Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  CCM yakana maamuzi
CCM yakana maamuzi
By Habari Tanzania | Published  07/31/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Martin Malera, Dodoma


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekanusha taarifa zilizoandikwa jana katika magazeti kadhaa nchini (si Tanzania Daima), kuhusu kusimamishwa kwa uongozi wa vigogo kadhaa wa chama hicho kutokana na tuhuma mbalimbali za ubadhirifu wa fedha.

Taarifa ya maandishi iliyotolewa na chama hicho kwa waandishi wa habari jana ilisema taarifa hizo zilizoripotiwa katika magazeti ya Mwananchi, Habari Leo na Majira hazikuwa na ukweli wowote.

Pasipo kutoa ufafanuzi kuhusu ukweli wa habari hizo, CCM ilivitaka vyombo vya habari kuwa na subira kuhusu maamuzi ya vikao vya chama hicho ambavyo vilitanguliwa na kikao cha siku tatu cha Kamati Kuu ya CCM kilichokuwa kikitarajiwa kumalizika jana, kabla ya kuanza kwa Halmashauri Kuu ya Taifa leo.

Katika magazeti kadhaa ya jana kulikuwa na habari ambayo iliwataja kwa majina viongozi wakuu wawili wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania na Katibu wa CCM wa mkoa kuwa watu waliosimamishwa uongozi wakituhumiwa kuhusika na ukiukwaji wa misingi ya uongozi ndani ya chama hicho.

Habari kuhusu kusimamishwa kwa viongozi hao, zilianza kusambaa juzi alasiri na hadi kufikia jioni ya siku hiyo, wajumbe kadhaa wa Kamati Kuu ya CCM, waliozungumza na Tanzania Daima pasipo majina yao kutajwa, walikanusha kufikiwa kwa maamuzi hayo.

Mmoja wa wajumbe hao, alilieleza gazeti hili kuwa, uamuzi wa kusimamishwa kwa viongozi hao, ulikuwa ukitarajiwa kufikiwa kutokana na kuwapo kwa pendekezo la Kamati ya Maadili iliyochunguza tuhuma mbalimbali dhidi yao.

Mjumbe mwingine wa Kamati Kuu hiyo aliyezungumza na Tanzania Daima alisema hadi kufikia hiyo juzi jioni, bado hatima ya wanasiasa hao ilikuwa haijajulikana rasmi.

“Subirini habari za kweli zitolewe na wanaohusika kwa utaratibu uliowekwa na chama na ambao vyombo vya habari vinaufahamu kwani vimekuwa vikiwasiliana na CCM mara kwa mara kupitia utaratibu huu.

“Mathalani, habari zilizoandikwa na Majira leo (jana), Julai 30 kuwa Kamati Kuu imemkemea Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, kwa kutumia lugha nzito katika mazungumzo ya mwafaka wa CCM na CUF si za kweli.

“Aidha, taarifa za magazeti ya Mwananchi, HabariLeo…ya leo (jana) Julai 30, si sahihi. Nasisitiza umuhimu wa kupata habari sahihi na zilizothibitishwa kutoka kwa wahusika sahihi. Si vema kwa chombo cha habari kuokoteza taarifa ilhali wasomaji wanakitegemea katika kupata habari sahihi,” alisema Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Aggrey Mwanri, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.

Mbali ya hilo, kikao cha Kamati Kuu ya CCM jana kiliendelea kwa siku ya tatu mfululizo kuteua majina ya wagombea wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho, kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na taifa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana ya Mwanri, ilisema miongoni mwa ajenda za mkutano huo ni taarifa ya maandalizi ya mkutano mkuu wa nane wa chama hicho, utakaofanyika Novemba mwaka huu.

Mwanri alisema katika taarifa hiyo kuwa, pamoja na ajenda ya hali ya kisiasa nchini, NEC itashughulikia uteuzi wa wagombea uongozi wa CCM wa ngazi zote za uongozi.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwapo kwa mvutano mkubwa miongoni mwa wagombea nafasi mbalimbali za uongozi katika baaadhi ya mikoa.

Vyanzo vyetu vya habari kutoka ndani ya NEC vinataja mikoa iliyoipasua kichwa CC ni Mbeya, Mara, Iringa na Shinyanga.

Kwa mujibu wa habari hizo, CC imelazimika kutumia muda wa siku tatu ili kuhakikisha haifanyi makosa katika kupitisha majina matatu matatu katika kila nafasi ya uongozi inayowaniwa.

“CC inajua kwamba ikifanya makosa katika uteuzi huo, mkutano wa NEC unaweza usimalizike. Tuko hapa kuhakikisha mambo yote yanaenda sawa,” alisema mmoja wa wapambe wa wawania nafasi hizo ambaye pia ni mjumbe wa NEC.

Mchujo wa wagombea wote zaidi ya 5,000, ulitarajiwa kukamilika jana jioni kabla ya leo kufikishwa mbele ya wajumbe wa NEC ambao baadhi yao wapo Dodoma kwa zaidi ya wiki moja sasa.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima, ulibaini kuwa wagombea, wajumbe wa NEC na wapambe wao wamekuwa na mikutano katika kambi tofauti kwa siri kwa ajili ya kufuatilia mwenendo mzima wa uchaguzi huo wenye ushindani mkubwa.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.