Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  CHADEMA yalia na Karamagi
CHADEMA yalia na Karamagi
By Habari Tanzania | Published  08/4/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Lucy Ngowi


CHAMA cha Demekrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeungana na mbunge wake, Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), kushikilia bango suala la serikali kusaini mkataba mpya wa madini nje ya nchi kabla hata kumaliza kupitia upya mikataba ya madini yenye utata.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema hayo jana alipokuwa akitoa tamko la Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu hali ya taifa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya chama hicho, Dar es Salaam.

Alisema hali hiyo inathibitisha ukosefu wa dhamira ya kweli ya Serikali ya CCM kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali ambazo Mungu amewajalia na ni kinyume cha ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ambayo aliitoa wakati wa uzinduzi wa Bunge.

“Kwa kuwa serikali imeonyesha kiburi katika kuhakikisha kuwa mikataba inawekwa wazi hata kwa Bunge, Kamati Kuu inatoa mwito kwa vyama vya wanasheria na vikundi vya haki za binadamu kuchukua hatua zinazostahili,” alisema Mbowe.

Alisema Kamati Kuu inaitaka CHADEMA kushirikiana na vyama vya siasa kuendelea kuhamasisha nguvu ya umma katika kulinda na kutetea maslahi ya taifa.

“Hakuna jambo la kawaida katika suala hilo, tutaendelea kulishikia bango suala la Karamagi kwenda kusaini mkataba nje. Tutaendelea kulifumua suala hili kwa kuwa tuna taarifa za kina. Tunaitaka serikali ichukue hatua kama serikali itaminya hili, sisi tutalifumua,” alisema Mbowe.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, katika Bunge la bajeti linaloendelea pamedhihirika kuwa serikali haitaki upinzani kwa kuwa kuna ushuhuda wa kimazingira na hata kimatendo.

Mbowe alisema Kamati Kuu ya CHADEMA inaona kuwa Bunge la Tanzania linaelekea kupoteza uhalali wake wa kuwa chombo kinachowakilisha umma wote wa Tanzania, kwa kuwa limejigeuza kuwa chombo cha chama kimoja cha CCM kwa vitendo vyake.

“Wabunge wa CCM wanaingiza ushabiki wa kisiasa katika mambo yenye maslahi kwa taifa kwa ujumla wake. Ni mkakati wa serikali kuufifisha na kuunyong’onyeza upinzani,” alisema Mbowe.

Aliwataka wananchi wasimame kidete kuhakikisha wawakilishi wao wanatanguliza mbele maslahi ya raia na si maslahi ya vyama vyao na kama wanapingana na matakwa ya umma, basi wawanyime kura katika chaguzi zijazo.

Alitumia fursa hiyo kwa kusema Kamati Kuu ya CHADEMA inaipongeza kambi ya upinzani bungeni kwa kuwasilisha bajeti mbadala, kwa kuwa ilipendekeza hoja nzito kuhusu vyanzo mbadala vya mapato na kupunguza matumizi ya serikali.

“Tunalaani utamaduni wa mawaziri na wabunge wa CCM kuweka mbele ushabiki wa kisiasa, ambao kimsingi hausaidii taifa letu wala wananchi wetu,” alisema.

Mbowe alisema kuwa Kamati Kuu inamtaka Rais Kikwete amwajibishe Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji kwa kuwa anachezea maisha ya Watanzania.

Alisema Meghji alilidanganya Bunge kwa kuwa serikali imeshindwa kudhibiti hali ya mfumo wa soko holela na inaelekea kuongoza kwa majaribio.

Akizungumzia elimu ya juu, Mbowe alisema wapo wanafunzi ambao wameshindwa kuchangia asilimia 40 ya masomo yao na hatimaye wamezuiliwa kufanya mitihani katika vyuo vya Tumaini Iringa, Ustawi wa Jamii, St. Augustine Mwanza na vingine.

Aliishauri serikali kutoa utaratibu wenye kuwawezesha wanafunzi hawa kufanya mitihani yao kama ambavyo ilifanyika kwa Chuo cha Kilimo Morogoro (SUA) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Awali, Mbowe alisema kuwa taifa limezidiwa na mzigo wa ufisadi kwani orodha ya ufisadi, matumizi makubwa na matumizi yasiyo na lazima ni ndefu, wakati nchi inateketea watawala wananeemeka.

“CHADEMA inalaani hali hii na kufadhaishwa na ukimya ama ucheleweshaji wa Rais Kikwete. Rais ameonekana kuwa na kigugumizi kikubwa kuhusiana na ufisadi.

“Madhila yanayolikumba taifa rais anastahili lawama asilimia 100. Kama anawalea wasaidizi wake na kukaa kimya, anachangia ufisadi,” alisema Mbowe.

Alimalizia kwa kusema kuwa hali ya taifa letu hairidhishi na hivyo jitihada za kila mwananchi zinahitajika katika kuhakikisha uwajibikaji wa viongozi na raia katika kulirejesha taifa letu katika mwelekeo mwafaka wa demokrasia na maendeleo.

Katika hali ya kujiamini mwenyekiti huyo wa CHADEMA alimtahadharisha Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba kuwa yuko mbioni kuanza kuwafuata wananchi kwa kutumia helikopta yake.

Alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na waandishi wa habari ni kwanini kila anapokwenda katibu huyo anafuata.

“Namwambia Makamba ajitayarishe kwani karibu nitaanza kuruka na helikopta yangu sijui yeye atafanyaje. Safari hii Makamba atanifuatilia, lakini hatanipata, mufilisi kabisa,” alisema.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.