Na Waandishi Wetu
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, ameeleza kukerwa kwake na na tabia ya baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa mamluki kwa kikimbilia vyama vingine kutafuta maslahi binafsi na kugeuka kama vinyonga. Vilevile, ameshangaa kwa nini vyama vinawapokea kwa shangwe na kuwapa madaraka.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa wadau kuangalia umuhimu wa marekebisho ya katiba kwa sasa, Warioba alisema tabia hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kudidimiza demokrasia.
"Aina hii ya viongozi ambayo tumekuwa tukiishuhudia inaleta mashaka, leo utamkuta katika chama hiki, anakitukana chama hiki, kesho ukimkuta kwenye chama kingine anakitukana kile alichokiacha kama vile hakuwahi kukisifia awali, cha ajabu viongozi wa aina hii wanapokelewa tena kwa mbwembwe na kupewa uongozi wa juu katika vyama wanavyokimbilia, lakini baada ya muda wasipopata wanachokitaka wanahama tena, hapa demokrasia inakuwa matatani," alisema Warioba.
Alisistiza kuwa viongozi wa aina hii hawana sababu ya kubebwa kwa kuwa kwa imani yake chama chochote ni sera kwa hiyo yeyote anayekimbilia chama kwa sababu ya maslahi binafsi na madaraka, ni mamaluki wa kisiasa asiyepaswa kuvumiliwa katika jamii yoyote.
Hata hivyo, Warioba alisema umoja wa kitaifa unaletwa na viongozi wa vyama vya siasa kuanzia ndani ya vyama vyao, hivyo kuvurugika ndani ni kudhoofisha umoja huo na kuua demokrasia.
Akizungumzia namna vyama vya siasa vinavyoedndeshwa nchini, Warioba alivitaka vyama hivyo kuacha utegemezi wa wafadhili kutoka nje na kuanza kutumia utaratibu wa kuwaunganisha wananchi kujenga vyama hivyo.
"Tatizo hili limevifanya vyama kuwa mbali na wananchi, haviwezi kuwakilisha mawazo ya wananchi, hatma yake viongozi wanataka kuwalazimisha wananchi kutekeleza mawazo yao, wanasahau kuwa wananchi kule walipo wana mahitaji yao na wapo wenye busara za kutosha, inapofikia hatua hiyo dhana ya demokrasia inapotea," alisisitiza.
Hata hivyo, alsema demokrasia lazima ianzie ndani ya vyama kwa kuwa haviwezi kusimamia ujenzi wa demokrasia ndani ya vyama hivyo, ambapo demokrasia inatokana na wananchi na vyama hivyo vinasimamia utekelezaji wa hitaji hilo la wananchi.
Aliwataka wanasiasa kuacha tabia za mamluki katika vyama na kusimamia maslahi binafsi, suala linaloleta utata juu ya uhai wa demokrasia ya kweli nchini.
Warioba pia alilaumu makundi ya uchaguzi katika vyama ambayo yanaendelea kuwapo hata baada ya chaguzi husika kumalizika.
"Ni kweli kwamba mahali popote duniani huwa kunakuwa na makundi kwa ajili ya uchaguzi mara unapofika, lakini kwa watu wenye utashi mzuri, uchaguzi unapomalizika, mnarudi katika imani zenu, lakini katika makundi ya mitandao tunayoyaona hapa nchini hata baada ya uchaguzi yanakuwa yanaendeleza mambo ya nyuma, hii inahatarisha na kudhoofisha umoja wetu kitaifa," alisema.
Alisema harakati hizo husababisha kubomolewa kwa misingi ya umoja wa kitaifa kama inavyoanishwa katika katiba ya nchi iliyopo kwa sasa; "kwa hiyo katiba inapobomolewa misingi yake si katiba tena," alisisitiza.
Mkutano huo wa kujadili umuhimu wa mabadiliko ya katiba kwa sasa, ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), umekutanisha wadau ambao ni viongozi wa vyama vya siasa na taasisi binafsi, za kidini na asasi zisizo za kiserikali.