Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Kamati yaeleza kutoridhishwa kasi ujenzi daraja la Kigamboni
http://www.habaritanzania.com/articles/4082/1/Kamati-yaeleza-kutoridhishwa-kasi-ujenzi-daraja-la-Kigamboni
By Habari Tanzania
Published on 08/4/2007
 

KAMATI ya Maendeleo ya Jamii ya Bunge, imesema hairidhishwi na kasi ya serikali katika kushughulikia suala la ujenzi wa daraja la Kigamboni, ambao umeasisiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).


na Martin Malera na Rahel Chizoza, Dodoma


KAMATI ya Maendeleo ya Jamii ya Bunge, imesema hairidhishwi na kasi ya serikali katika kushughulikia suala la ujenzi wa daraja la Kigamboni, ambao umeasisiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Akiwasilisha maoni kuhusu hotuba ya makadirio ya Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, mjumbe wa kamati hiyo, Ezekiel Mahige, alisema pamoja na maandalizi ya kutosha yaliyokwishafanywa na NSSF kwa ajili ya mradi huo, kinachohiotajika hivi sasa ni serikali kuruhusu kuanza kwa utekelezaji wake kwa kuuingiza katika mipango yake ya utekelezaji ukiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005.

Kadhalika, kamati hiyo imependekeza mikopo inayotolewa kwa wajasiriamali ielekezwe katika vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS), ili kupunguza mzigo wa riba kwa wakopaji ambao ni wazalishaji wadogo.

Alisema kiwango cha riba ya asilimia 10 inayotozwa kwa SACCOS zinazopewa mikopo na benki ya CRDB, wakati benki ikilipa riba ndogo ya asilimia 2 tu si haki na kushauri riba hiyo kugawanywa kwa usawa wa kila upande kulipa asilimia 6.

Kuhusu mgogoro baina ya wafanyakazi na uongozi wa kiwanda cha sukari cha TPC Moshi, kamati hiyo imeishauri serikali kushughulikia suala hilo na kwamba hali ilivyo kwa sasa inaweza kuleta madhara makubwa na kurudisha nyuma kasi ya uwekezaji nchini.

Kamati pia imezungumzia mradi wa ujenzi wa jengo la wamachinga jijini Dar es Salaam na kushauri kufanyika kwa zoezi la kuwatambua mapema wafanyabiashara wadogo kisha kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali kabla ya kupewa nafasi za kufanya kazi zao katika jengo hilo.