RAIS Jakaya Kikwete ameunga mkono pendekezo la kuondoa mfumo wa viti maalum kwa wabunge ili kuwafanya wanawake wagombee nafasi hizo kupitia majimbo.
Akifungua Mkutano Maalum wa Umoja wa Wananwake Tanzania (UWT) jana, kwenye Ukumbi wa Kilimani mjini hapa, alisema kuwepo kwa viti maalum bungeni kunawapunguzia nguvu wanawake.
Alisema kwa kuwa kwao wabunge wa viti maalum, kunawafanya washindwe kuchangia hoja za msingi wakati inapozuka mijadala mizito baina ya wabunge bungeni.
“Huwezi kuwa na nguvu ya kuchangia mjadala bungeni kama mbunge mwenye jimbo. Kwa vyovyote vile ukiongea watasema unaongea kwa ajili ya nani, lakini wenye majimbo wakisema wanasema kwa niaba ya wananchi wa jimbo fulani,” alisema.
Alisema kuwepo kwa asilimia 50 kwa 50 katika nafasi za ubunge baina ya wanawake na wanaume, kutawaongezea nguvu wanawake katika kutoa michango yao na kuonyesha uwezo wao katika uongozi, iwapo watapatikana kupitia katika majimbo.
Kikwete alisema wazo hilo la kuwa na asilimia 50 kwa 50 na kuondoa viti maalum, bado linafanyiwa kazi na majibu yakitolewa utekelezaji utaanza bila kuchelewa ili kuleta usawa.
Alisema nia ya kulifanyia kazi suala hilo ni kutaka kuleta usawa kwani maslahi ya mbunge wa jimbo na yule wa viti maalum hayalingani.
Kikwete alisema kuwa UWT inalo jukumu la kuhakikisha mfumo huo utakapoanza utawawezesha wanawake wengi kuingia katika kinyang’anyiro na kushinda. Alisema ubunge wa jimbo utawapa nguvu wabunge wanawake kutetea maslahi ya wanawake kwa nguvu zote bila kuogopa.
Aidha, aliipongeza UWT kwa kufanya jitihada mbalimbali za kimaendeleo, ambazo zimewawezesha wanawake wa Tanzania kushika nyadhifa mbalimbali kubwa, ndani na nje ya nchi, ikiwemo katika mashirika ya dini.
Alisema mtazamo potofu juu ya uwezo, kasi na wajibu wa mwanamke katika utendaji kazi, ni kikwazo, ambapo huchochewa na mila na desturi zilizopitwa na wakati za kuona wanawake walio mstari wa mbele katika mambo ya siasa ni ‘vimbelembele.’
Hata hivyo, Rais Kikwete alionyesha kusikitishwa kwake na tabia ya wanawake kutopendana na wamekuwa wakiwekeana vigingi ambavyo hukwamisha maendeleo yao na kuwafanya washindwe kupambana na umasikini unaowakabili katika maeneo yao.
“Adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe, msifikiri kuwa maadui ni wanaume, wapo wanawake wasiopenda wenzao wapate ambapo huwafanyia hiana kwa madai kuwa watawapita kimaendeleo,” alisisitiza.
Rais Kikwete alisema mambo hayo yamepunguza kasi ya maendeleo nchini miongoni mwa wanawake, ambapo aliwataka kuachana na dhana hiyo potofu ambayo ni hasidi kwa maendeleo ya wanawake nchini.
Alisema kasumba hizo zinazokwamisha maendeleo zinapewa nguvu na mtazamo duni wa kuwa wanawake ni raia wa daraja la pili na kuwa wao ni tegemezi na wapo katika daraja la chini.
“Nguvu ya mnyonge ni umoja, umoja wenu huu wa UWT ni muhimu sana nchini katika kuwatetea na kusaidia kuondoa mfumo dume katika jamii,” alisema.
Alisema mfumo dume pia ni kikwazo cha maendeleo ya wanawake kwani wanawake wengi wamekuwa wakizalisha, lakini wanaonufaika na uzalishaji huo ni wanaume ambao ndiyo hupenda kufanya kazi ya kuingia sokoni baada ya wenzao kuzalisha.
Alibainisha kuwa zipo sheria zenye mapungufu ambazo husababisha wanawake waendelee kunyanyaswa ambazo hivi sasa serikali inazifanyia marekebisho ili ziendane na wakati wa sasa.
Alizitaja sheria hizo kuwa ni Sheria ya Watoto, Sheria ya Ndoa na Sheria ya Mirathi ambapo ameitaka UWT kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuziboresha.
Aidha, alionyesha hofu yake kuhusu kuwaruhusu wanafunzi wanaojifungua kuendelea na masomo, ambapo alisema ruhusa hiyo inaweza kuongeza idadi ya mimba shuleni.
“Kuwaruhusu wanafunzi wa kike kuendelea na masomo baada ya kujifungua kutasababisha nusu ya wanafunzi darasani maziwa yawe yanavuja kutoka na watoto wao kulia nyumbani.
“Siukatai utaratibu huo, ongeeni muone ni njia gani nzuri ya kuwafanyia watoto hawa, lakini kuweni makini katika kuamua,” alisema.
Aliwataka wazazi kukaa na kuongea na watoto wao ili kuwajulisha madhara yaa kupata mimba wakiwa wadogo na kuwafundisha kusema hapana, kwani wakikwepa mimba wanaweza kupata ukimwi ambao ni hatari zaidi.
Alisema kwa upande wake, serikali haitakaa kimya, itaendelea kupiga vita swala hilo na kuwachukulia hatua wanaume mabazazi wanaowazalisha wanafunzi na kuwakatisha masomo.
Aliwaasa wajumbe hao wa mkutano maalum wa wanawake kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa haki na usawa na si viongozi ambao huangalia maslahi yao kwanza.
Aliwataka kutosikiliza mawazo ya mgombea yeyote anayesema kuwa amechaguliwa na viongozi wa ngazi ya juu, kwani mwenye haki ya kuchagua kiongozi ni atakayeongozwa na kiongozi huyo.
Alisema wasikubali kuchaguliwa viongozi na baadaye wakaanza kujilaumu kwamba wangejua wasingefanya hivyo wakati uchaguzi unakuwa umepita na hauwezi kurudiwa tena mpaka muda wake utakapofika.