Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Uraia wa nchi mbili karibuni
Uraia wa nchi mbili karibuni
By Habari Tanzania | Published  08/2/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Martin Malera, Dodoma


SUALA nyeti linalohusu uraia wa nchi mbili sasa lipo mikononi mwa Baraza la Mawaziri na linatarajiwa kulitolea maamuzi katika siku chache zijazo, Bunge lilielezwa jana.

Sambamba na hilo, serikali ilieleza pia kuwa kuanzia sasa, mahabusu watakaogoma kwenda mahakamani, watahukumiwa kwanza papo hapo kwa kosa hilo na kubadilika kuwa wafungwa wakati kesi za awali zikiendelea.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Mungai, alisema hayo jana bungeni wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2007/08.

Alisema suala la kuwa na uraia wa nchi mbili, hivi sasa liko katika ngazi ya Baraza la Mawaziri kwa kujadiliwa na hivi karibuni hatima ya suala hilo itajulikana.

Hata hivyo, wakati akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Kigoma Kusini, Manju Msambya (CCM), alipinga kuanzishwa kwa utaratibu wa uraia wa nchi mbili kwa madai kuwa hali hiyo itaifanya nchi kuwa kokoro.

Akizungumzia migomo ya mahabusu, Mungai alisema mahabusu kugoma kwenda mahakamani ni kosa la jinai na kwamba wahusika wameshafahamishwa kuwa mahabusu atakayegoma, atahukumiwa papo hapo.

Kuhusu msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani, alisema tatizo hilo bado lipo ingawa limepungua kiasi.

Alisema hali hiyo inasababishwa na baadhi ya sheria zinazotoa adhabu kali za kifungo cha muda mrefu kama vile miaka 30 kwa makosa ya kujamiiana.

Ili kupunguza hali hiyo magerezani, Mungai alisema wizara yake imedhamiria kujenga mabweni mapya na kukamilisha ujenzi wa viporo.

“Katika jitihada hizo tunaweza kuongeza nafasi za kuhifadhi wafungwa na mahabusu kutoka 22,699 hadi kufikia 27,653,” alisema Waziri Mungai.

Alitaja njia nyingine ya kupunguza msongamano wa magerezani kuwa ni kupitia utekelezaji wa Sheria ya Bodi ya Parole namba 25/1994 iliyofanyiwa marekebisho kwa sheria namba 5 ya mwaka 2005.

“Tatizo lililopo ni ufinyu wa wigo uliopo unaoruhusu wafungwa kuachiwa kwa parole kwa mujibu wa sheria iliyopo. Hata hivyo Januari mwaka huu, nilikutana na Bodi ya Taifa ya Parole ili kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais la kuimarisha mfumo wa parole nchini ili wafungwa wengi zaidi waweze kufaidika na utaratibu huo.

“Natarajia mwaka huu kuliomba Bunge lifanyie marekebisho ya sheria husika ili kuongeza wigo wa parole,” alisema.

Kwa mujibu wa Waziri Mungai, hatua nyingine ya kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani ni kupitia msamaha wa Rais ambapo mwaka huu pekee, ameshasamehe wafungwa 8,686.

Akizungumzia mradi wa vitambulisho vya uraia, alisema hivi sasa wizara yake imeanza kutekeleza mradi huo kwa kununua jengo kwa ajili ya ofisi anzilishi ya mradi pamoja na kuendelea na mchakato wa kuundwa kwa wakala itakayosimamia kuendesha kazi ya utoaji wa vitambulisho vya kitaifa.

Kuhusu kuimarisha kitengo cha Zimamoto, Waziri Mungai alisema sheria mpya ya Zimamoto ambayo tayari imeshatiwa saini na Rais, itaanza kutumika mwaka huu na hatua kadhaa zitachukuliwa kuunda jeshi la zimamoto na uokoaji wa kisasa.

Alitaja juhudi nyingine zinazofanywa kuimarisha kikosi hicho kuwa ni pamoja na kukipatia magari ya zimamoto baadhi ya mikoa nchini wakati katika Mkoa wa Dar es Salaam, wizara ina mpango wa kujenga jengo jipya la makao makuu ya Zimamoto.

Kuhusu Idara ya Uhamiaji, Waziri Mungai alisema imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kudhibiti uingiaji haramu nchini katika kipindi cha Julai hadi Aprili mwaka huu, wageni 531,834 waliingia nchini kihalali.

Alisema kati ya Julai 2006 hadi Aprili 2007, wageni haramu 1,876 walikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pia alisema idara hiyo kuanzia Julai 2006 hadi Aprili 2007 imetoa pasipoti 52,345 za kawaida, 1,675 za Afrika Mashariki, 273 za kibalozi na 88 za watumishi.

Pia alizungumzia ufanisi wa kuwarejesha wakimbizi makwao ambapo hadi sasa kambi tano za wakimbizi nchini, zimefungwa kutokana na idadi yao kupungua.

Ili kutekeleza shughuli zake za maendeleo katika kipindi cha mwaka huu wa fedha, Mungai aliomba Bunge kuidhinisha sh 94,712,920,000.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.