Serikali imeahidi kutoa kiasi cha shilingi elfu hamsini kwa wahanga wa ajali ya gari la mizigo iliyotokea wilayani Biharamlo na kupelekea vifo vya watu 29 wakiwemo wakazi 12 wa wilaya ya Kibondo.
Taarifa hiyo imetolewa na mbunge wa jimbo la Muhambwe Bw. Felix Ntibenda Kijiko wakati alipotembelea wahanga hao kwa nia ya kuwafariji na kuwapa pole.
Bw. Kijiko akiongea na wahanga hao wiki iliyopita katika vijiji vya Nyagwijima, Kumwambu, Kibondo mjini, Kigaga na Biturana ameeleza kuwa ofisi ya waziri mkuu imeamua kutoa kiasi hicho cha fedha kama sehemu ya rambirambi ya serikali.
Amebainisha kuwa msiba wa takribani watu 12 ni wa sehemu moja ni wa kutisha sana na serikali imepata pigo kubwa kwani waliokufa walikuwa wakichangia pato la taifa kama wafanyabiashara na walipa kodi wa serikali.
Aidha mbunge huyo amewataka wananchi na wafanyabiashara kuwa makini wanapotumia vyombo vya usafiri kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na amewataka kutoa ushirikiano kwa askari wa usalama barabarani.
Wakati huo huo jeshi la polisi wilayani Kibondo limetopa amri kwa wenye magari ya abiria kutojaza abiria kuzidi uwezo wa gari na limeonya juu ya tabia za wenye maroli kupakia abiria na mizigo.
Mkuu wa polisi wa wilaya ya Kibondo Bw. Ramadhani Twaha SSP ametangaza kuwachukulia hatua wamiliki na madereva watakao kiuka sheria za usalama barabarani na amewataka madrev waio na leseni kuacha mara moja kuendesha magari.
Aidha Bw. Twaha amewataka waenda kwa miguu na waendesha baiskeli kuwa makini wawapo barabarani na amekemea vitendo vya ulevi kwa watumiaji wa barabara na vyombo vya usafiri.
Hata hivyo licha ya rai hizo kutolewa na Mbunge wa jimbo la Muhambwe, jeshi la polisi na Mkuu wa wilaya ya Kibondo bado wafanyabiashara wa dagaa na samaki kutoka chato kwenda Kibondo na Mabamba wanajaza mizigo na abiria kuzidi uwezo wa magari yao.
Gazeti la Uhuru wiki hii imeshuhudia wafanyabiashara hao wakiwa wamening’inia juu ya mizigo ya dagaa na samaki na walipohojiwa juu ya vifo vilivyotokea walijibu kuwa ilikuwa bahati mbaya na si sababu ya kujaza mizigo.