MICHEZO ya Mataifa ya Afrika ‘All African Games’ inafikia tamati leo mjini Algiers, Algeria huku Tanzania ikiwa imepata medali moja ya fedha kati ya wanamichezo wake 21 walioiwakilisha.
Licha ya mafanikio hayo finyu, lakini Tanzania kwa mara nyingine tena imeshuhudiwa ikifutwa machozi na mchezo wa riadha katika mashindano makubwa ya kimataifa.
Ni mwaka jana tu, Tanzania iliposhiriki mashindano mengine makubwa duniani ya Jumuiya ya Madola, huko Melbourne, Australia ambako iliambulia medali mbili, moja ikiwa ya dhahabu, zikiwa zimenyakuliwa na wanariadha Samson Ramadhani, medali ya dhabau katika Marathoni na Fabian Joseph shaba katika mbio za mita 10,000.
Mwaka huu, tena hali imejirudia kwenye All African Games, kwa mwanariadha Martine Sulle kunyakua medali ya fedha katika mbio za Nusu Marathoni, medali ambayo ni pekee kwa Tanzania katika michezo hiyo.
Sulle alinyakua medali hiyo Ijumaa iliyopita baada ya kushika nafasi ya pili, baada ya kutumia saa 1:03.01 akitanguliwa sekunde kadhaa na Deriba Merga wa Ethiopia, aliyenyakua medali ya dhahabu baada ya kutumia saa 1:02.24.
Kwa kitendo hicho cha kishujaa cha Sulle, hatuna budi kumpongeza sambamba na Chama cha Riadha Tanzania (RT), ambacho kwa mara nyingine kimedhihirisha umahiri katika kupeperusha vema bendera ya Tanzania kimataifa.
Licha ya ushindi huo kuwa finyu, jambo la kuiondolea aibu Tanzania katika mashindano kwa kutotoka mikono mitupu kama zilivyo nchi nyingine, hatuna budi kumpongeza Sulle na RT kwa ujumla.
Hata hivyo, pongezi hizi zitakuwa hazisaidii, kama jamii kwa ujumla, serikali na wadau mbalimbali kutoupa hamasa na misaada mbalimbali ili uzidi kukua na kufanya vema zaidi ya hivi tulivyozoea.
Si kana kwamba, tunawalaumu wachezaji wa michezo mingine kwa kufanya vibaya katika mashindano hayo na mengineyo yaliyopita, la hasha! Lakini nao wanapaswa kuwa na wivu wa maendeleo na mafanikio huku wakiwa waoga wa kuvurunda.
Tunayasema haya kwa kuzingatia kuwa kwa mchezo au mchezaji kufanya vema, huwa ni fahari kwa chama au mchezaji husika na taifa kwa ujumla kwani ushindi au kushindwa, huwa ni kwa taifa.
Kama hivyo ndivyo, ipo haja kwa wachezaji na vyama kwa ujumla kujipanga upya ili kuwa washindani katika mashindano husika badala ya kuwa wasindikizaji kama ilivyotokea safari hii kule Algeria kwa kuambulia medali moja pekee.
Tukija kwa Sulle na riadha kwa ujumla, hatuna budi sasa kukubali kuwa Tanzania ina hazina kubwa katika riadha na kama tutajipanga vema kwa ajili ya kufanya vema, ninaamini hakuna kitakachoshindikana.
Wakati tukiwakumbusha wachezaji na vyama vya michezo kujipanga upya, serikali kwa upande wake nayo inapaswa kuwajibika kwa sehemu yake ikishirikiana na wadau wake katika kuinua michezo kwa ustawi wa vijana na taifa letu kitaifa na kimataifa.
Kutokana na soka kuwa juu zaidi kuliko mingine, ipo haja kwa serikali na wadau mbalimbali kuelekeza macho yao kwenye michezo mingine pia kama riadha ili kujenga hazina ya wachezaji bora wa kuipeperusha vema bendera ya Tanzania kimataifa.
Riadha kama michezo mingine, ni moja ya ajira bora zaidi kwa vijana wenye vipaji na kuamua kujikita kwenye mchezo huo.
Kushindwa kwa Sulle kuchukua medali ya dhahabu ni changamoto kwetu sote wakiwamo viongozi wa michezo na wachezaji kwa ujumla kujipanga upya ili kuvunja rekodi katika michuano mbalimbali ya kimataifa.
Kadhalika, changamoto si vema ikaishia kwa wanamichezo ambao wameshindwa kunyakua medali kwenye mashindano hayo, bali riadha bado wana nafasi ya kufanya vema kwenye michuano wanayoshiriki mara kwa mara ya kimataifa, ikiwamo ya dunia huko Tokyo, Japan hivi karibuni.
Kwa mara nyingine, tunampongeza Sulle kwa kututoa tongotongo kwenye michuano hiyo angalau tumepata medali moja inayotuweka ndani ya ramani ingawa tuko pembeni kama si chini.
Juhudi zifanyike kwa wadau wote kuhakikisha kwamba tunatoka mafichoni na kujikita katikati kama si juu ya kilele katika medani zote za michezo kwa manufaa ya wachezaji wetu na taifa kwa ujumla.
Tunamaliza kwa kusema, hongera Sulle, ingawa ipo haja ya kujipanga zaidi kwani ni aibu Tanzania kuambulia medali moja katika michuano ya Algeria