CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) kila kimoja kwa wakati wake, vimeeleza kusikitishwa na mwenendo wa mwingine katika mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kisiasa ya Zanzibar ambayo katika siku za hivi karibuni yameonekana kulegalega.
Kiongozi wa kwanza kueleza dukuduku lake hilo safari hii alikuwa ni Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alisema mazungumzo hayo yalikuwa yamekwama na juhudi za kuyakwamua zilikuwa zikionyesha dalili mbaya.
Akizungumza na wana habari katika ofisi za makao makuu ya CUF, Buguruni, jijini Dar es Salaam jana, Lipumba alisema chama chake kimelazimika kuwatangazia Watanzania na ulimwengu mzima kuwa mazungumzo hayo yaliyochukua miezi minane yamekwama kwa kipindi kirefu sasa.
“Kukwama kwa mazungumzo haya kumetokana na CCM kuingia katika mzungumzo haya ikiwa haina dhamira ya kweli ya kuupatia ufumbuzi mpasuko wa kisiasa ulioko Zanzibar,” alisema Profesa Lipumba, jambo ambalo lilikanushwa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba muda mfupi baadaye.
Profesa Lipumba aliitaja sababu nyingine inayoonyesha kukwama kwa mazungumzo hayo kuwa ni Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kushindwa kusimamia ipasavyo mazungumzo hayo na kutoa mwongozo wa kisiasa unaohitajika.
“Imeonekana lengo pekee la CCM katika mazungumzo haya lilikuwa kuwahadaa Watanzania na jumuia za kimataifa kwa kujaribu kuidhibiti CUF kupitia utaratibu wa kuwapa matumaini ya uongo na kuyarefusha mazungumzo kadiri inavyowezekana hadi kipindi kinachokaribia uchaguzi mkuu pasipo kuchukua hatua zozote za maana zinazolenga kutoa ufumbuzi wa kweli, haki na wa kudumu,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema kutokana na hali hiyo, CCM imeonyesha waziwazi kuwa inachezea amani iliyopo na kwamba haiitakii mema Tanzania, kwa vile haitaki kuona umoja wa kitaifa na utuluvu wa kudumu unapatikana Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema CUF kwa upande wake inachukua hatua hiyo kuwahakikishia Watanzania na jumuia ya kimataifa kwamba imechukua juhudi za kuona mazungumzo hayo yanapata ufumbuzi.
“CUF imetoa kila aina ya ushirikiano kwa CCM unaohitajika na hata kuachia madai yake makuu ili kunusuru mazungumzo na kuyafanikisha, lakini CCM haionekani kuyajali au kuthamini juhudi hizo, sasa tusipoziba ufa Zanzibar tutajenga ukuta Tanzania,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema maelezo ya kina kuhusu nini kilichojiri kwenye mazungumzo hayo chama chake kitayatoa kwa Watanzania na ulimwengu mzima baada ya kumalizika muda waliokubalina na CCM kwa maandishi kati ya makatibu wakuu wa vyama hivyo Agosti 15 mwaka huu.
Alisema hali ya kisiasa Zanzibar bado ni mbaya kutokana na wananchi kukatishwa tamaa na tabia ya kigeugeu, hadaa na hiana ya CCM inayolenga kuendelea kuibakisha Zanzibar katika mgogoro.
“Kumbukumbu za wananchi na hujuma za CCM kuvuruga mwafaka wa kwanza na wa pili, zinaonekana kuthibitishwa na hatua za sasa za kukwamisha na kuyavuruga mazungumzo tuliyoyaanza kwa imani kubwa,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema ni jambo la hatari kwa nchi yoyote kwa watu wake kukata tamaa, kwani kufanya hivyo wanaweza kujichukulia sheria mikononi na kuigharimu nchi na kuiondolea sifa iliyokwisha kujitangazia kuwa ni kisima cha amani katika Bara la Afrika.
“Sasa CCM wanataka kuleta yale yanayotokea kwenye Jimbo la Darfur nchini Sudan, sisi CUF tunasema hatutaki kuyaona kamwe kwa vile hayana faida kwetu,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema baada ya Tanzania yenyewe kushindwa katika utatuzi wa mgogoro huo wa muda mrefu, wakati umefika kwa jumuia ya kimataifa kuingilia kati kwa kuchagua mpatanishi anayeheshimika kuja kusuluhisha suala hilo ili aweze kufikisha ukingoni makubaliano ya dhati yatakayotoa ufumbuzi wa kweli na wa haki wa mpusuko wa kisiasa Zanzibar.
“Jumuiya ya kimataifa iepuke fedheha iliyoipata katika nchi nyingine za Afrika ambazo iliziacha hadi hali ikachafuka na ndipo ikaingilia kati, hali ya Zanzibar bado ni mbaya sana, ilitulia kwa vile wananchi walikuwa na matumaini ya kufikiwa muafaka chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete aliyeahidi kumaliza tatizo hili,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema mara baada ta Agosti 15 ambayo ndiyo siku ya mwisho ya mazungumzo hayo, CUF itapeleka suala hilo kwa wananchi ili waamue nini cha kufanya.
Akizungumza na Tanzania Daima kuhusiana na kauli hiyo kwa simu jana, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, alisema ameshutushwa na kauli hiyo kwa vile mazungumzo baina yao bado yanaendelea.
“Nimeshtushwa sana na kauli ya CUF kwamba wameamua kuachana na mazungumzo haya, tumetoka mbali, sasa kwanini Profesa Lipumba ambaye si msemaji amefikia hatua hiyo? Nilitegemea Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye tuko naye kwenye kamati ndiye mwenye kulizungumzia suala hili,” alisema Makamba.
Alisema sababu kubwa ya kuahirisha mazungumzo hayo ilitokana na yeye kuwa safarini mkoani Kigoma, pia kukabiliwa na mikutano ya Kamati Kuu ya CCM mjini Dodoma, hali iliyosababisha kusitisha mazungumzo hayo.
“Kabla ya safari ya kwenda Kigoma na kwenye mkutano wa Kamati Kuu ya CCM niliwasiliana na mwenzangu, Maalim Seif kwa ajili ya kusitisha mazungumzo haya hadi nitakaporudi, na yeye alikubali, sasa uamuzi huo umetoka wapi?” alihoji Makamba.
Alisema CCM inaamini kwamba mazungumzo hayo hayajakwama, kwa kuwa muda waliokubaliana nao bado uko palepale na kwamba watafikia muafaka.
Kuhusu suala la kusema kwamba CCM wanachezea amani, Makamba alisema hali inayoonyeshwa na CUF imeashiria wazi kwamba wanataka kuvuruga umoja na amani iliyopo nchini.
“Sasa kama wao wanasema kwamba baada ya Agosti 15 watapeleka suala hili kwa wananchi, wanataka kuvuruga umoja na amani iliyopo nchini, napenda kuwaasa waache,” alisema Lipumba.
Kuhusu suala la msuluhishi wa kimataifa, Makamba alisema hakuna sababu yoyote ya msingi ya kuletwa kwa msuluhishi huyo kwa vile atakuwa hajui nini kinachoendelea kati ya CCM na CUF.
“Jamani sasa wanataka kuleta msuluhishi wa nini? Yeye anajua nini katika mazungumzo haya…sisi ndiyo ambao tunaelewa kila kitu katika vyama vyetu na kwamba mazungumzo haya yatafikia mwafaka bila msuluhishi kutoka nje,” alisema Makamba.
“Kama tatizo jingine ni uchaguzi wa Zanzibar, vyama vyote tulishiriki na kile kilichoshinda ndicho kilichounda serikali sasa tatizo liko wapi? Aliyeshinda anajulika,” alisema Makamba.