MGOGORO mpya unaweza ukaibuka tena katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), baada ya uongozi wa chuo hicho kuwaandikia barua ya kujieleza na kuitwa kwenye kamati ya nidhamu wanafunzi 20 ambao awali walisimamishwa masomo na kuwarejesha tena baada ya wenzao kutishia kugoma.
Habari zilizolifikia Tanzania Daima zinaeleza kuwa ubaya wa barua kuwa ni kwamba zimetolewa wakati wanafunzi hao wako likizo ambapo wahusika wengi wako mikoani na wengine nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali.
Tanzania Daima inayo nakala ya barua hiyo ambayo inamtaka kila aliyeandikiwa baada ya kuichukua aandike maelezo ya kujitetea ndani ya siku saba na kwamba Agosti 20 mwaka huu wataitwa kwenye Kamati ya Nidhamu chuoni hapo ambayo itakuwa imeteuliwa kwa mahojiano zaidi.
Kwa maelezo ya mmoja wa wanafunzi ambao wamepatiwa barua hizo, alisema barua hizo zinapingana na madai ya awali ambayo walituhumiwa.
“Mbaya zaidi hizi barua zinapingana na madai ya kwanza ambayo tulishaletewa. Madai ya sasa ni mengine ambayo hatukuwahi kuyazungumzia. Kwa maelezo mengine ni madai mapya,” alisema mwanafunzi huyo kwa niaba ya wenzake.
Alieleza kuwa madai hayo badala ya kuzungumzia kupinga sera ya asilimia 40 ambayo tayari imerekebishwa, sasa wanatuhumiwa kuwa walikuwa wanaipinga Bodi ya Mikopo, jambo ambalo amesema halina ukweli.
“Tulikuwa tunapingana na sera hasa ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza ambao tayari imesharekebishwa,”alisema mwanafunzi huyo.
Alisema kuwa barua hizo walizoandikiwa sasa zinaonekana zimetoka sehemu ambazo hakuna uhakika kama kuna tuhuma wanazodaiwa kwa sababu barua nyingi zimekosewa majina, namba za usajili za wanafunzi, vitivo vyao na hata shahada wanazochukua.
“Suala hili sasa linaweza kuleta mgogoro mkubwa sana kitu ambacho hakikutarajiwa chuo kitakapofunguliwa. Wanafunzi walishasahau suala hili kutokana na mabadiliko mazuri ya serikali yaliyofanywa. Hali hii italeta uhasama kati ya utawala wa chuo na wanafunzi,” alisema.
Alisema serikali imetambua kilio cha wanafunzi hao kilichowasababisha wakagoma na kufanya marekebisho mazuri, lakini baadhi ya watawala wa chuo, wanataka kusababisha hali ya kutokuwa na utulivu.
“Sisi kama wahanga tumesikitishwa na kitendo hicho, hatuwezi kuendeshwa kidikteta wakati pande nyingine wakiwepo wabunge wametambua kilio chetu ila chuo kinaleta uhasama kati yetu,” alisema mwanafunzi huyo.
Alisema wanafunzi hao wanashangaa kwa kuwa hawajapewa majibu ya kesi yao ya awali waliyohojiwa, wanaanzishiwa kesi nyingine. Alihoji itakuwaje kwa wanafunzi ambao wako nje ya Mkoa wa Dar es Salaam na nje ya nchi endapo barua zao hazitawafikia wala kufika kwenye kamati ya nidhamu.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Mipango, Fedha na Utawala), Profesa Yunus Mgaya, alikiri chuo kutoa barua kwa wanafunzi 20 ambao walionekana kuwa ni vinara wa mgomo baada ya mchujo wa awali.
Profesa Mgaya alisema katika barua hiyo wametoa siku saba kama kuna mwanafunzi ambaye yuko nje ya Mkoa wa Dar es Salaam au nje ya nchi aanze kupanga safari ili aweze kufika kwenye kamati ya nidhamu ambayo inatarajiwa kuketi Agosti 20, mwaka huu.
Alisema wanafunzi hao wanatuhumiwa kwa kuvunja taratibu za chuo chini ya sheria ndogo za chuo zilizowekwa, na ndiyo maana chuo kimewapa nafasi ya kujieleza tena kwa kuandika maelezo ndani ya siku saba na kuitwa kwenye kamati hiyo ya nidhamu.
Alipoulizwa kwamba kuna uwezekano chuo kitakapofunguliwa kuwepo kwa mgomo mwingine, Mgaya alisema bado hawajajua kama maamuzi ya chuo hicho yanaweza kuzusha upya mgogoro chuoni hapo.
“Hatujajua kama suala hili linaweza kuzusha mgomo mwingine chuoni hapa, ngoja tuwape nafasi ya kuwasikiliza, kwani bado hatujawatuhumu. Bado hayajawa maamuzi ya mwisho hii ni mwanzo tu,” alisema Mgaya.
Alisema wanafunzi hao wamevunja taratibu za chuo, hivyo kamati ya awali iliwabaini hao 56 ndiyo waliohusika, kamati hiyo ikatoa ripoti kwamba wanafunzi hao wana kesi ya kujibu.
Aprili mwaka huu, Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lilitangaza kuwasimamisha masomo kwa muda usiojulikana, wanafunzi wote wa shahada za awali kutokana na mgomo waliouitisha kuishinikiza serikali iwaongezee fedha za mikopo.
Mei mwaka huu uongozi wa UDSM uliwarejesha wanafunzi wote isipokuwa wanafunzi 56 walioshiriki katika mgomo wa kuishinikiza serikali iwalipie gharama kamili za masomo yao kwa maelezo kuwa walikuwa vinara wa mgomo.