Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Waraka wa siri washtua vigogo wa polisi
Waraka wa siri washtua vigogo wa polisi
By Marshy Abdu | Published  07/25/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Waraka wa siri washtua vigogo wa polisi
na Waandishi Wetu


WARAKA wa siri unaoonyesha kupanda kwa viwango vya mishahara kwa askari polisi kuanzia wale wenye vyeo vya chini hadi vya juu uliolifikia Tanzania Daima mwishoni mwa wiki iliyopita, umesababisha mtafaruku mkubwa ndani ya jeshi hilo.

Habari za uhakika kutoka ndani ya jeshi hilo zinaeleza kwamba, waraka huo ambao unatumiwa na baadhi ya askari kuwa kigezo cha serikali kuwasahau polisi, umesababisha kuanza kwa uchunguzi wenye lengo la kujua kiini cha kuvuja kwake.

Ofisa mmoja wa juu wa polisi aliyezungumza na Tanzania Daima, alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa waraka huo ulinyofolewa kutoka katika faili mojawapo la siri katika mazingira ambayo hadi hivi sasa bado yamesababisha maswali menngi.

Tukio hilo kwa mujibu wa ofisa huyo limesababisha uchunguzi kuanza, ili kuwabaini wale ambao walihusika katika kuunyofoa waraka huo wa siri kabla ya hatua za kinidhamu juu yao kuchukuliwa.

Hatua hiyo ya polisi inakuja takriban siku tatu tu sasa, tangu gazeti hili katika toleo lake la Jumapili iliyopita liandike habari kuhusu kusambazwa kwa waraka huo wa siri na baadhi ya polisi wa Dar es Salaam.

Ofisa mmoja wa juu wa polisi (jina tunalo) tayari amefika katika chumba cha gazeti hili kwa zaidi ya mara moja akijaribu bila ya mafanikio kufanya kila linalowezekana ili kubaini majina ya polisi wanaosambaza waraka huo.

“Ndugu yangu mhariri tunaomba utusaidie kutueleza kuhusu hawa polisi ambao waliwaletea waraka huo ambao ni classified (wa siri) kwenu…unajua katika jeshi askari wa namna hii ni wasaliti na wanaweza wakafikishwa katika mahakama ya kijeshi wakibainika,” alisema ofisa huyo wa polisi.

Tanzania Daima katika habari kubwa iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho: ‘Si ujambazi hii sasa vita’ iliandika pamoja na mambo mengine kuhusu kuwapo kwa kikundi cha polisi waliokuwa wakisambaza waraka huo wa siri kama njia ya kupinga nyongeza ndogo za mishahara yao.

Polisi waliosambaza waraka huo ambao sasa wanasakwa, wamekuwa wakidai kuwa nyongeza hiyo imekuwa ndogo kulinganisha na hali halisi ya kipato cha askari wa chini ambao wanadai mishahara yao haitoshelezi kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

Kwa mujibu wa polisi hao, hatua hiyo ya kupewa nyongeza kidogo, inaweza kusababisha askari wengi kukata tamaa na hivyo kushindwa kuchukua hatua zinazostahili katika kukabiliana na ujambazi ambao katika siku za hivi karibuni unaonekana kurejea kwa kasi.

Polisi hao waliieleza Tanzania Daima kwamba, tayari baadhi ya askari waliokuwa na mawazo hayo walikuwa wameshafanya kikao kimoja kujadili hali hiyo ambayo waliielezea kuwa ni ya kukatisha tamaa.

Waraka uliosambazwa na polisi hao umeainisha mishahara yote ya polisi, ukitaja nyongeza ya mishahara kwa mwaka jana na mwaka huu wa fedha.

Kwa mujibu wa waraka huo, kiwango cha chini cha mshahara wa polisi kilionekana kufikia sh 135, 070 baada ya kupewa nyongeza ya sh 3,000 kulinganisha na viwango vya mwaka jana.

Aidha, waraka huo unaonyesha pia kwamba kiwango cha juu kabisa cha mshahara katika jeshi hilo, sasa kitakuwa ni sh 1,893,000 kutoka sh 1,760,000 za mwaka jana.

Akizungumza na Tanzania Daima katika mahojiano maalumu ofisini kwake juu ya waraka huo mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, alieleza kushangazwa kwake na hatua ya polisi hao kusambaza waraka huo ambao alikiri kuwa ulikuwa ni wa kweli.

“Waraka huu ni halali na kwamba viwango vya mishahara vilivyoanishwa hapo vimetangazwa baada ya serikali kuongeza posho mbalimbali… sasa sioni kwanini watu wanaamua kusambaza mpaka kwenye magazeti,” alisema DCI Manumba.

Alisema viwango hivyo vimeainishwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo na kwamba vimepitiwa kwenye Idara ya Utawala ya jeshi hilo.

“Haya ni baadhi ya mabadiliko yaliyochukuliwa na serikali katika mchakato mzima wa kuboresha mishahara ndani ya jeshi letu, na mpaka sasa tuko kwenye maboresho makubwa na mapendekezo yote yatakayopatikana yatayawasilishwa serikalini na IGP (Said) Mwema kwa hatua zaidi,” alisema DCI Manumba.

Alisema mpaka sasa serikali imekwishatambua suala la maboresho, hivyo askari wote wanapaswa kuwa na subira wakati mapendekezo zaidi yakifanyiwa kazi.

Kuhusu ujambazi ambao unaonekana kuibuka upya, DCI Manumba alisema kwamba jeshi hilo limejipanga vyema na kwamba majambazi yasifikiri kwamba wamelala.

Mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akihitimisha ziara yake ya kutembelea Kanda Maalumu ya Polisi ya Dar es Salaam, IGP Mwema, aliwataka maofisa wa polisi kuwachukulia hatua polisi wote watakaobainika kufanya kazi kinyume cha miiko ya kazi ya jeshi hilo.


Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.