Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  SMZ sasa yakiri upungufu
SMZ sasa yakiri upungufu
By Habari Tanzania | Published  08/5/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Saada Said, Zanzibar


SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imekiri kwamba inazo kasoro kadhaa katika utekelezaji wa utawala bora.

Imesema serikali inatambua kuwepo kwa kasoro hizo, lakini inaendelea kuimarisha utawala bora ili kuimarisha utendaji wa vyombo vyake.

Kauli hiyo ya SMZ, ilitolewa juzi na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, wakati akifunga kikao Baraza la Wawakilishi kilichokuwa kikijadili makadirio na mapato ya matumizi ya mwaka wa fedha wa 2007/2008 visiwani hapa.

“Utawala Bora una mwanzo, lakini hauna mwisho. Nakiri kuwa zipo kasoro za hapa na pale katika utekelezaji wa masuala ya utawala bora, Serikali itaendelea kuimarisha masuala ya utawala bora ili kuimarisha utendaji wa vyombo vyake,” alisema Nahodha.

Alisema kuwa tangu kuanzishwa Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Katiba na Utawala Bora, shughuli za utawala bora nchini zimeimarika na wajumbe wa Baraza wamethibitisha hilo kwa michango yao wanayoitoa katika vikao vya Baraza.

Alisema katika kuimarisha dhana ya utawala bora nchini, Tume ya Haki za Binadamu Tanzania, iliyokuwa imepigwa marufuku kufanya kazi zake visiwani hapa, sasa imeanza kufanya kazi zake tena.

Aliitaja pia Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuwa moja ya ofisi zinazofanya kazi kwa uhuru na kwamba kesi za jinai, sasa zinaendeshwa na ofisi hiyo badala ya Jeshi la Polisi.

Nahodha alisema jambo hilo ni muhimu katika kuimarisha upelelezi na uendeshaji wa kesi, sambamba na uchapishaji wa vitabu vya sheria za Zanzibar na ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.

Katika hotuba hiyo aliyoisoma kwa zaidi ya saa moja, alinukuu baadhi ya maneno ya marehemu Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere yaliyo katika kitabu chake cha ‘Uhuru na Maendeleo’ kama muongozo mzuri wa kuwa kiongozi bora.

Alisema Nyerere aliandika kwenye kitabu chake maneno ya hekima ambayo ni vema kuyafuata ili kiongozi aweze kutekeleza majukumu yake ya kazi kwa ufanisi.

Aliwaonya viongozi kuacha tabia ya kuwakemea na kuwatukana wanapowaelekeza au kuwaongoza katika kazi za kujitafutia maendeleo na badala yake watumie njia ya mijadala na kushauriana zaidi ili kujenga uhusiano mzuri na wapiga kura wao.

Kabla Nahodha hajasoma hotuba yake, mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Ramadhani Pandu, wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo alitaka serikali ieleze kwa nini wizara hiyo inatoa ajira kwa ubaguzi.

Alisema miaka kadhaa iliyopita, wizara hiyo iliwahi kuwabagua wafanyakazi sita kwa misingi ya imani za dini na kwamba hivi karibuni wizara hiyo iliajiri wafanyakazi wasio na sifa zinazostahili kwa nafasi walizoomba na kuwaacha wenye sifa hizo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kiongozi na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa SMZ, Ali Juma Shamuhuna, alisema hahusiki na yaliyofanyika nyuma katika wizara hiyo kwa vile hakuwepo katika uongozi wa wizara hiyo, bali waziri aliyekuwepo ameshafariki dunia.

Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, alilazimika kuingilia kati na kusema serikali ni ile ile tangu kupinduliwa 1964 na hakuna haja ya kukwepa hoja kwa kisingizio hicho, hivyo alimtaka Shamhuna kutumia lugha ya diplomasia zaidi kuzungumza na watendaji wake endapo kuna kasoro zirekebishwe. Aliyekuwa Waziri wa Habari wakati huo miaka 15 iliyopita ni Balozi Issa Mohammed, ambaye pia aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.