JESHI la Polisi nchini limesema kuwa litakabiliana kwa nguvu zake zote na kuwakamata wale wote wanaojihusisha na wizi wa fedha kwenye ATM katika benki mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Sydney Mkumbi.
Alisema hivi sasa Jeshi la Polisi kwa kuwatumia makachero wake linatekeleza mpango mkakati wa kukabiliana na wale wote wanaojihusisha na mtandao huo, ili kunusuru uchumi wa nchi.
Aidha, alisema polisi inawashirikisha pia viongozi wa benki mbalimbali zinazotumia mfumo wa ulipaji fedha kwa njia ya ATM, ili kusaidia kuondoa uwezekano wa kutokea tena kwa wizi kama huo.
Alisema viongozi hao pia wametakiwa kudhibiti nyendo za wafanyakazi waliopo na hata waliowahi kufanya kazi katika mabenki hayo ambao walifukuzwa ama kuachishwa kwa makosa yasio ya uaminifu.
Mkumbi alisema kwa vile wezi hao wanazorotesha uchumi wa nchi, Jeshi la Polisi litahakikisha kuwa wale wote wanaojihusisha na wizi huo wanafahamika na kukamatwa, ili kuchukuliwa hatua kali za kisheria, iwe mfano kwa wengine wenye nia na mawazo ya kufanya vitendo hivyo.
Hivi karibuni, Jeshi la Polisi liliwatia nguvuni watu kadhaa wakiwemo raia wa kigeni kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa fedha katika moja ya ATM za benki jijini Dar es Salaam na wamefikishwa mahakamani.