SAUTI ya Tanzania Zanzibar (STZ) imelaumiwa kwa kukataa kutoa tangazo kuwataarifu wananchi wa Kijiji cha Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja juu ya ujio wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma, kijijini kwao Kidombo.
Wakizungumza kwa jazba katika shamrashamra za kumlaki kiongozi huyo, wananchi hao walisikika wakiilaumu STZ kwa kukataa kutoa tangazo hilo, licha ya wao kuwa tayari kulilipia.
Wananchi hao walisema, waliamua kutayarisha tangazo hilo ili kuwapa taarifa wananchi wengi zaidi kujitokeza kumlaki kiongozi huyo wakati atakapowasili kijijini kwao, ambako alizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.
Ofisa mmoja wa kituo cha STZ, alikiri kuwaona baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wakiwa na tangazo hilo kituoni hapo, lakini hakufahamu mambo yaliyoendelea na kusababisha lisitolewe redioni.
“Tumesikitishwa kwa kweli na kitendo cha redio kukataa kutangaza tangazo letu, lakini tunawaambia sisi hata kama hawajatangaza, tumekuja kumpokea Dk. Salmin,” alisema mmoja wa akina mama waliokuwa wamejipanga kumlaki kiongozi huyo.
Akihutubia umati mkubwa wa wananchi, Dk. Salmin aliwashukuru kwa kujitokeza kwa wingi kwenda kumsalimia, lakini pia aliwapongeza kwa kuonyesha mapenzi ya dhati kwake.
Alisema: “Leo si siku ya mazungumzo marefu… leo ni siku ya kusalimiana na nishukuru Mungu mie sijambo na nyie hamjambo? Wazima?”
Aidha, Dk. Salmin aliwashukuru wananchi wa Jamhuri ya China kwa ushirikiano wao kwake na kubainisha kuwa, China ni rafiki wa kweli wa Tanzania. Kiongozi huyo alirejea kutoka nchi hiyo hivi karibuni baada ya kupata matibabu ya macho kwa miezi takriban minane.
Awali, wazee wa Mkwajuni walimwambia Dk. Salmin kupitia risala yao iliyosomwa na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Maulid Nafasi Juma, kujisikia yupo nyumbani kwani wazee wa kijiji hicho wamefarijika sana na kurejea kwake akiwa mzima wa afya.
Akimkaribisha Dk. Salmin kuhutubia mkutano huo wa kwanza wa aina yake tangu aliporejea kutoka katika matibabu, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini A, Haji wa Haji, alimshukuru kiongozi huyo kwa kwenda kuwasalimia kwani kuna wazee wengine wasingeliweza kufika mjini kutokana na sababu mbalimbali.
Katika mkutano huo, Dk. Salmin alilakiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Riziki Omar, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kakazini Unguja, Fum Mati na baadhi ya viongozi wengine wa Jimbo la Mkwajuni na wengine kutoka maskani kaka ya Kisonge.
Kiongozi huyo maarufu kwa jina la Komandoo, alilakiwa kijijini hapo kwa dufu iliyoambatana na kaswida huku wakereketwa na wananchi mbalimbali wakiwa wamejipamba kwa sare za CCM.