiri inavyowezekana hadi kipindi kinachokaribia uchaguzi mkuu pasipo kuchukuwa hatua zozote za maana zinazolenga kutoa ufumbuzi wa kweli, haki na wa kudumu,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema kutokana na hali hiyo, CCM imeonyesha waziwazi kuwa inachezea amani iliyopo na kwamba haiitakii mema Tanzania, kwa vile haitaki kuona umoja wa kitaifa na utulivu wa kudumu unapatikana Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.

Alisema CUF kwa upande wake, inachukua hatua hiyo kuwahakikisha Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwamba imechukua juhudi za kuona mazungumzo hayo yanapata ufumbuzi.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu kuhusu kauli hiyo ya Lipumba, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, alieleza kushutushwa na kauli hiyo, akisema mazungumzo baina yao yalikuwa bado yanaendelea.

“Nimeshitushwa sana na kauli ya CUF, kwamba wameamua kuachana na mazungumzo haya, tumetoka mbali, sasa kwanini Profesa Lipumba ambaye si msemaji amefikia hatua hiyo? Nilitegemea Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad ambaye tuko naye kwenye kamati ndiye mwenye kulizungumzia suala hili,” alisema Makamba bila ya kujua wakati Lipumba akitoa kauli hiyo alikuwa ameongozana na Maalim.

Shaka kuhusu kusuasua kwa mazungumzo hayo, ilianza tangu Makamba afanye ziara Pemba miezi takriban mitatu iliyopita na kueleza kuwa, kulikuwa hakuna serikali ya mseto wala uchaguzi mwingine Zanzibar kabla ya mwaka 2010.

Aidha, CUF wamekuwa wakieleza kuhusu wasiwasi wa kukwama kwa mazungumzo haya kutokana uamuzi wa Rais Kikwete kuamua kutojibu barua zao za kulalamikia mwenendo wa kauli za wanasiasa kadhaa wakiwamo, Makamba na baada yake Kingunge Ngombale Mwiru.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.