WAZIRI Mkuu mstaafu na mwanasheria mkongwe, Jaji Joseph Warioba, ameeleza kushangazwa kwake na tabia za ukigeugeu za baadhi ya watu wanaohamahama vyama vya siasa.
Warioba, mmoja wa wanasiasa wanaoheshimika hapa nchini alitoa changamoto hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mjadala wa mabadiliko ya katiba ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia nchini (TCD).
Mwanasiasa huyo aliyepata kuongoza Tume ya Rais ya Kuchunguza Mianya ya Rushwa, maarufu kama Tume ya Warioba alieleza kushangazwa na tabia ya baadhi ya wanasiasa kuwashambulia wenzao wa vyama vingine na kisha wao wenyewe kuhamia katika vyama walivyokuwa wakiviponda kwa kukimwagia sifa.
Bila ya kutaja jina la mwanasiasa yeyote, Jaji Warioba alisema jambo baya zaidi ni kwamba, wanasiasa hao wanapohamia katika vyama vingine hupokewa kwa mbwembwe za kupewa madaraka, kitu ambacho huwa hakiwafurahishi baadhi ya wanachama ambao siku zote wamekuwa watiifu kwa chama hicho.
Alisema kuwa hatari haiishii hapo tu, kwani hata ndani ya vyama nako kumeanza kuonekana kuwapo kwa migawanyiko inayojengwa na makundi mbalimbali.
Alisema hivi sasa ni jambo la kawaida kwa mitandao ndani ya vyama ikiendelea kupingana waziwazi wakati wa kuwania uongozi na hata baada ya hapo, licha ya kuwapo kwa kauli zinazodai kuwa mashindano ya namna hii ndani ya chama, huisha baada ya uchaguzi.
Alisema hali hiyo inadhoofisha mshikamano na endapo umoja ndani ya vyama vya siasa utadhoofu, basi kuna hatari hata umoja wa nchi na demokrasia kwa jumla kuyumba.
Aliongeza kuwa, kusudi moja la msingi la kuwapo kwa mfumo wa vyama vingi ni kuweka utaratibu wa kutengeneza demokrasia, hivyo vyama vinapaswa kujenga demokrasia kuanzia ndani.
Mbali ya hilo, Jaji Warioba alionya kuwa hali ya mambo inaonyesha kuwa, vyama vya siasa vinawagawa wananchi, hasa maeneo ya vijijini.
Alisema kuwa muonekano huo wa vyama vya siasa, ambao unawatenga watu katika makundi, mfano wa makabila, unahatarisha uhuru na mshikamano wa Watanzania.
Mwanazuoni huyo, alisema hali hiyo inatakiwa kurekebishwa mara moja ili isifikie hatua ya watu kuwa na uhasama kutokana na itikadi tofauti.
Aidha, akizungumzia wajibu wa Bunge alisema kuna haja ya kufanya mabadiliko yatakayolipatia Bunge nguvu zaidi katika kuisimamia serikali.
Alisema mbali ya kulipa Bunge nguvu, ipo haja vile vile ya kufanya mabadiliko yatakayoainisha kinagaubaga, mgawanyo wa madaraka baina ya serikali na chombo hicho cha kutunga sheria.
Alionya kuhusu kuongezeka kwa hatari ya serikali kulisimamia Bunge, badala ya Bunge kuisimamia serikali, kutokana na pamoja na mambo mengine, wingi wa mawaziri walioko bungeni.
Alisema hiyo imeanza kujidhihirisha wazi hivi sasa kwa wabunge wakati wakichangia mada mbalimbali kuanza kutumia maneno ya kuomba na kuishauri serikali badala ya kuiagiza.
Alisema umefika wakati kwa Tanzania kuanza kutafuta utaratibu ambao utawafanya wabunge wakiingia bungeni wawe sawa.
Alisema umefika wakati wa mabadiliko makubwa yatakayowawezesha wananchi kuhusishwa kuliko ilivyo hivi sasa ambapo semina na mikutano ambayo inahudhuriwa na wadau ndiyo inayopewa nafasi.
Warioba alisema kuongoza kwa kutafuta maoni ya watu unaowaongoza ni kuzuri kuliko kuongoza kwa semina na mikutano inayoendeshwa na wafadhili.
Aidha, alisema hivi sasa nchi zinazoendelea kama Tanzania zinabanwa na masharti ya utandawazi, ambayo yanazifanya kuwa kimya kuhusu matatizo yanayotokea duniani kwa kusikiliza wakubwa, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo Tanzania ilikuwa ikiongea.