Habari za hivi karibuni zinaeleza kuwa, licha ya juhudi za kumaliza migogoro hiyo, mtu mmoja aliuawa hivi karibuni kutokana na mapigano ya koo mbili.
Habari hizo zinaeleza kuwa, mkazi wa Kijiji cha Ng’ereng’ere, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, aliuawa kwa kuchomwa mshale katika mapigano yaliyosababishwa na mgogoro wa kugombea ardhi baina ya wananchi wa koo za Wakira na Wanchari.
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Sirari, Anthony Manga, mwanakijiji huyo, Isack Joseph (25), aliuawa kwa kuchomwa mshale juzi jioni na mtu ambaye hajafahamika wakati yeye na wenzake kadhaa walipokuwa wakilinda mashamba yao kijijini hapo.
Diwani huyo wa Kata ya Sirari wanakoishi wananchi wa koo ya Wakira, aliiambia Tanzania Daima jana asubuhi kuwa, tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Stanley Kolimba, kuondoka kijijini hapo alikokuwa amekwenda kuhimiza usalama na amani kufuatia mgogoro huo.
Aidha, Manga alisema kwamba jana asubuhi, mikusanyiko ya watu waliokuwa na upinde, mishale, mikuki, panga na sime kutoka koo za Wakira na Wanchari, walionekana wakizunguka jirani na eneo la Nyabichune linalogombewa na koo hizo.
Wakati hayo yakitokea, serikali mkoani Mara imeanza kuandaa utaratibu wa kuharakisha zoezi la kuweka mpaka utakaozitenganisha koo hizo za kabila la Wakurya.
Hatua hiyo imefikiwa kufuatia kitendo cha Wakira na Wanchari kujaribu kupigana siku za Jumanne na Jumatano wiki hii bila mafanikio, baada ya askari polisi kuletwa mapema jirani na eneo la Nyabichune linagombewa na koo hizo.
Akizungumza na Tanzania Daima ofisini kwake juzi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, David Saibul, alisema kuwa Kolimba alikwenda kuweka mikakati ya kuimarisha usalama na amani katika vijiji vya Ng’ereng’ere na Remagwe wanakoishi Wakira na Korotambe wanakoishi Wanchari.
Saibul alisema mkuu huyo wa wilaya alizungumza na viongozi wa kata na vijiji husika juu ya usalama na amani na kuweka mikakati ya kuwabaini na kuwashughulikia kisheria watu wanaochochea mapigano baina ya koo hizo.
“Hivi sasa uongozi wa mkoa unakutana na viongozi mbalimbali wa serikali kwa ajili ya kuandaa utaratibu wa kuweka mpaka wa kuzitenganisha koo hizo haraka iwezekanavyo,” alisema Kamanda Saibul.
Serikali inaamini hatua hiyo itakomesha mgogoro huo ambao umekuwa ukizusha mapigano ya mara kwa mara baina ya wananchi hao na kusababisha mauaji ya watu, majeruhi, ulemavu, uharibifu wa mali mbalimbali na ukwamishaji wa shughuli za maendeleo.
Awali, serikali ilizuia uendeshaji wa shughuli yoyote katika eneo la Nyabichune hadi hapo litakapopangiwa matumizi ya shughuli za umma au kuwekwa mpaka wa kugawa eneo la Wanchari na Wakira.
Mwezi Novemba mwaka jana, Lowassa aliongoza kikao cha maofisa wa ngazi za juu serikalini na mkoani humo, kupanga mikakati ya kukomesha mapigano hayo.
Moja kati ya mambo yaliyoafikiwa katika kikao hicho ni kuwa ulinzi wa polisi utaongezwa na kuimarishwa katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara ili kumaliza moja kwa moja mapigano ya koo wilayani humo, yanayochochewa na kugombea ardhi na kuibiana ng’ombe.
Lowassa alisema pia kwamba, wataalamu wa ardhi watapelekwa katika wilaya hiyo kushirikiana na mabaraza ya ardhi ili kuweka sawa mipaka, kumaliza ugomvi wa ardhi ambao pia husababisha mapigano hayo.
Waziri Mkuu alitoa maelekezo hayo akihutubia ‘kongamano la amani’ la siku moja lililowashirikisha viongozi wa kijadi, kidini, vijiji, kata, tarafa na wilaya kupata ufumbuzi wa mapigano hayo.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu alifuatana na Waziri wa Nchi katika ofisi yake anayesimamia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mizengo Pinda; Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu; Waziri wa Utawala Bora, Philip Marmo; Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Saidi Mwema. Wote walipata nafasi ya kuzungumza.
Waziri Mkuu alisema: “Mapigano sasa basi. Serikali haiwezi kuvumilia jambo hili kwa maelezo yoyote yale. Serikali sasa itasimamia sheria na kutimiza wajibu wake na ninyi mtimize wajibu wenu.”
Aliwataka wazee wa kijadi ambao alisema wakitaka wanaweza kumaliza mapigano hayo na viongozi wa kidini washirikiane na serikali katika kuhakikisha mapigano hayo yanakoma moja kwa moja.
Waziri Lowassa alitoa maelekezo mengine kadhaa kwa wilaya hiyo kukabiliana na mapigano hayo ambayo alisema si jambo la kulifanyia mzaha. Miongoni mwa maelekezo hayo, ni pamoja na kupiga marufuku kilimo cha bangi na kuwasaka walimaji, wavutaji na watetezi wa bangi.
Maelekezo mengine ni kutoa mafunzo ya maboresho kwa viongozi wa serikali za mitaa; kuchanganya wanafunzi kutoka makabila mbalimbali shuleni na kujenga barabara katika maeneo ambayo sasa hayafikiki.
Hata hivyo, alisema endapo wilayani Tarime kuna tatizo la ardhi, basi wananchi wake wana uhuru wa kuhamia katika maeneo mengine kama wanavyofanya wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao wanahamia katika maeneo ya Tanga na Morogoro.
Akifafanua kuhusu kuongezwa kwa ulinzi wilayani humo, Mwema alisema askari watakaoongezwa ni kwenye maeneo ya intelijensia, uzuiaji wizi wa ng’ombe na kuzuia ghasia.
Jumla ya watu 29 waliuawa na wengine 13 kujeruhiwa kati ya mwaka 2001 hadi wakati huo kutokana na mapigano hayo. Nyumba zaidi ya 700 na vihenge vya nafaka 149 vilichomwa moto na mashamba yenye mazao yalifyekwa.