KAMATI ya Bunge ya Fedha na Uchumi, imepitisha mahesabu ya fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwaka 2005/06, baada ya Gavana wake, Daudi Balali, kutoa majibu yaliyoiridhisha kamati hiyo.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Handeni, Dk. Abdallah Kigoda (CCM), imepitisha mahesabu hayo baada ya kumhoji Balali na kisha kuichambua kwa kina Ripoti ya Matumizi ya Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) kwa mwaka huo.
Katika kuchambua ripoti hiyo, kamati hiyo ilihoji kuhusu mahesabu ya madai ya malimbikizo ya malipo ya nje, yanayofikia sh 131,725,294,000.
Akijibu madai hayo, Balali alisema nyaraka halisi za fedha hizo ziko benki ya NBC na kwamba ni halali, ila wanachosubiri ni uchunguzi kutoka IMF.
Kamati pia ilihoji malipo makubwa ya ada ya huduma iliyolipwa kwa Kampuni ya Mkono and Co. Advocates, ambayo malipo yake ya ada yalifikia sh 2,990,221,907 kwa kuendesha kesi moja.
Pia katika ripoti yake, CAG alitaka suala hilo lichunguzwe na kueleza kuwa malipo kwa kampuni hiyo ya uwakili ni asilimia 13.5 ya fedha ambazo serikali inadaiwa ambazo ni sh bilioni 60.
Akijibu suala hilo, Balali alisema kesi hiyo ni ya muda mrefu, ndiyo sababu fedha zilizolipwa kwa kampuni hiyo zimefikia kiwango hicho, na kwamba utafiti juu ya suala hilo, ulikuwa unafanyika nchini Ireland. Kesi hiyo itatolewa uamuzi Agosti 2, mwaka huu.
Kuhusu utaratibu wa sasa wa kumfanya Gavana wa BoT kuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi (audit committees) kubatilishwa, kamati hiyo ilisema kuwa suala hilo ni la kisheria, hivyo halitawezekana kwa sasa hadi hapo sheria itakapobadilishwa.
Hata hivyo, kamati hiyo imeshauri kuundwa kwa kamati teule ya Bunge ya kufuatilia suala hilo.
Kamati hiyo ilimuita Balali kutoa ufafanuzi kuhusu hoja kadhaa zilizokuwa zimeainishwa katika ripoti hiyo ya CAG, licha ya ofisi yake kupewa hati safi ya mahesabu.
Hayo yanatokea wakati gavana huyo akiwa ameandamwa na tuhuma za ubadhirifu. Lakini akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Balali alishasema hatojiuzulu wadhifa wake, kwani madai ya ubadhirifu yanayotolewa dhidi yake, ni uzushi na uongo mtupu.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 12, mwaka huu, Balali alisema: “Niko comfortable (muruwa), moyo wangu mweupe, ari yangu ya kazi iko juu, kwani tuhuma hizo ni uongo na uzushi mtupu na siwezi kujiuzulu kwa tuhuma zisizo na ushahidi.”
Ingawa hakutaja majina ya anaowatuhumu alipokutana na waandishi, Balali alisema tuhuma hizo zilizosambazwa kwenye mtandao wa intaneti, zimetokana na watu wenye ugomvi wa kibiashara na kusisitiza kuwa ni uzushi usio na chembe ya ushahidi.
“Tuhuma zote dhidi yangu ni za uongo mtupu. Kwanza sijui zimetoka wapi, nani mtunzi na kwanini amefanya hivyo, hilo tunawaachia wanaofanya uchunguzi na naamini siku moja atajulikana na ukweli utajulikana, lakini mimi siwezi kujiuzulu kwa mambo ya uzushi,” alisisitiza.
Aliwahusisha wafanyabiashara wakubwa na tuhuma hizo dhidi yake na kusema kuwa, wafanyabiashara hao wamekuwa na mikakati yao ya kibiashara kama walivyozoea zamani licha ya serikali kufanya mageuzi makubwa kiuchumi.
Alisema hivi sasa BoT imekuwa makini kuwabana wafanyabiashara wanaokopa kwenye mabenki makubwa ili walipe madeni yao, jambo ambalo zamani halikufanyika, kwani walikopa bila kurejesha mikopo, lakini sasa BoT imeamua kuwabana, jambo ambalo limewafanya wajenge chuki kati yao na BoT.
Kutokana na tuhuma hizo, Waziri Meghji wakati akifanya majumuisho ya hoja yake, alisema serikali imeagiza kuanza kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika akaunti ya madeni ya biashara ya nje zinazoikabili BoT.
Alikiri serikali kupata taarifa za kuwapo kwa vitendo vya rushwa na nyingine za matumizi mabaya ya fedha katika Benki Kuu.
Waziri Meghji alisema, tayari alikuwa ameshamwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali, kuanza uchunguzi kuhusu tuhuma hizo.
Alisema, serikali ilikuwa ikitarajia kukamilisha kazi hiyo na taarifa kamili ya uchunguzi huo kutangazwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.