WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania akidai fidia ya shilingi bilioni 20 kwa madai ya kuchafuliwa jina lake.
Sumaye ambaye amerejea hivi karibuni kutoka masomoni katika chuo kikuu maarufu duniani cha Harvard, nchini Marekani, anadai fidia hiyo kutoka kwa gazeti la Tanzania Leo kwa madai ya kuandika habari za kashfa dhidi yake.
Uamuzi huo wa Sumaye ambao umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu baada ya yeye mwenyewe mara kadhaa kuahidi kufanya hivyo, umekuja kutokana na habari iliyoandikwa katika gazeti hilo, ikidai mwanasiasa huyo alikuwa na ukwasi unaokadiriwa kufikia sh trilioni 10, alizokuwa ameziweka katika akaunti yake iliyopo nje ya nchi.
Kesi hiyo ambayo huenda ikavuta hisia za watu, ilitajwa kwa mara ya kwanza jana mbele ya Jaji Robert Makaramba wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Katika kesi hiyo, Sumaye anamshitaki mwandishi wa habari hizo, mhariri, mmiliki na mchapishaji wa gazeti hilo, ambalo kwa muda mrefu sasa limekuwa halionekani mitaani.
Mbali ya mwandishi wa habari hizo ambaye hati ya mashitaka haimtaji, wengine wanaotajwa kushitakiwa ni, Benedict Sichalwe (Mhariri) na Hamis Yowa (Mchapishaji) ambaye pia ametambulishwa kama mmiliki wa gazeti hilo.
Hata hivyo, wakili wa Sumaye, Deusdedith Duncan, alidai mahakamani hapo kuwa, hadi hiyo jana wakati kesi ikitajwa, ni mchapishaji wa gazeti hilo pekee ambaye alikuwa amepewa hati ya mashitaka, huku washitakiwa wengine wakiwa bado hawajapatikana.
Kutokana na hali hiyo, Duncan aliiomba mahakama kuwapatia washitakiwa hao hati ya mashitaka kupitia katika machapisho na matangazo ya vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Katika kesi hiyo, Sumaye anadai kukashifiwa na gazeti hilo katika machapisho yake mawili tofauti, la kwanza likiwa ni toleo namba 340 la Machi na la pili likiwa ni toleo la Aprili yote ya mwaka jana.
Alidai kuwa toleo hilo la Machi mwaka jana, lilikuwa na habari iliyobeba kichwa cha habari kisemacho; “Sumaye aonja shubiri ya ari na kasi mpya.”
Sumaye anadai pia kuwa, toleo hilo liliendelea kumshutumu kwa kusema alikuwa amewekeza fedha nyingi katika benki moja ya nje, na kwamba anao utajiri wa fedha kama za aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mobutu Seseseko.
Habari hiyo iliyobeba uzito wa kwanza kwa siku hiyo na kuwa gumzo nchini, iliendelea kudai kuwa, Sumaye anamiliki akaunti yenye thamani ya sh trilioni 10, fedha ambazo zinaweza kuiendesha nchi kwa miaka mitatu.
Mbali ya hiyo, habari nyingine ambayo Sumaye ameilalamikia mahakamani ni ile iliyokuwa katika toleo namba 341 iliyokuwa na kichwa cha habari; “Pesa za Sumaye zilizo nchini zafahamika.”
Katika habari hiyo, ilielezwa kuwa, Sumaye alikuwa amejiwekea fedha zinazofikia shilingi bilioni moja katika akaunti mbalimbali hapa nchini.
Kwenye malalamiko yake, Sumaye anadai pia kuwa, habari hizo si sahihi, kwani ni za uongo na uzushi mtupu na kwamba, mbali ya kumchafulia jina, pia zimemdhalilisha na kumshushia heshima na hadhi yake na kumfanya awe mtu asiyeaminika nchini.
Mbali ya hilo, Sumaye analalamikia kitendo cha yeye kufananishwa na marehemu Mobutu, ambaye alidai kuwa mwanasiasa gaidi, mla rushwa, kiongozi dikteta kwa wananchi na mtu ambaye hapaswi kufananishwa naye kwa namna yoyote.
Mbali ya kumshushia heshima na hadhi yake kama Waziri Mkuu mstaafu, Sumaye anadai pia kuwa, habari hizo zimemsababishia matatizo ya kisaikolojia na kumfanya atengwe na familia yake pamoja na marafiki wa karib, hata viongozi wa nchi.
Mbali ya kudai fidia ya sh bilioni 20, Sumaye aliiomba mahakama kutoa amri ya kulitaka gazeti hilo kuandika habari ya kukanusha kwa uzito kama huo kwamba taarifa hizo ni za uongo.
Sumaye mbali ya kuwa waziri mkuu wa kwanza katika historia ya nchi kushika wadhifa huo kwa kipindi kirefu cha miaka 10 mfululizo, pia amewahi kuwa mbunge wa Hanang.
Mwanasiasa huyo ambaye kitaaluma ni mtaalam wa masuala ya mifugo na sasa uongozi, amewahi pia kuwa, Naibu Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo kabla ya kuwa waziri kamili akiongoza wizara hiyo hiyo hadi alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1995.
Mwaka 2005, Sumaye alikuwa mmoja wa wagombea 11 wa kiti cha urais ndani ya CCM, lakini alienguliwa na Kamati Kuu ya CCM kabla ya jina lake kufikishwa kwenye mkutano mkuu wa chama hicho tawala na hatimaye Jakaya Kikwete kuibuka na ushindi mnono.
Baada ya uchaguzi, Sumaye alikwenda nchini Marekani kusomea shahada ya uzamili katika masuala ya uongozi na akarejea nchini hivi karibuni baada ya kuhitimu kwa mafanikio masomo yake.
Ikiwa ni takriban miaka miwili sasa tangu aondoke madarakani, Sumaye ameshasema mara kadhaa kwamba, ataendelea kuwa mwanasiasa na mwanachama mwadilifu wa chama hicho.
Hivi karibuni, alichukua fomu ya kugombea moja ya nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na jina lake limekuwa likihusishwa na dhamira ya kusaka moja ya nafasi za juu ndani ya chama chake.
Uamuzi wake wa kwenda kusoma Marekani, tena masuala ya uongozi umekuwa moja ya mambo yanayozua maneno mengi ya chini chini yakimhusisha na kutaka kusaka uongozi kitaifa miaka ijayo, minong’ono ambayo yeye mwenyewe ameikanusha mara kadhaa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 17, mwaka huu.