Kibondo
Mwananfunzi mmoja wa shule ya sekondari Maragalasi wilayani Kibondo amefanikiwa kuunganisha mitambo na kurusha matangazo ya radio katika eneo la Kibondo mjini.
Mwanafunzi huyo Eliud Kajuna mwenye umri miaka 20 anayesoma kidato cha nne akihojiwa na radio Kwizera amesema alifanikiwa kurusha matangazo yake mwezi april wakati akisherehekea sikikuu ya pasaka mwaka huu.
Amesema yeye ni mtoto wa fundi mitambo hususani radio na saa na kwa kuishi na mzazi wake amekuwa akiona kazi hizo na kutamani kujifunza fani hiyo na kwamba amekuwa akipata fursa ya kufanya majaribio.
Bw. Kajuna amebainisha kuwa yeye licha ya kjifunza masomo ya sayansi amekuwa na hamu kubwa ya kufanya kazi za utangazaji na ufundi hali iliyomsukumu kubuni chombo cha matangazo.
Akaielezea jinsi alivyofanikiwa kurusha matangazo yake kwa mawimbi ya FM 108.00MHZ amesema alibadilisha mfumo wa radio za kawaida kupokea na kuiwezesha kurusha matangazo yake.
Mwanafunzi huyo amesema mpango wake ni kuendelea kujifunza zaidi ili afanikiwe kuanzisha kituo chake cha radio kwa lengo la kuwasaidia watoto wengine wenye vipaji mbalimbali.
Aidha kijana huyo anaomba msaada kwa wadau wa maendeleo ili afanikiwe zaidi katika ubunifu wake hususani kielimu na vifaa vya kufanyia majaribio.