BENDI ya muziki wa dansi ya The Afrika Ngoma, ambayo inafanya shughuli zake nchini Ujerumani imezidi kupanda chati na kuwashika raia wa nchi mbalimbali nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa Tanzania Daima na kiongozi wa bendi hiyo, Ebrahim Makunja ‘Ras Makunja Kichwa Ngumu’, katika shoo waliyoifanya Juni 2, mwaka huu, katika viwanja Altersorfer jijini Humburg, wakati wa Tamasha la Africa Market, bendi hiyo inayoundwa na wanamuziki kutoka nchi mbalimbali, iliwashika vilivyo maelfu ya mashabiki waliohudhuria.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bendi hiyo inayopiga muziki wa makabila mbalimbali ya Afrika, ilifanikiwa kuwapeleka puta mashabiki.
Baadhi ya wanamuziki waliocha gumzo kwenye tamasha hilo, ni Christian Bokotesa ambaye alitesa kwenye gitaa la solo, Maxime Vayituma aliyeng’ara kwenye drum, sambamba na kijana mdogo wa miaka 18, mwenye asili ya Kizungu, Lars Bernsmann, aliyekuwa akilicharaza gitaa la rhythm.
Kutokana na kung’ara katika onyesho hilo, bendi hiyo ilitangazwa kuwa bora kwa mara nyingine na kuufanya muziki wa Tanzania kuzidi kupendwa nchini humo.
Mmoja wa waandaaji wa tamasha hilo, Niger Asher, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Colour Music, alisema, haijawahi kutokea kwa muziki wa Afrika kuteka nyoyo za mashabiki, katika historia ya maonyesho ya muziki jijini Humburg.